Apr 21, 2018 10:36 UTC
  • Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu (43)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yenu wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo. Karibuni kusikiliza kipindi hiki kinachozungumzia suala muhimu na la msingi la Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu. Suala ambalo kutokana na kipindi ambacho Ulimwengu wa Kiislamu unakipitia hivi sasa umuhimu wake unahisika zaidi wakati huu pengine kuliko wakati mwengine wowote ule. Endeleeni basi kuwa pamoja nami kuanzia awali hadi tamati ya mfululizo huu, hii ikiwa ni sehemu yake ya 43.

Kwa wale wasikilizaji wa kawaida wa kipindi hiki bila shaka mngali mnakumbuka kuwa katika kipindi kilichopita tulijiuliza suali moja la msingi nalo ni je, kujitokeza na kupata nguvu harakati na magenge ya ukufurishaji, chimbuko na chanzo chake ni nje tu ya Ulimwengu wa Kiislamu? Tukajibu kwa kusema tukifanya upembuzi yakinifu tutabaini kuwa kujitokeza kwa wimbi na harakati hiyo ni matunda na kielelezo dhahiri kabisa cha mfungamano wa sababu za ndani ya Ulimwengu wa Kiislamu na nje ya ulimwengu huo katika kuleta mpasuko na mgawanyiko katika Ulimwengu wa Kiislamu. Katika sehemu hiyo ya 42 ya mfululizo huo tulianza kuzungumzia harakati ya Utalibani nchini Afghanistan. Tulieleza kwamba jina la Taliban, likiwa ni kundi jipya la kifikra, kiitikadi na kisiasa na wakati huohuo la kijeshi lilisikika na kuonekana kwa mara ya kwanza mwaka 1994 katika ripoti zilizotolewa kuhusiana na matukio na mapigano yaliyojiri nchini Afghanistan. Kwa msaada wa wanafunzi wa kidini waliotumwa kutoka Pakistan, Taliban waliweza kidogo kidogo kuyatia mkononi na kuyatawala maeneo mengi ya ardhi ya Afghanistan. Pakistan, Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu zilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo zilizoutambua utawala wa Taliban kuwa ni serikali halali ya Afghanistan. Wakati ule, wachambuzi wengi hawakuipa uzito mkubwa harakati ya Taliban lakini kadiri muda ulivyopita ndipo ilipobainika kuwa Taliban ni dhihirisho na kielelezo halisi cha vuguvugu hatari la kifikra, kiitikadi na kisiasa ambalo linaukeketa na kuuhasiri mshipa wa uhai wa Ulimwengu wa Kiislamu. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, kwa kutumia majina na kujiratibu katika makundi na magenge tofauti, harakati ya Taliban imeeneza moto wa chuki na uadui baina ya Waislamu na kuichafua hadhi na heshima yao katika kila pembe ya dunia.

Shikamaneni na Kamba ya Allah nyote wala msifarikiane

 

Kujitokeza kwa kundi la Taliban na kuibuka fikra ya Utalibani nchini Afghanistan chimbuko lake limetokana na sababu za ndani na nje ya nchi hiyo. Imeelezwa hapo kabla kwamba udikteta na uingiliaji wa maajinabi ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi za kubaki nyuma kimaendeleo nchi za Kiislamu na kujitokeza mifarakano na utengano katika Ulimwengu wa Kiislamu. Nchini Afghanistan udikteta na uingiliaji wa madola maajinabi ni mithili ya pande mbili za sarafu moja zilizochangia kwa pamoja kuvurugika amani, kujitokeza hali ya mchafukoge na kudumaa kiuchumi na kiutamaduni na kuandaa mazingira ya kuchipua na kushamiri fikra potofu na za kufurutu mpaka za kidini kama za kundi la Taliban. Baada ya kupita miaka mitano, tangu Daud Khan alipotwaa madaraka mwaka 1973 kwa kuuangusha utawala wa Dhahir Shah kupitia mapinduzi ya kijeshi, mapinduzi mengine yaliyoongozwa na chama cha demokrasia cha wananchi wa Afghanistan yaliuondoa utawala wake na kumgharimu pia maisha yake. Mapinduzi hayo ya kijeshi yaliiandalia fursa Urusi ya zamani kujiingiza kijeshi nchini Afghanistan. Katika zama hizo, kutokana na uhusiano mzuri uliokuwepo baina ya chama cha demokrasia cha wananchi wa Afghanistan na Shirikisho la Kisovieti la Urusi, mnamo mwaka 1979, serikali ya Moscow ilituma vikosi vya jeshi lake huko Kabul kwa lengo la kuihami na kuilinda serikali ya wakati huo iliyokuwa katika hali ya kuporomoka na kusambaratika. Urusi ilianza kujikita kijeshi rasmi nchini Afghanistan tarehe 24 Desemba mwaka 1979 kwa kuishambulia nchi hiyo kutokea pande kadhaa; na kwa utaratibu huo vita vilivyokuwa maarufu kwa jina la "Vietnam ya Urusi" vikaanza rasmi.

*********

Katika kipindi hicho, makundi kadhaa yaliyojulikana kama Mujahidina yaliundwa kwa lengo la kukabiliana na jeshi la Urusi, ambapo jeshi hilo Jekundu liliandamwa na mashambulio ya makundi ya Mujahidina katika kila pembe ya Afghanistan. Marekani, ambayo haikupendezwa na uingiliaji kijeshi wa Urusi nchini Afghanistan, ilianza kuyapatia silaha makundi ya Mujahidina ya nchi hiyo. Ni katika wakati huo, Usama bin Laden alielekea Afghanistan akitokea Saudi Arabia huku akiungwa mkono na Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) na kukabiliana na majeshi ya Shirikisho la Kisovieti. Kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na Urusi ya zamani na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi hiyo kwa upande mmoja, na kwa upande mwengine kushindwa viongozi wa jihadi na makundi ya Kiafghani kuunda serikali pana na shirikishi ambayo ingeleta uthabiti wa kisiasa na kurejesha usalama ndani ya nchi na matokeo yakawa ni kuenea ukata wa kiuchumi na kiutamaduni na kushtadi hitilafu za kikaumu, zilikuwa miongoni mwa sababu na chanzo kikuu cha kuibuka harakati hiyo hatari katika Ulimwengu wa Kiislamu; kwa sababu licha ya majeshi ya Urusi ya zamani kuondoka katika ardhi ya Afghanistan mnamo tarehe 15 Februari mwaka 1989, Najibullah aliweza kwa muda fulani kuendelea kuongoza serikali ya Kabul iliyokuwa ikiungwa mkono na Wakomunisti na Shirikisho la Kisovieti, lakini baada ya yeye kuondolewa madarakani hitilafu nyingi zilizuka baina ya Mujahidina ambazo ziliwasha cheche ya moto wa vita vya ndani nchini Afghanistan. Hali hiyo ya mchafukoge yalikuwa matokeo ya uingiliaji wa dola ajinabi ndani ya ardhi ya nchi za Kiislamu na kujitokeza mipasuko ya kikaumu na kimadhehebu baina ya Waislamu wenyewe ambavyo viliandaa mazingira ya utangulizi wa kuzuka harakati zenye misimamo ya kufurutu mpaka.

 

Miaka kumi ya vita vikali kati ya wapiganaji wa makundi ya jihadi ya Afghanistan na majeshi ya Shirikisho la Kisovieti la Urusi kuanzia mwaka 1979 hadi 1989 kwa upande mmoja, na kuvurugika uthabiti na kuzuka mapigano ya wenyewe kwa wenyewe baina ya makundi ya mujahidina kwa upande mwengine viliisambaratisha misingi ya uchumi wa Afghanistan na kusababisha ufakiri na umasikini ndani ya nchi. Kuendelea na kushadidi hali hiyo ya umasikini miongoni mwa wananchi ni miongoni mwa sababu muhimu zaidi za kujitokeza kwa Taliban. Nukta hii ni ya kuzingatiwa, kwa kutilia maanani kwamba, akthari ya wapiganaji wa kundi la Taliban na vitengo vikuu vya kundi hilo vinatokana na vijana wa matabaka ya chini na ya mafakiri katika jamii ya Afghanistan hususan ya Wapashtun, ambao katika miaka ya baada ya kuondoka majeshi ya Urusi na kumalizika vita vya makundi ya jihadi walikuwa wakisoma kwenye madrasa za kidini nchini Pakistan, ili kwa msaada mdogo wa kifedha waliokuwa wakipata kutoka kwa viongozi wa kidini wa madrasa hizo wakati wakiwa masomoni waweze kujiondoa kwenye hali ya ukata na ufukara. Hali mbaya ya uchumi na ukata wa kiutamaduni kwa upande mmoja, na ushawishi wa tangu na tangu wa desturi za kidini pamoja na hamu ya kusoma katika madrasa ni sababu muhimu iliyoziwezesha baadhi ya nchi za eneo kuiunda na kuitumia harakati ya Taliban kama kundi la kidini na kijeshi.

Wapenzi wasikilizaji, sehemu ya 43 ya kipindi cha Umoja Katika Ulimwengu wa Kiislamu imefikia tamati. Nakuageni basi huku nikikutakieni kila la kheri maishani.

Tags