Apr 17, 2018 13:08 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (38)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 38.

Katika sehemu ya 36 na 37 za kipindi hiki tulieleza kuwa Utaifa na udikteta wa watawala katika mataifa ya Waislamu ni mambo mawili makuu miongoni mwa sababu za ndani zilizosababisha mpasuko na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika kipindi chetu cha leo tutaashiria mifano kadhaa ya tajiriba zilizoshuhudiwa katika Ulimwengu wa Kiislamu zinazoonyesha kuwa Utaifa umetoa mchango hasi na haribifu wa kusababisha mifarakano kati ya nchi za Kiislamu. Kisha baada ya hapo tutagusia maudhui ya pili, yaani nafasi ya tawala za kiimla na kidikteta katika suala hilo.

Tajiriba na mfano wa kwanza wa taathira hasi na mbaya ya Utaifa kwa umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu inahusiana na kugawanywa dola kuu la Kiislamu katika sehemu tatu za Waarabu, Waajemi au Wairani na Waturuki. Sambamba na mabadiliko yaliyojiri katika uhusiano wa Kanisa na wafalme na kujitokeza Dola la Utaifa, yaani Nation-State huko Magharibi, mageuzi makubwa na ya kina yalishuhudiwa pia katika dola kuu la Kiislamu, ambayo yalisababisha kuporomoka dola hilo na kujitokeza vuguvugu na harakati za utaifa katika sehemu hiyo ya dunia. Hadi kabla ya hapo, dini ya Uislamu ilikuwa haijawawekea mpaka wowote watu waliosilimu; na kila Muislamu aliyekuwa akisafiri kutoka mahali alikozaliwa na kuelekea mji wowote ule wa ardhi za Waislamu alikuwa akiiona ardhi na eneo hilo kuwa ni wat’ani na nchi yake. Lakini baada ya hujuma na uvamizi uliofanywa na Wamongolia na Wataimuri na kusambaratika misingi ya Ukhalifa wa Bani Abbasi huko Baghdad, dola kuu la Kiislamu liligawanywa katika sehemu tatu za Waarabu, Wairani na Waturuki.

Hatukukutuma ewe Muhammad ila uwe rehema kwa viumbe wote

 

Tajiriba nyengine ya athari hasi za Utaifa ilishuhudiwa katika kipindi cha mwanzoni mwa karne ya 19. Katika zama hizo Utaifa uliovuvumka kutokana na Mapinduzi ya Ufaransa na fasihi yake ya hisia za njozi na utiaji chumvi ulikuwa ndio chachu kuu ya harakati za upinzani wa ndani zilizojitokeza dhidi ya Dola la Othmaniyyah. Kwa ujumla ni kwamba wapenda mageuzi wa kile kilichojulikana kama “Waothmaniyya Wapya” walioutumia Utaifa wa Kituruki na fikra ya mielekeo ya Kiothmaniyya, sambamba na propaganda za Wamishionari wa Kikatoliki na makanisa, hali mbaya na isiyoridhisha ya ndani na utumaji majeshi nje ya mipaka ya dola hilo, yote hayo yalichangia na kuandaa mazingira ya kusambaratika na kuporomoka dola kuu la Othmaniyya. Uasi wa Wabulgaria, vita baina ya Urusi na dola la Othmaniyya, uhusiano wa dola hilo na mataifa ya Kikristo ya eneo la Balkan, kujitenga Bulgaria, Serbia, Romania na Montenegro na utawala wa Othmaniyya pamoja na kujitokeza vuguvugu la Umajimui wa Waarabu yaani Pan-Arabism yalikuwa miongoni mwa matokeo ya kuporomoka dola la Othmaniyya. Katika kipindi hicho, Utaifa, iwe ni wa sura ya Umajimui wa Waturuki, Pan-Turkism au wa Umajimui wa Waarabu, Pan-Arabism, ulianza taratibu kubadilika kutoka katika hali ya kifikra na kiutamaduni na kuchukua muelekeo wa kisiasa na kijamii; lakini kuenea kwake kulikuwa ni kwa sura isiyo endelevu ya jibu na radiamali dhidi ya ukoloni wa Magharibi; na tena basi ni katika baadhi ya masuala tu na katika kipindi na awamu maalumu.

*********

Tajiriba nyingine inahusiana na kipindi cha mwishoni mwa karne hiyo. Katika kipindi hicho, ndani ya dola la Othmaniyya, Sultan Abdulhamid wa Pili alijaribu kuhamasisha hisia na itikadi za kidini kwa lengo la kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Lakini wakati huohuo harakati na vuguvugu la Vijana Waturuki liliendeleza fikra na harakati ya Waothmaniyya Wapya kwa kuasisi kamati ya Umoja na Maendeleo, ambapo katika mwaka 1889, waliratibu mkakati wa kumwangusha Sultan Abdulhamid wa Pili. Miongoni mwa hatua walizochukua ni kuchapisha gazeti lililoitwa Mashauriano lililofanya kazi ya kuhamasisha hisia za Utaifa wa Waturuki na kuleta umoja na mshikamano baina yao. Walianzisha mawasiliano na uhusiano wa siri na Mustafa Kamal Pasha na kupitisha mpango wa kutumia nguvu kwa lengo la kuuangusha utawala wa Othmaniyya kwa njia ya kuhamasisha uasi dhidi ya Sultan Abdulhamid wa Pili. Kutokana na harakati hiyo, fikra zake za kuleta Umajimui wa Waislamu, Pan-Islamism ziligonga mwamba, na hatimaye mwaka 1908 akapinduliwa na kuondolewa madarakani.

Katika kile kilichokuwa kama hisia za Waarabu kuhusiana na Utaifa wa Kituruki, kulikuwepo na wasiwasi kwamba utambulisho wao wa kiutamaduni usije ukasombwa na kufutwa na dhoruba ya mawimbi ya Umajimui wa Kituruki. Kwa sababu hiyo wanafikra wa Ulimwengu wa Kiarabu wakajiwa na wazo la kuasisi jumuiya mbalimbali kwa lengo la kulinda haki na utambulisho wa Waarabu na kuanzisha Umajimui wa Waarabu, yaani Pan-Arabism. Kwa juhudi zilizofanywa na shakhsia kadhaa akiwemo Najib Azuri za kuasisi "Jumuiya ya Ukereketwa kwa Wat'ani wa Kiarabu", jiwe la msingi wa mielekeo ya utaifa wa Kiarabu wa kukabiliana na harakati ya Turani liliwekwa rasmi. Harakati na vuguvugu hilo liliendelezwa katika nusu ya pili ya karne ya ishirini kwa fikra za watu kama Michel Aflaq na kubuniwa mielekeo ya kikaumu ya Kiarabu iliyotilia mkazo sha'ar na kaulimbiu ya "umma mmoja wa Kiarabu wenye kazi moja ya kudumu daima dawamu".

 

Mnamo karne ya ishirini pia mavuguvugu ya Utaifa yalishadidisha mpasuko na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika nusu ya mwanzo ya karne hiyo zilijitokeza nchi au taasisi za utaifa katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kuanzia Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia na kuendelea, Waarabu Waislamu walianza kidogo kidogo kugawanywa katika taasisi za kitaifa za kujitegemea, na baada ya kujitokeza nchi kama Iraq, Jordan, Saudi Arabia, Lebanon, Syria, Misri, Libya, Tunisia na Algeria walianza kushindana na kufanyiana uadui wenyewe kwa wenyewe. Kwa upande mwengine, tawala za nchi ndogo ndogo za kifalme za kwenye pwani ya Ghuba ya Uajemi kama Kuwait na Qatar zilitengana, na kila moja ikabaki peke yake. Bangladesh ilitengana na Pakistan, wakati Pakistan nayo ilikuwa imeshatangulia kujitenga na India. Nchi za pwani ya Afrika Mashariki pia ambazo nyingi zao zilikuwa na idadi kubwa ya Waislamu zilibadilishwa kuwa nchi ndogo ndogo, kila moja ikiwa ni taifa linalojitawala; na kwa njia hiyo umma wa Kiislamu ukawa umegawanyika vipande vipande. Hata ndani ya nchi zenyewe pia, hisia za utaifa wa kikaumu zilihamasishwa na kutiliwa nguvu, kiasi kwamba kaumu za Waturuki, Wakurdi, Waarabu, Mabulushi na wengineo waliokuwa wakiishi katika nchi moja zikawa na uadui baina yao na kugeuka makundi yanayojitenga na kujiweka mbali na serikali kuu. Kwa utaratibu huo utambulisho wa utaifa na ukaumu ukapata nguvu zaidi na kuufuta utambulisho wa kidini na umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu.

Wasikilizaji wapenzi, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo umemalizika, hivyo sina budi kuishia hapa huku nikitumai kuwa mumeelimika na kunufaika na yote mliyoyasikia katika mfululizo huu. Tutakutana tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo, katika sehemu ya 39 ya kipinid hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags