Apr 21, 2018 10:26 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (41)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 41.

Bila shaka wapenzi wasikilizaji mngali mnakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tulieleza kwamba kwa mtazamo wa wanafikra na warekebishaji umma wengi wa Ulimwengu wa Kiislamu, moja ya sababu kuu za kubaki nyuma kimaendeleo Waislamu ni mifarakano na utengano unaosababishwa na uingiliaji unaofanywa na maajinabi katika mataifa ya Waislamu hususan nchi za Magharibi. Sayyid Jamaluddin Asad Abadi, ambaye ni mbeba bendera ya harakati ya mwamko wa Kiislamu, alianzisha harakati yake ya kuleta mwamko, wakati mataifa ya Waislamu duniani yalipokuwa yameandamwa na hujuma za kisiasa na kijeshi na uvamizi wa madola ya Ulaya. Wakati hapo awali Sayyid Jamal alikuwa akiyaangalia masuala na matatizo ya ndani katika nchi za Kiislamu kuwa sababu kuu ya kubaki nyuma kwao kimaendeleo, alianza kidogokidogo kubaini kwamba matatizo ya ndani na uingiliaji wa maajinabi ni pande mbili za sarafu moja ambazo hazipasi kutenganishwa katika kuzifanyia uhakiki na uchambuzi. Kwa sababu hiyo alianzisha jumuiya ya siri ya kisiasa ya Al-U'rwah na kuyafanya mapambano dhidi ya ukoloni kuwa ndiyo ajenda kuu ya harakati zake za kifikra na kivitendo. Ili kufanikisha lengo la kuwahamasisha Waislamu kupambana na ukoloni, Sayyid Jamaluddin Asad Abadi alipendekeza Waislamu wa ulimwengu mzima wakubaliane juu ya kuwepo nchi moja kubwa na yenye nguvu ya Kiislamu ambayo itakuwa ni kama kambi yao ya muqawama, ili nguvu zote za Ulimwengu wa Kiislamu ziratibiwe na kuelekezwa katika kukabiliana na uingiliaji wa maajinabi hususan nchi za Magharibi. Kwa sababu hiyo, katika makala na hotuba zake alijaribu kuivunja na kuonyesha kuwa ni ngano tu dhana kwamba Ukoloni hauwezi kushindika ili kuzipa ilhamu ya ujasiri na ushujaa nyoyo za wananchi na watawala wa mataifa ya Kiislamu. Kwa mtazamo wa Sayyid Jamaluddin, wale waliokuwa wakiufungulia njia Ukoloni ili kujipenyeza na kuwa na satua ndani ya nchi za Kiislamu, na vilevile watu waliokuwa wakikataa kujiunga na vuguvugu la kukabiliana na Ukoloni, wote wao walistahili kuitwa mahaini na wasaliti. Mtazamo huo waliendelea kuwa nao warekebishaji umma wengi waliofuatia baada yake.

Hatukukutuma Ewe Muhammad ila uwe rehema kwa viumbe wote

 

Kutilia mkazo nafasi ya sababu za nje, yaani Ukoloni wa maajinabi si mtazamo waliokuwa nao wanafikra wa Kiislamu wa mwanzoni peke yao, lakini hata warekebishaji umma na wanafikra waliofuatia pia waliliwekea msisitizo na mkazo maalumu suala hilo. Hakuna shaka kuwa Imam Khomeini (MA) ni kiranja na jemadari wa harakati hiyo ya kifikra na kisiasa katika kipindi cha nusu karne iliyopita. Katika kuhakiki na kuifanyia upembuzi hali ya kubaki nyuma kimaendeleo nchi za Kiislamu, mbali na Imam Khomeini kusisitiza juu ya mfungamano uliopo kati ya udikteta wa ndani na ukoloni wa nje, ameyataja maslahi ya madola makubwa na ya kikoloni kuwa moja ya vizuizi vya kupatikana umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu. Imam Khomeini amesema: "Kuna mikono inayoshughulika kwa kutumia mbinu tofauti ili kuzuia Uislamu usisimame. Hivi sasa kuna mbinu tofauti zinazotumiwa; maajinabi wamefikia hitimisho kwamba Uislamu unahatarisha maslahi yao; ikiwa Uislamu utasimama, na ikatokea nchi ikawa na utawala wa Kiislamu hawatoweza daima kufanya chochote kile… wanachojaribu wao kufanya hivi sasa ni kuzusha mfarakano baina ya Waislamu." (Loho ya Nuru, juzuu ya 7, ukurasa wa 99). Katika mahali pengine, Imam Khomeini anasema: "Wale wanaotaka kuyanyonya mataifa ya Waislamu, wale wanaotaka kuzipora rasilimali za Waislamu, wale wanaotaka nchi za Kiislamu ziwe chini ya mamlaka na udhibiti wao, wao wenyewe na wanaowatumikia wamefanya kila njia kuzusha mfarakano baina ya Waislamu." (Hiyohiyo, juzuu ya 13, ukurasa wa 164).

