Apr 17, 2018 13:15 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (40)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 40.

Katika kipindi kilichopita tulisema kuwa kwa ushahidi wa historia, kuwepo mifumo ya kisiasa ya kidikteta na isiyotokana na ridhaa ya wananchi katika Ulimwengu wa Kiislamu kumekuwa kizuizi cha kupatikana mshikamano na msimamo mmoja baina ya nchi za Kiislamu, kwa sababu katika mifumo hiyo ya utawala, kwanza, matakwa na irada ya viongozi wanaotawala huwa haiendani na matakwa na matilaba ya wananchi; na viongozi hao huwa hawahisi kama kuna haja ya kuimarisha mfungamano baina ya nchi yao na nchi nyengine za Kiislamu. Lakini pili, tawala hizi huwa hazina uhalali wa kisiasa kwa mtazamo wa wananchi. Kwa sababu hiyo matamanio na malengo makuu ya tawala hizo huwa tofauti na yale ya wananchi. Ni wazi kwamba katika mifumo ya aina hii, hata kama wananchi wenyewe wa mataifa ya Waislamu watakuwa na hamu ya kuwa na ushirikiano kwa ajili ya amani na maslahi yao, kutokana na serikali zinazotawala katika mataifa hayo kukosa uhalali wa kisiasa wa kutawala na kutokuwa tayari kuakisi maoni ya wananchi katika uga wa kisiasa wa ndani na wa kimataifa, huwa haziko tayari kuliunga mkono na kulipa msukumo wazo hilo. Lakini tatu ni kwamba katika mifumo ya tawala za kiimla, kutokana na mwenendo wa kidikteta, wa kiumimi na usio wa Kiislamu wa watawala, wananchi huwa hawana imani tena ya kushirikiana na watawala hao. Na kwa sababu hiyo umoja wa Kiislamu hutoweka kutokana na wananchi kupoteza imani kwa watawala wa nchi zao.

 

Baada ya maelezo hayo sasa tutaashiria mifano michache ya nafasi ya mifumo ya tawala za kidikteta katika kuleta au kushadidisha mpasuko na mgawanyiko katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Wakati taasubi za kikaumu, kimbari na za utaifa zilipopea na kujikita kwenye kitovu cha Ukhalifa wa Othmaniyya; na kwa upande mmoja ndani ya dola hilo ukazuka mfarakano baina ya makundi na kaumu tofauti; na kwa upande mwengine utawala huo wa Othamniyya ukaingia kwenye mzozo na ugomvi na kambi na mhimili mwengine wa Ulimwengu wa Kiislamu, yaani utawala wa Safawiyyah nchini Iran, Sultan Abdulhamid wa Pili aliamua kufuata sera ya Umajimui wa Kiislamu, Pan-Islamism na kuifanya kuwa ndio dira kuu ya siasa zake, ambapo kwa hatua mbalimbali alizochukua ili kuweza kuimarisha mfungamano baina ya nchi za Kiislamu aliandaa mazingira ya kuwepo mielekeo ya umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika kufanikisha lengo hilo alitekeleza mambo kadhaa ikiwemo kuanzisha njia ya reli na kuwahudumia mahujaji wa Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu. Lakini moja ya vizuizi muhimu zaidi vilivyokwamisha kuthibiti dhana na ndoto hiyo ya umoja ni sera zake mwenyewe za kiimla ndani ya dola la Othmaniyya. Kwa maneno mengine ni kwamba kwa vile kwa upande wa ndani Sultan Abdulhamid wa Pili alikuwa akiamiliana na Waislamu kidikteta na hatua alizokuwa akichukua zilikuwa haziendani na maadili ya Kiislamu, alishindwa kuvutia imani za wananchi na watawala wa nchi nyengine za Kiislamu. Hatua alizochukua Sultan Abdulhamid zilionekana kuwa zililenga kukidhi maslahi yake ya kisiasa, kupenda jaha kwake na matashi yake binafsi; na kwa sababu hiyo dhana na ndoto yake ya Umajimui wa Kiislamu yaani Pan-Islamism ilifeli na kugonga mwamba.

