Apr 17, 2018 10:35 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (35)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 35.

Kwa wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba harakati za kuzusha mifarakano katika safu za Waislamu hazihusiani na Masuni tu kupitia matapo ya Kisalafi na Kitakfiri. Miongoni mwa Mashia pia kuna watu na makundi yanayochochea na kukoleza moto wa hitilafu na uadui baina ya Waislamu kwa kuwavunjia heshima viongozi wakubwa wa dini ya Uislamu na masahaba wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Tukatoa mfano kwa kuashiria hatua chafu na ambayo haihalalishiki wala haiwezi kutetewa ya mtu mmoja aliyevalia vazi la alimu wa dini wa Kishia ambaye aliwahi kusimama mbele ya chombo cha habari na kutoa maneno ya kashfa na ya kumvunjia heshima mke wa bwana Mtume SAW bibi Aisha ambaye anaheshimika mbele ya Ahlu-Sunnah. Tukatanabahisha kwamba katika zama hizi ambapo ulimwengu mzima wa kikoloni umepanga safu kukabiliana na Uislamu, lengo lake likiwa ni kuufuta Uislamu, hatua hiyo na harakati nyenginezo za kimatapo na kimadhehebu zenye lengo la kuzitumbukiza kwenye mizozo na machafuko jamii za Kiislamu, bila shaka ni fimbo na silaha ya kikoloni; na kwa sababu hiyo Ushia wa Kiingereza ni jina mwafaka inalostahiki kupewa harakati hiyo.

Pamoja na hayo tusisahau na kughafilika na mchango chanya na wa kuleta umoja uliotolewa na baadhi ya shakhsia na duru zenye uelewa wa kidini na kisiasa kuzima njama hizo na juhudi zilizofanywa kwa madhumuni ya kuimarisha umoja baina ya Waislamu. Kwa mfano katika hatua ya kuelimisha fikra za Waislamu, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, akiwa ni Marjaa-Taqlidi wa Kishia ametoa fatua ya kudumu na ya kihistoria ambayo imetokana na jawabu yake kwa suali aliloulizwa na maulamaa wa Kishia wa nchini Saudi Arabia ambao walitaka kujua hukumu ya kumtusi na kumvunjia heshima Bibi Aisha, mke wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Katika fatua yake hiyo, Ayatullah Khamenei anasema: "kuzivunjia heshima nembo za ndugu (zetu) wa Ahlu Sunnah ikiwemo kumzushia tuhuma mke wa Mtume (bibi Aisha) ni haramu. Suala hili linajumuisha wake wa Mitume wote hususan Bwana wa Manabii, Mtume mtukufu Muhammad SAW.

 

Fatua hii imepokelewa vizuri sana na kwa wingi katika Ulimwengu wa Kiislamu ikiwemo Chuo Kikuu cha kidini cha Al-Azhar cha Misri, vyuo vikuu vya nchi za Kiarabu pamoja na shakhsia mashuhuri wa Kiislamu wa kila pembe ya dunia na hivyo kuhitimisha na kuzima moto wa kuzusha machafuko ya kimadhehebu katika jamii za Kiislamu. Marjaa Taqlidi wengine wakubwa wa Kishia kama Ayatullah Makarim Shirazi, Ayatullah Sayyid Sadiq Rouhani na wanafikra wa vyuo vya kidini vya Kishia (Hawza) nao pia waliunga mkono fatua hiyo.

Katika upande wa pili, katika hatua inayostahili pongezi, chuo cha Al-Azhar kilichukua hatua ya kuwaalika maulamaa wakuu wa Kishia kutembelea chuo hicho. Hatua hiyo ya Al-Azhar ilipokelewa kwa radiamali na hisia tofauti. Miongoni mwa radiamali hizo ni msimamo ambao ulichukuliwa na maulamaa wa kitakfiri; hata hivyo Sheikh Abbas Shuman, Naibu Mkuu wa Chuo cha Al Azhar alieleza kwamba kuipokea fatua hiyo ni jambo la dharura na kubainisha kwamba: "madhehebu ya Shia ni moja ya madhehebu za Kiislamu; na Mashia ni Waislamu. Al Azhar haimkufurishi Muislamu yeyote; kituo hichi cha Kiislamu kinawatambua Shia Imamiyyah na Zaydiyyah kama madhehebu mbili miongoni mwa madhehebu za Kiislamu; na hadi sasa kuna tasnifu nyingi ambazo zimeandikwa katika ngazi ya Uzamili na Uzamivu kuhusu madhehebu hizo na zinapatikana kwenye maktaba za Al Azhar."

Ukweli huu, kwamba Mashia ni kundi moja kati ya makundi ya Waislamu umekubaliwa na maulamaa wote wa Al Azhar; na kualikwa maulamaa wa Kishia kwa ajili ya kikao cha pamoja kumefanywa ili kutilia mkazo jambo hilo.

Kongamano la Umoja wa Kiislamu mjini Tehran, Iran

 

Wapenzi wasikilizaji, kama tulivyotangulia kueleza katika vipindi vilivyopita, tunu na thamani za pamoja za Waislamu wote za kuwa na Mtume mmoja, kibla kimoja na kuitakidi kuwa kitabu chao cha Qur'ani kimetakasika na kuongezwa au kupunguzwa chochote kile ndani yake ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuwa msingi wa umoja baina ya nchi za Kiislamu. Hakuna shaka yoyote kwamba haitoyumkinika kujenga umoja wa aina yoyote ile na kuweza nchi za Kiislamu kuwa na mtazamo na muelekeo mmoja bila ya kuzingatia na kushikamana na usuli na misingi hii ya pamoja. Isitoshe, masuala mengine ya kuleta umoja kama manufaa na maslahi ya pamoja ya kiuchumi na kisiasa hayawezi kuwa msingi imara na wa kutegemewa kwa ajili ya kuzifanya nchi za Kiislamu ziwe kitu kimoja, kwa sababu hakuna adui na rafiki wa kudumu katika uchumi na siasa; bali kutokana na kubadilika mazingira, waitifaki, maadui na washindani wa mataifa nao pia hubadilika. Kwa msingi huo, umoja wa aina yoyote ile katika Ulimwengu wa Kiislamu inapasa ujengeke juu ya misingi hiyo tuliyoitaja.

Wapenzi wasikilizaji, kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki sina budi kuishia hapa kwa leo hadi tutakapokutana tena inshallah wiki ijayo katika siku na saa kama ya leo ili kukuleteeni sehemu ya 36 ya mfululizo huu. Nakuageni basi hadi wakati huo na kukutakieni kila la heri maishani

Tags