Tunapoyatalii matukio na mabadiliko ya kisiasa katika nchi za Kiislamu inatubainikia kwamba Ukoloni, siku zote umekuwa ukizusha mfarakano baina ya mataifa ya Waislamu kwa kutumia siasa za "wafarakanishe ili uwatawale" ili kuweza kuyafikia haraka zaidi na kwa wepesi zaidi malengo yake ya kikoloni. Kwa kufanya hivyo umeweza kwa karne kadhaa kupora utajiri wa nchi za Kiislamu. Mfano wa mwanzo na kielelezo cha kihistoria cha nafasi ya maajinabi katika kusababisha utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu ni jinsi walivyoyafarakanisha madola mawili makuu ya Ulimwengu wa Kiislamu, yaani Iran ya wakati huo na utawala wa Othmaniyya. Wakati dola la Othmaniyya, likiwa ni dola kubwa la Kiislamu, lilipokuwa na nguvu zaidi kulinganisha na madola ya Magharibi, kiasi kwamba Magharibi haikuwa na uwezo wa kukabiliana na mashambulio makubwa ya kisiasa na kijeshi ya dola hilo, moja ya hatua muhimu zaidi zilizochukuliwa na Wamagharibi kukabiliana na Ulimwengu wa Kiislamu, ilikuwa ni kuandaa mazingira na kuwasha moto wa hitilafu na mapigano ya ana kwa ana kati ya Iran na dola la Othmaniyya, ambayo yalikuwa maeneo makubwa kijiografia ya Ulimwengu wa Kiislamu.

 

Katika zama za utawala wa Wasafawiyyah nchini Iran, kwa hila zilizofanywa na madola ya Ulaya, utawala huo ulikubali kushirikiana na madola hayo kuanzisha vita na mashambulio dhidi ya adui yao wa pamoja, yaani dola la Othmaniyya. Katika upande wa pili pia, Waothmaniyya nao walichukua hatua kadhaa za kuvunja na kudhoofisha nguvu na umoja wa Waislamu; na kwa njia hiyo Wazungu wa Ulaya wakaweza kufikia malengo yao kwa njia hiyo ya kuzifarakanisha kambi hizo mbili kuu za Ulimwengu wa Kiislamu. Baada ya kuanguka dola la Othmaniyya pia wakoloni waliendelea kutekeleza siasa hizo. Wakati dola la Othmaniyya liliposhindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia yalipatikana mazingira mwafaka ya kuleta mgawanyiko na mpasuko ndani ya dola hilo. Kambi ya waliojulikana kama 'Waitifaki', ambao ndio waliokuwa washindi wa vita hivyo walifanya kila njia kuligawanya dola hilo katika sura ya nchi mbalimbali, zilizochorewa na kuwekewa mipaka bandia, ambayo baadaye ilikuja kusababisha mizozo na mapigano mengi baina ya nchi hizo. Kuchipuka nchi kama Uturuki, Syria, Iraq, Jordan na Saudi Arabia kulikuwa miongoni mwa matokeo ya kugawanya vipande vipande dola la Othmaniyya baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Tukiziangalia hitilafu na tofauti na mapigano mbalimbali yaliyozuka baina ya nchi hizo katika kipindi cha miaka ya baada ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia tutabaini kuwa nchi za Ulaya zilifanikiwa kufikia malengo yao kwa kuligawanya vipande vipande dola la Othmaniyya.

Wasikilizaji wapenzi, muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki kwa leo umemalizika, hivyo sina budi kuishia hapa huku nikitumai kuwa mumeelimika na kunufaika na yote mliyoyasikia katika mfululizo huu. Tutakutana tena wiki ijayo inshallah katika siku na saa kama ya leo, katika sehemu ya 42 ya kipinid hiki. Basi hadi wakati huo nakuageni huku nikikutakieni kila la heri maishani.

Tags