Jul 25, 2018 01:18 UTC
  • Jumatano Julai 25, 2018

Leo ni Jumatano tarehe 11 Dhulqaada 1439 Hijria sawa na Julai 25, 2018.

Siku kama ya leo miaka 1291 iliyopita, sawa na tarehe 11 Dhulqaad mwaka 148 Hijria, alizaliwa Imam Ali bin Mussa Ridha (as), mmoja kati ya Watu wa Nyumba ya Mtume Muhammad (as) katika mji wa Madina. Imam Ridha alichukua jukumu la kuwaongoza Waislamu mara baada ya kufariki dunia baba yake Imam Mussa al-Kadhim (as), mnamo mwaka 183 Hijiria. Shakhsia huyo alikuwa mbora zaidi katika ulimwengu wa Kiislamu wakati wa zama zake. Kwa minajili hiyo, Ma'amun Khalifa wa Kiabbasi alijaribu kumpatia wadhifa Imam Ridha (as) kwa shabaha ya kuimarisha nafasi yake na wakati huo huo kumdhibiti Imam. Imam Ridha (as) alikubali pendekezo hilo kwa kulazimishwa na kwa mashinikizo ya utawala wa Ma'amun. Mtukufu huyo aliwaeleza Waislamu wote, wakiwemo watu wa eneo la Khorasan, ukweli wa mambo ulivyo, na kuwaathiri mno wananchi kuhusiana na uhakika wa Ahlul-Bayt wa Mtume (as). Redio Tehran inatoa mkono wa heri na fanaka kwa Waislamu wote duniani hususan wapenzi wa Watu wa Nyumba ya Mtume (as) kwa mnasaba huu.

Siku kama ya leo miaka 1103 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 11 Dhul Qaad 336 Hijria, ilizaliwa Muhammad bin Muhammad mwenye lakabu ya Sheikh Mufid, msomi na mwanafaqihi mkubwa wa ulimwengu wa Kiislamu katika mji wa Baghdad. Sheikh Mufid alilelewa katika familia ya kielimu, kidini na yenye imani na kisha kujipatia elimu kutoka kwa wanazuoni wakubwa katika zama hizo. Miongoni mwa harakati zake za kifikra na kiutamaduni za Sheikh Mufid ilikuwa ni kufanya midahalo na mafaqihi na wasomi wa Madhehebu mbalimbali. Sheikh Mufid ametuachia vitabu mbalimbali vyenye thamani vikiwemo al Irshaad, al Arkaan na Usuulul Fiqh.

Sheikh Mufid

Miaka 124 iliyopita katika siku kama ya leo, vita kati ya Uchina na Japan vilianza kwa mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Japan dhidi ya maeneo ya pwani ya Uchina. Vita hivyo vilitokea baada ya mashambulio yaliyofanywa na Japan kwa lengo la kuiteka ardhi kubwa ya Peninsula ya Korea na kaskazini mwa China. Japan ndiyo iliyoshinda katika vita hivyo kutokana na kujizatiti vyema kwa silaha za kisasa.

Vita vya Japan na China

Tarehe 25 Julai mwaka 1938 yaani miaka 80 iliyopita, Wapalestina wasio na hatia 62 waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika milipuko miwili ya mabomu iliyotokea kwa nyakati tofauti katika soko la kuuzia mboga za majani huko Palestina. Makundi ya kigaidi ya Wazayuni ndiyo yaliyotega mabomu hayo mawili na lengo lao lilikuwa ni kuzusha hali ya machafuko na ukosefu wa amani kwa Wapalestina. 

Na miaka 25 iliyopita katika siku kama ya leo, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga na baharini huko kusini mwa Lebanon. Mashambulizi hayo yalikuwa operesheni kali zaidi ya kijeshi kuwahi kufanywa na Wazayuni dhidi ya Lebanon baada ya mashambulio waliyoyafanya dhidi ya ardhi nzima ya Lebanon mwaka 1982.

Mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon