Jul 11, 2018 18:26 UTC
  • Wanasayansi Wairani wakabiliana na saratani ipatikanayo katika viazi

Karibuni katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu mtaweza kuwa nami hadi mwisho.

Katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia, hivi karibuni, watafiti wa Chuo Kikuu cha Tehran nchini Iran wakishirikiana na wenzao wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Malaysia walifanikiwa kuunda nanocomposite ambazo zinaweza kuainisha na kutambua mada za sumu zenye kusababisha saratani katika vyakula vinavyotumika kwa wingi kama vile viazi. Acrylamide ni mada yenye kusababisha saratani na inapatikana katika baadhi ya bidhaa za chakula. 

Mwaka 2002, msomi mmoja nchini Sweden alithibitisha kuwa acrylamide inapatikana zaidi katika vyakula vyenye kabohaidreti kama vile viazi na mikate na mada hiyo ya saratani huibuka wakati chakula hicho kinapowekwa katika joto kali au wakati wa kukaangwa.

Kwa mujibu wa watafiti Wairani katika mradi huo, acrylamide ni ishio kubwa kwa afya ya watumizi wa bidhaa husika za chakula. Kwa msingi huo kiwango cha mada hiyo kinapaswa kuchunguzwa na kupimwa kabla chakuka hakijatumika. Katika kutatua tatizo hilo, watafiti wametengeneza nanokompositi ya hybrid kwa kutumia chembechembe za nano na mada ya graphen ambayo inaweza kutumika kupima kiwango cha acrylamide. Hivi sasa mbinu inayotumika kupima kiwango cha Acrylamide katika bidhaa za chakula ni ngumu na ghali mno.

Kutokana na umuhimu na udharura wa kutafuta njia ya haraka na isiyo ghali ya kuainisha kiwango cha Acrylamide katika vyakula mbali mbali, katika mradi wao, watafiti wamejaribu kuwasilisha mbinu mpya ya kutatua tatizo hilo kwa kufanya majaribio katika vyakula mbali mbali.

Kwa mujibu wa Dk Rashid Hamid Navadeh mmoja wa wataalamu katika mradi huu anasema mbinu ya nano teknolojia waliotumia ina uwezo mkubwa wa kupima mada hiyo ya acrylamide kwa njia sahali na isiyo na gharama kubwa na hivyo kuokoa maisha ya watu wengi.

 

 

Bendeji yenye kuponya kidonda haraka

Katika utafiti mwingine wa pamoja, hivi karibuni watafiti Wairani wakishirikiana na wenzao wa Australia walifanikiwa kuunda bendeji kwa kutumia teknolojia ya nano ambayo mada yake kuu imetokana na  mbuni. Bandeji hiyo ina uwezo mkubwa wa kuponya kwa kasi kidonda na kuwezesha ngozi kurejea katika hali yake ya kawaida.

Wagonjwa wengi huwa hawaridhiki na hali ya ngozi yao baada ya kupona vidonda vikubwa kwani alama huwa zinabaki. Kwa hivyo watafiti wamekuwa wakitafuta njia za kuhakikisha kuwa ngozi inarejea katika hali yake ya kawaida baada ya kidonda kupona au kuugua maradhi ya ngozi. Ni kwa sababu hii ndio watafiti wakaanzisha mkakati wa kutegeneza bandeji isiyotumia malighafi ya kemikali katika kutibu haraka vidonda na kurejesha ngozi katika hali yake ya kawaida. Watafiti wametumia mafuta ya mbuni yanayojulikana kama Emu  kuunda bandeji za nano.

Mmoja wa wahusika katika mradi huu,Younes Pilehvar Soltanahmadi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Tabriz anasema bandeji zenye mafuta ya mbuni husaidia kulinda na kuongeza seli shina za ngozi ambazo zinajulikana kama epidermal.

Naibu waziri wa afya Iran aenziwa kimataifa

Mapema mwaka huu Naibu Waziri wa Afya wa Iran Daktari Reza Malekzadeh, ambaye pia ni mtafiti bingwa wa saratani alitunukiwa nishani ya heshima ya Wakala wa Kimataifa wa Utafiti wa Saratani IARC.

Daktari Malekzadeh alitunukiwa nishani hiyo mnamo Januari 9 katika sherehe iliyofanyika katika makao makuu ya IARC mjini Lyon Ufaransa. Kikao hicho kilihutubiwa na mkurugenzi wa IARC Christopher P Wild.

