Apr 17, 2018 13:12 UTC
  • Waislamu wa nchini Brazil
    Waislamu wa nchini Brazil

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 39.

Kwa wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila ya shaka mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulisema kuwa Utaifa na udikteta wa watawala katika mataifa ya Waislamu ni mambo mawili makuu miongoni mwa sababu za ndani zilizosababisha mpasuko na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu, ambapo katika kipindi hicho tulitoa mifano ya tajiriba kadhaa zilizoshuhudiwa katika Ulimwengu wa Kiislamu zinazoonyesha kuwa Utaifa umetoa mchango hasi na haribifu wa kusababisha mifarakano kati ya nchi za Kiislamu. Uimla wa watawala, nao pia kama ulivyo Utaifa ni sababu nyengine iliyochochea na kuleta mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Kama mtakuwa mngali mnakumbuka, katika vipindi kadhaa vya huko nyuma tuliwahi kudokeza kwamba kwa mtazamo wa wanafikra na warekebishaji umma wengi wa Ulimwengu wa Kiislamu kama Sayyid Jamaluddin Asad Abadi na Abdurahman Al Kawakibi, udikteta na tawala zisizotokana na ridhaa ya wananchi zimekuwa moja ya vizuizi vya kupatikana umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Sayyid Jamaluddin alikuwa akiitakidi kwamba tawala zisizo za kidikteta huzibadilisha taasubi za kikaumu na kimbari ambazo husababisha hitilafu na mifarakano, kuwa taasubi za kidini na wenzo wa kushikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu na kuleta upendo na mshikamano katika jamii. Naye Al Kawakibi, kama alivyokuwa Sayyid Jamaluddin alikuwa akiamini kwamba kukosekana uelewa wa kisiasa miongoni mwa Waislamu, ambao matokeo yake ni kujitokeza tawala za kidikteta ndio sababu ya kubaki nyuma kimaendeleo nchi za Kiislamu. Kwa kutilia mkazo juu ya nukta hiyo ya udikteta wa ndani Abdurahman Al Kawakibi alikuwa akilielezea suala hilo kuwa ndilo tatizo kuu la jamii za Kiislamu. Na kwa sababu hiyo alikuwa akisisitiza kwamba udikteta wa watawala ndio sababu ya utengano, mifarakano na kubaki nyuma kiustawi na kimaendeleo Ulimwengu wa Kiislamu.

Waislamu wa nchini Tanzania

 

Kuna kesi na mifano mingi katika historia ya nchi za Kiislamu inayoonyesha udikteta wa watawala ulivyochangia kuleta au kushadidisha mpasuko na mgawanyiko katika Ulimwengu wa Kiislamu. Lakini kabla ya kuzungumzia kesi na mifano hiyo ni vyema tukafahamu kwanza kwamba msamiati wa uimla au udikteta, kama ilivyo misamiati na istilahi nyingine za Sayansi ya Siasa ni tata na zina mjadala wa kiwango fulani. Kwa sababu hiyo si rahisi kutoa tafsiri kamilifu ya udikteta na inayoridhiwa na kukubaliwa na watu wote. Kwa mfano haijulikani ni kiwango gani cha mbinyo, utumizi wa nguvu na ukandamizaji wa utawala au mtawala na uhodhi na ukiritimba wake ni dhihirisho na kielelezo cha uimla na udikteta. Kwa sababu, vyovyote iwavyo katika kila jamii huwepo na serikali; na mbinyo na utumiaji nguvu ni mambo ambayo kila serikali inalazimika kuyafanya, kwa sababu uendeshaji wa masuala ya nchi unahitaji kutumia nguvu na madaraka. Lakini suali ni, kitu gani kinazipambanua na kuzitafautisha tawala za kidikteta na zile zisizo za kidikteta na za kidemokrasia?

Tunapotaka kupambanua tawala za kiimla na zile za kidemokrasia inapasa tuzingatie kwanza misingi miwili mikuu. Kwanza ni kwamba tawala za kiimla huwa zinaingia madarakani kwa mbinu za utumiaji nguvu na zisizotokana na msukumo wa wananchi. Kwa maneno mengine ni kwamba tawala za aina hii huwa mara nyingi haziingii madarakani kwa njia ya uchaguzi. Na msingi wa pili ni kuwa katika mifumo ya tawala hizi, kwa kawaida madaraka yanakuwa yamehodhiwa na mtu mmoja au chama maalumu; na kwa hivyo maamuzi mengi yanayopitishwa hutegemea matakwa na nia ya mtu au chama kinachotawala; ni kwa sababu hiyo katika mifumo hiyo haki za kiraia, kijamii na kisiasa huwa hazina uthabiti; na maamuzi yanayochukuliwa, badala ya kutokana na maoni ya wananchi huwa zaidi yanatokana na matakwa na yanazingatia maslahi ya mtawala dikteta au chama chake tawala. Mifumo ya tawala za kidikteta duniani inatafautiana katika aina za idiolojia zao, kuwa kwao udikteta wa kijeshi au wa kiraia, ukubwa wa udikteta wa kila utawala na nyenzo zilizotumia kufikia madarakani; lakini takribani misingi hiyo miwili tuliyoiashiria, inashuhudiwa katika mifumo yote ya tawala za kidikteta iliyoko ulimwenguni.

Mwito wa Umoja

 

Kwa ushahidi wa historia, kuwepo mifumo ya aina hii ya kisiasa ya kidikteta na isiyotokana na ridhaa ya wananchi katika Ulimwengu wa Kiislamu kumekuwa kizuizi cha kupatikana mshikamamo na msimamo mmoja baina ya nchi za Kiislamu, kwa sababu katika mifumo hii ya utawala, kwanza, matakwa na irada ya viongozi wanaotawala huwa haiendani na matakwa na matilaba ya wananchi; na viongozi hao huwa hawahisi kama kuna haja ya kuimarisha mfungamano baina ya nchi yao na nchi nyengine za Kiislamu. Lakini pili, tawala hizi huwa hazina uhalali wa kisiasa kwa mtazamo wa wananchi. Kwa sababu hiyo matamanio na malengo makuu ya tawala hizo huwa tofauti na yale ya wananchi. Ni wazi kwamba katika mifumo ya aina hii, hata kama wananchi wenyewe wa mataifa ya Waislamu watakuwa na hamu ya kuwa na ushirikiano kwa ajili ya amani na maslahi yao, kutokana na serikali zinazotawala katika mataifa hayo kukosa uhalali wa kisiasa wa kutawala na kutokuwa tayari kuakisi maoni ya wananchi katika uga wa kisiasa wa ndani na wa kimataifa, huwa haziko tayari kuliunga mkono na kulipa msukumo wazo hilo. Lakini tatu ni kwamba katika mifumo ya tawala za kiimla, kutokana na mwenendo wa kidikteta, wa kiumimi na usio wa Kiislamu wa watawala, wananchi huwa hawana imani tena ya kushirikiana na watawala hao. Na kwa sababu hiyo umoja wa Kiislamu hutoweka kutokana na wananchi kupoteza imani kwa watawala wa nchi zao.

 Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo umemalizika, hivyo sina budi kuishia hapa lakini nikiwa na matumaini kwamba mtajiunga nami tena inshaaAllah juma lijalo katika siku na saa kama ya leo katika mfululizo mwengine wa kipindi hiki. Basi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni usikilizaji mwema wa sehemu iliyosalia ya matangazo yetu.

Tags