Apr 17, 2018 13:00 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (36)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 36.

Kwa wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki, bila shaka mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba, tunu na thamani za pamoja za Waislamu wote za kuwa na Mtume mmoja, kibla kimoja na kuitakidi kuwa kitabu chao cha Qur'ani kimetakasika na kuongezwa au kupunguzwa chochote kile ndani yake ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuwa msingi wa umoja baina ya nchi za Kiislamu. Na tukabainisha kuwa haitoyumkinika kujenga umoja wa aina yoyote ile na kuweza nchi za Kiislamu kuwa na mtazamo na muelekeo mmoja bila ya kuzingatia na kushikamana na usuli na misingi hiyo ya pamoja. Aidha tukaashiria kuwa masuala mengine ya kuleta umoja kama manufaa na maslahi ya pamoja ya kiuchumi na kisiasa hayawezi kuwa msingi imara na wa kutegemewa kwa ajili ya kuzifanya nchi za Kiislamu ziwe kitu kimoja, kwa sababu hakuna adui na rafiki wa kudumu katika uchumi na siasa; bali kutokana na kubadilika mazingira, waitifaki, maadui na washindani wa mataifa nao pia hubadilika. Kwa msingi huo, umoja wa aina yoyote ile katika Ulimwengu wa Kiislamu inapasa ujengeke juu ya misingi hiyo tuliyoitaja.

 

Lakini pamoja na hayo, kuna suali linaloweza kutupitikia akilini mwetu; nalo ni kwamba usuli na misingi hii ya pamoja imekuwepo muda wote tangu ulipodhihiri Uislamu karne kumi na nne zilizopita. Kama ni hivyo, kwa nini misingi hii haijawezesha kupatikana umoja na kuwepo muelekeo wa pamoja kati ya nchi za Kiislamu; bali kadiri muda unavyopita mifano hai na vielelezo vya mifarakano na utengano vimezidi kuongezeka kati ya nchi hizo? Suali hili linatupeleka kwenye nukta muhimu sana na ya msingi; nayo ni kwamba, ni sawa kabisa kwamba umoja na mshikamano wa aina yoyote kati ya nchi za Kiislamu inapasa usimame juu ya misingi na thamani za pamoja tulizoashiria hapo kabla, lakini chimbuko la migongano na mifarakano inayoshuhudiwa katika Ulimwengu wa Kiislamu badala ya kusababishwa na misingi hiyo, zaidi inatokana na masuala yasiyokuwa hayo kama maslahi ya kikabila, yanayozingatia asili za watu, ya kiuchumi na ya kisiasa ya nchi hizo. Kwa maneno mengine, mambo ya pembeni na ya kando, ambayo Bwana Mtume Muhammad SAW alikuwa akiyatolea tahadhari kuwa yanaweza kufufuliwa na kujitokeza ndani ya jamii ya Kiislamu yameshuhudiwa kwa sura tofauti katika historia ya nchi za Kiislamu na kusababisha mifarakano na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Nukta hii ina umuhimu mkubwa kwa sababu kama tutataka kuwa na umoja katika mazingira ya mahala na zama hizi za sasa inapasa tuyazingatie hayo masuala yasiyo ya usuli; na baada ya kutambua hali zote mbili zinazochangia kuzuka mifarakano na zinazoshajiisha kupatikana umoja tufanye kazi ya kufuatilia suala la umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu.

*********

Nukta hii wapenzi wasikilizaji haimaanishi kwamba tufumbie macho kuwa na umoja na kukurubiana katika masuala ya kimadhehebu, kifikra na kiitikadi bali maana yake ni kwamba sambamba na kuimarisha misingi inayoleta umoja katika usuli na thamani za msingi, inatakiwa tuzingatie na kuzipa umuhimu pia sababu za pembeni. Na kwa msingi huo tunaweza kuthubutu kusema kwamba hata ikiwa usuli na misingi mikuu ya Uislamu ya kujenga umoja itaimarishwa katika nchi za Kiislamu, kufanya hivyo ni jambo la lazima lakini halitoshi kwa ajili ya kuufanya Ulimwengu wa Kiislamu uwe na muelekeo mmoja. Kwa maneno mengine ni kwamba misingi na thamani za pamoja za Uislamu ni sharti la lazima kwa ajili ya kufikiwa umoja kati ya nchi za Kiislamu, lakini peke yake halitoshi. Sharti kamilishi linapatikana kwa kuyafuta au kuyahafifisha mambo yanayochochea mifarakano na kuyapa nguvu mambo yanayoimarisha umoja. Kwa sababu hiyo pamoja na kuwepo thamani za pamoja na kufanyika jitihada ya kuziimarisha, kuna haja pia ya kuyafuta au kuyahafifisha mambo yanayosababisha mifarakano na utengano. Kufanya hivyo kutaleta tija maridhawa kwa ajili ya umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu.

Katika kuzihakiki sababu na mambo yanayosababisha mifarakano na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu, tunaweza kuyagawa mambo na sababu hizo katika sehemu mbili za ndani ya ulimwengu wenyewe wa Kiislamu na za nje ya ulimwengu huo. Baadhi ya matatizo ya ndani yanahusiana na mifarakano na migawanyiko ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu na baadhi ya mengine yanatokana na uingiliaji na ulaji njama unaofanywa na maajinabi na maadui wa Uislamu. Kwa mujibu wa rai na mitazamo ya wanafikra na warekebishaji umma na kulingana na tajiriba na uzoefu wa kihistoria wa nchi za Kiislamu tunaweza kuutaja utaifa na udikteta wa watawala kuwa ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi zinazochochea mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Utaifa ni kadhia inayohusishwa na zama za sasa hususan kuanzia enzi za Renaissance, yaani kipindi cha mwamko wa Sanaa barani Ulaya hadi wakati huu. Zama hizo zinajulikana kama zama za Ubinafsi kwa kimombo Indivisualism, yaani kumfanya mtu binafsi ndio asili ya kila kitu na kuvuvumka hisia na uelewa wa mtu binafsi dhidi ya mashinikizo ya kimakundi na kijamii. Mwanadamu wa zama mpya ametupilia mbali thamani za kijamii za zama zake na kuweka thamani na tunu nyengine mpya pahala pake. Katika kipindi hicho dola kuu la mamlaka ya Kikristo lilivunjwa na kusambaratika na badala yake zikaundwa dola na tawala za utaifa. Niccolò Machiavelli, mwananadharia wa Kitaliano, ni miongoni mwa wanafikra walioasisi nadharia ya uundaji wa serikali na kuporomoka dola kuu la Ukristo. Kwa kutenganisha maadili na siasa, Machiavelli alikuwa akiitakidi kuwa kuunganisha na kuunda Serikali ya Taifa yaani Nation State ndio njia pekee ya kuiokoa Italia na fujo na hali ya mchafukoge.

Ukiondoa mijadala ya kinadharia, kwa muhtasari tunaweza kuielezea fikra ya Utaifa, yaani Nationalism kuwa ni hisia za jamii ya watu wenye asili maalumu, lugha maalumu, utamaduni maalumu au kaumu maalumu kuwa na mfungamano na ardhi yenye mipaka maalumu. Katika baadhi ya vipindi vya historia, Utaifa ulitumika kuzipa nchi nguvu na uwezo, na katika baadhi ya vipindi ulisaidia kujikomboa nchi zilizokuwa kwenye pingu na minyororo ya Ukoloni. Katika miaka ya baada ya Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, kwa kutegemea Utaifa, mataifa mengi yaliweza kujikomboa na kuondokana na unyonyaji wa madola ya kikoloni. Pamoja na hayo, kuna baadhi ya zama, ambapo Utaifa ulikuwa sababu ya kuzuka vita vya umwagaji damu kati nchi mbalimbali. Suali la kujiuliza hapa ni hili: kuna uhusiano gani kati ya Utaifa na fikra ya Kiislamu, na je Utaifa umekuwa na nafasi gani katika kuwaunganisha au kuwatenganisha Waislamu? Kutokana na kumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki, jibu suali hili tutakuja kulitoa inshallah katika kipindi chetu kijacho. Basi hadi siku nyengine na katika kipindi kingine cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu nakuageni huku nikikutakieni kila la kheri maishani.

Tags