Katika hotuba yake, Daktari Malekzadeh aliwashilisha matokeo ya uchunguzi wa eneo la  Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini ambao ulifanyika Iran kuhusu namna afiuni inavyoweza kueneza saratani.  

Daktari Malekzadeh ni Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti cha Golestan kaskazini mashariki mwa Iran ambacho kinafanya utafiti kuhusu uhusiano wa utumizi wa afiuni na saratani.  Daktari Malekzadeh ametunukiwa nishani hiyo kutokana na mchango wake wa utafiti kwa muda wa miongo miwili katika taasisi hiyo.

Wakala wa Kimataifa wa Utafiti wa Saratani ulianzishwa mwaka 1965 kama taasisi ya utaalamu wa saratani katika  Shirika la Afya Duniani WHO. Lengo la IARC ni kustawisha ushirikiano wa kimataifa katika utafiti kuhusu saratani.

Daktari Malekzadeh

Medali za IARC hutunikiwa wanasayansi ambao utafiti wao umetoa mchango mkubwa katika kustawisha ufahamu wa kitaalamu wa saratani sambamba na kubaini njia zinazopelekea kuibuka saratani na kuwasilisha njia za kuzuia na kutibu saratani.

Mayai yenye kutibu magonjwa sugu yavumbuliwa Japan

Hivi karibuni wanasayansi nchini Japan walitangaza kupata njia mpya ya kuzalisha dawa ambazo zinaweza kutumiwa kutibu idadi kubwa ya magonjwa kwa kutumia mayai ya kuku.

Wanasayansi wa Japan wamefanikiwa kubadilisha muundo wa kijenetiki wa kuku ili waweze kutega mayai yenye kiwango kikubwa cha  beta protini ya interferon ambayo hutumika kutibu magonjwa sugu kama saratani na MS  au multiple sclerosis ambao ni  ugonjwa wa mfumo mkuu wa neva.

Kwa kawaida beta protini ya interferon ni ghali mno na hugharimu baina ya $300-$1000 kila mikrogramu moja. Kwa mfano katika kutibu mfumo wa neva, dozi ya interferon  huanzia mikrogramu 30.

Utafiti huo umefanywa kwa pamoja na wanasayansi wa Kituo cha Kitaifa cha Sayansi ya Juu ya Kiviwanda na Teknolojia cha Japan, Kituo cha Kitaifa cha Utafiti wa Kilimo na Chakula cha Japan na Shirika la Utegenezaji Dawa la Cosmo Bio.

Kwa mujibu wa Mika Kitahara, msemaji wa Cosmo Bio,  teknolojia waliobuni inaweza kupunguza gharama za matibabu ya saratani kwa asilimia 90 iwapo majaribio zaidi yatafanikiwa.

Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Ubunifu na Teknolojia (INOTEX 2018)

Na wiki hii mjini Tehran kumefanyika Maonyesho ya 7 ya Kimataifa ya Ubunifu na Teknolojia (INOTEX 2018) ambapo mashirika ya kiteknolojia ya hapa nchini na ya kigeni yameshiriki katika maonyesho hayo ya siku tatu yaliayoanza Julai tano.

Kwa mujibu wa taarifa nara na kauli mbiu ya maonyesho ya mwaka huu ya INTOTEX 2018 ilikuwa ni 'Mji Erevu' ambapo washiriki wamejikita zaidi katika masuala ya usimamizi erevu wa nishati, uchukuzi erevu na usimamizi erevu wa data na Intaneti ya Vitu (IoT). Kwa mujibu wa nadharia ya IoT katika mustakabali usio mbali kila chombo unachomiliki kitakuwa kimeunganishwa  na intaneti na hivyo kuifanya intaneti iingie katika upeo mpya maishani.

Aidha pembizoni mwa maonyesho ya mwaka huu mameya wa miji ya Iran wamefanya kikao kwa lengo la kujadili njia za kuimarisha miji yao kiteknolojia.

Maonyesho hayo ya INOTEX hudhaminiwa na serikali ya Iran kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais Anayeshughulikia Masuala ya Sayansi na Teknolojia, Kituo cha Ubunifu na Teknolojia katika Ofisi ya Rais pamoja na Mfuko wa Ushirkiano wa Kiteknolojia na Ubunifu.