Jul 05, 2018 02:42 UTC
  • Alkhamisi tarehe 5 Julai 2018

Leo ni Alkhamisi tarehe 21 Shawwal 1439 Hijria sawa na 5 Julai 2018.

 Miaka 1347 iliyopita katika siku inayosadifiana na ya leo, ardhi ya Andalusia huko Uhispania ya leo ilidhibitiwa na jeshi la Kiislamu lililoongozwa na Tariq bin Ziyad. Tariq ambaye alikuwa na wapiganaji karibu ya elfu 12, alivuka kwa boti mlango bahari ulioko kati ya Morocco na Uhispania ambao umepewa jina lake Tariq bin Ziad au "Gibraltar". Tariq bin Ziyad aliamuru kochomwa moto boti zote zilizotumiwa na wapiganaji wake kuvukia lango bahari na Gibralta ili kuwahamasisha zaidi kupigana na maadui. Katika kipindi cha karne 8 za utawala wao huko Andalusia, Waislamu walianzisha vituo mbalimbali vya utamaduni na taasisi za kiuchumi na kwa kipindi kirefu ardhi hiyo ilikuwa kituo kikuu cha ustaarabu wa Kiislamu barani Ulaya.

Tariq bin Ziyad

Miaka 1085 iliyopita mwafaka na leo, alifariki dunia Ibn Habban, mtaalamu wa hadithi, elimu ya fiq'hi na mwanahistoria mashuhuri wa karne ya 14 Hijiria. Alipata elimu ya msingi kwa walimu mashuhuri wa zama zake na kisha akaelekea Neishabur kaskazini mwa mashariki mwa Iran, ambao katika kipindi hicho ulikuwa ni moja ya vituo muhimu vya kielimu. Ibn Habban anahesabika kuwa mtu mwenye nadharia muhimu katika elimu ya hadithi. Miongoni mwa athari muhimu za msomi huyu mkubwa ni pamoja na kitabu cha"At-Thuqat" na Rawdhatul-Uqalaai wa Nazahatul-fudhalaai."

Siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, nchi ya Venezuela ilijitangazia uhuru wake na kwa ajili hiyo, tarehe 5 Julai, hutambuliwa kama siku ya kitaifa nchini humo. Tangu mwanzoni mwa karne ya 16 Miladia, na kwa kipindi cha karne tatu Venezuela ilikuwa chini ya ukoloni wa Uhispania. Katika kipindi cha ukoloni huo, raia wa nchi hiyo walipatwa na matatizo mengi, kiasi kwamba makumi ya maelfu ya Wahindi Wekundu ambao ni raia asili wa taifa hilo waliuawa na mahala pao kuchukuliwa na Wahispania. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, mapambano ya wananchi yalianza chini ya uongozi wa Francisco Miranda na kuzaa matunda katika siku kama ya leo mwaka 1811.

Bendera ya Venezuela

Siku kama ya leo miaka 185 iliyopita, alifariki dunia Nicéphore Niépce, mvumbuzi wa kamera. Niépce alifanikiwa kusajili kwa mara ya kwanza uvumbuzi huo mnamo mwaka 1826 baada ya kufanya majaribio kadhaa ya kielimu katika uwanja huo.

Nicéphore Niépce

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, wananchi wa Algeria walipata uhuru wao dhidi ya wavamizi wa Ufaransa, kufuatia kujiri mapambano makali na ya muda mrefu na wavamizi hao. Ufaransa iliikalia kwa mabavu Algeria kwa kutegemea jeshi lake kubwa mnamo mwaka 1830. Kwa kipindi cha miaka 130 ya kukoloniwa taifa hilo, raia wa Algeria waliasisi harakati kadhaa za kupigania uhuru zilizokuwa zikiongozwa na Amir Abdulqadir al Jazairi, ambazo hata hivyo zilikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa jeshi la Ufaransa. Hata hivyo harakati hizo zilishika kasi zaidi na kuzaa matunda baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia na kujipatia uhuru wake miaka 53 iliyopita katika siku kama ya leo.

Bendera ya Algeria

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Jenerali Muhammad Zia-ul-Haq alifanya mapinduzi ya kijeshi yaliyoiondoa madarakani serikali ya Zulfiqar Ali Bhutto nchini Pakistan. Muhammad Zia-ul-Haq alitwaa madaraka yote ya waziri mkuu na rais wa Jamhuri ya Pakistan na mbali na kuwanyonga Zulfiqar Bhutto na wapinzani wake wengine, alivunja mabunge ya nchi hiyo na kusimamisha shughuli zote za vyama vya siasa nchini Pakistan. Zia-ul-Haq aliuawa katika ajali ya ndege akiwa na maafisa kadhaa wa jeshi la Pakistan, na utawala wake ukakomea hapo.

Muhammad Zia-ul-Haq

Na siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, wanadiplomasia watatu na mwandishi habari mmoja wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran walitekwa nyara na wapiganaji wa chama cha Falanja cha Lebanon kaskazini mwa Beirut. Wanadiplomasia hao na mwandishi wa habari wa Iran walitekwa nyara wakati walipokuwa wakielekea kazini katika ubalozi wa Iran huko Beirut. Wakati tukio hilo lilipojiri jeshi la utawala wa Kizayuni lilikuwa limeishambulia Lebanon na chama cha Falanja kilikuwa na ushirikiano wa karibu na utawala ghasibu wa Israel. Ushahidi na nyaraka zilizopo zinaonyesha kuwa raia hao wa Iran wanashikiliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

 

Tags