********

Vilevile katika muongo wa 1970 wakati Ulimwengu wa Kiislamu ulipokuwa katika muelekeo wa kujenga umoja chini ya mhimili wa kadhia ya Palestina huku akthari ya nchi za Kiislamu zikiwa zimeshikamana pamoja katika kukabiliana na Israel, utawala wa kiimla na kidikteta uliokuwa ukitawala wakati huo nchini Iran ulikataa kujiunga na vuguvugu la mwaka 1973 la kususa kuziuzia mafuta nchi za Ulaya na Magharibi na hivyo kupelekea kushindwa vuguvugu na harakati hiyo ya Ulimwengu wa Kiislamu. Katika makabiliano hayo, nchi za Kiislamu na Kiarabu zilisimama katika kambi moja iliyoungana chini ya mhimili wa kadhia ya Palestina kukabiliana na utawala wa Kizayuni, lakini tamaa ya kutaka makuu aliyokuwa nayo Shah wa Iran na uhusiano mzuri aliokuwa nao na Israel na Marekani ulikwamisha kupiga hatua mkakati huo katika sura ya wigo mpana wa umoja wa Kiislamu; kwa sababu mfalme huyo wa Iran ambaye alikuwa dikteta kwa maana halisi hakujali wala kuyapa umuhimu sana maoni na matakwa ya wananchi Waislamu wa Iran. Kwa sababu hiyo alikataa kuungana na nchi nyengine za Kiislamu na kupelekea kupotea fursa hiyo adhimu ya kupatikana umoja na msimamo mmoja katika Ulimwengu wa Kiislamu.

 

Lakini pia wakati Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yalipopata ushindi na kuporomoshwa utawala wa kidikteta wa Mohammad Reza Shah, ambapo yalikuwa yamepatikana mazingira mwafaka ya kuleta umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu kutokana na kuwepo utawala wa Kiislamu nchini Iran ulioonyesha nia na hamu ya kuungana na Ulimwengu mzima wa Kiislamu ili kukabiliana na kambi ya Marekani, Urusi na Israel, utawala wa kidikteta nchini Iraq uliokuwa ukiongozwa na Saddam Hussein uliishambulia na kuivamia kijeshi Iran huku ukichochea na kuhamasisha hisia za utaifa wa Kiarabu dhidi ya Iran na kukwamisha kufikiwa umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Ulichofanya utawala wa kiimla wa Saddam ilikuwa ni kuzitumbukiza nchi mbili za mataifa ya Kiislamu za Iran na Iraq kwenye lindi la vita vya miaka minane. Muelekeo huo wa utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu ulionekana dhahiri shahiri katika namna mataifa ya Kiarabu yalivyoamiliana na Iran na misimamo yao ya kuipendelea Iraq katika vita ilivyoanzisha dhidi ya Iran. Hivi sasa pia baada ya kuangushwa na kusambaratika utawala wa kidikteta wa Saddam na kuja madarakani nchini Iraq serikali iliyotokana na wananchi wenyewe, mazingira ya kupatikana muelekeo mmoja katika Ulimwengu wa Kiislamu yamepata nguvu zaidi; hata hivyo watawala madikteta na wenye kupenda kuingilia masuala ya mataifa mengine wanaoshikilia hatamu za uongozi katika baadhi ya nchi za Kiislamu za Kiarabu wanafanya uafriti na kila njia ili kukwamisha kupatikana umoja baina ya Waislamu.

Wapenzi wasikilizaji, muda uliotengwa kwa ajili ya sehemu ya 40 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu umefikia tamati. Hivyo sina budi kuishia hapa kwa leo nikitumai kuwa mumefaidika na kunufaika na yale mliyoyasikia katika kipindi chetu cha leo. Basi hadi wiki ijayo inshaallah tutapokutana tena katika sehemu ya 41 ya mfululizo huu nakuageni huku nikikutakieni heri na fanaka maishani.

Tags