Sep 23, 2018 16:39 UTC
  • Teknolojia (22)

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio ya sayansi na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani.

Mwanabiolojia Muirani, kwa mara ya kwanza duniani, amevumbua njia ya kuwezesha kutibu ugonjwa wa Mfumo wa Neva (Multiple Sclerosis) maarufu kama MS.

Mahmoud Sedaqati, mwanabiolojia Muirani akishirkiana na binti yake ambaye ni daktari, wamevumbua antigen zenye kubaini ugonjwa wa MS baada ya miaka 11 ya utafiti na hivyo kukaribia kuweza kutibu ugonjwa huo.

Akibainisha zaidi kuhusu uvumbuzi wake huo,  amesema kwa mara ya kwanza duniani sasa itawezekana kubaini uwepo wa ugonjwa wa MS kupitia vipimo vya damu.

Matibabua ya ugonjwa wa MS kwa kutumia antigen iliyovumbuliwa na mtaalamu wa Kiirani

 

Sedaqati ameongeza kuwa, antigen za matibabu ndio njia pekee ya kutibu ugonjwa wa MS na kuelezea matumaini kuwa, katika kipindi cha miaka minne ijayo, kutaweza kupatikana matibabu kamili ya MS.

Ugonjwa wa MS ni hatari na husababisha mwasho kwenye mfumo wa neva, yaani ubongo na uti wa mgongo. Madaktari wengi wanaamini kwamba ugonjwa huo hutokea wakati kinga za mwili zinaposhambulia chembe fulani za mwili. Kisababishi cha ugonjwa huo hakijulikani lakini inadhaniwa kwamba huenda unasababishwa na virusi. Kisha sehemu fulani za mfumo wa kinga huvamia utando muhimu wenye mafuta unaofunika nyuzi za mfumo wa neva, na hivyo kuacha makovu kwenye utando huo.

Kwa kawaida dalili huwa uchovu, unyonge, kufa ganzi kwa mikono na miguu, kushindwa kutembea, kuhisi kiu, uchungu, mwasho, matatizo ya kibofu na tumbo, na vilevile kushindwa kukuza fikira na kutofanya maamuzi inavyopaswa.

Uvumbuzi wa simu ya mkononi na fimbo erevu kwa ajili ya vipofu uliofanywa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Azad cha Sanandaj, Iran

 

Watafiti katika Chuo Kikuu cha Azad Islami katika mji wa Sanandaj nchini Iran wamefanikiwa kuunda simu erevu ya mkononi au smartphone maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho. Hivi sasa kuna takribani watu milioni 285 duniani ambao wana ulemavu wa macho ambapo miongoni mwao, milioni 39 hawana uwezo wa kuona hata kidogo. Ni kwa msingi huu ndio wavumbuzi Wairani wakatekeleza mradi wa kuwawezesha wenye ulemavu wa macho kutumia chombo cha kieletroniki ambacho kinafanya kazi kama simu ya mkononi au rununu.

Watafiti wa mradi huu wanasema wameunda rununu ambayo ina skirini yenye kibodi  iliyo na herufi za braile. Kibodi hiyo imeundwa kwa msingi wa kanuni za kimataifa za braile. Aidha simu hiyo ina uwezo kama ulio katika simu zingine za mkono duniani. Hali kadhalika watafiti wa chuo hicho pia wamefanikiwa kuunda fimbo maalumu (white cane) ya watu wenye ulemavu wa macho. Fimbo hiyo ya walemavu wa macho iliyoundwa na watafiti Wairani ni erevu na imetajwa kuwa fupi zaidi duniani. Fimbo hiyo inaweza kutambua vizingiti vilivyo hadi umbali wa mita mbili katika maeneo ya wazi yenye msongamano mkubwa.

Utaalamu wa kugundua ugonjwa wa Parkinzon na Alzeima kwa kutumia teknolojia ya Nano uliobuniwa na watafifi wa Iran na Ufaransa.

 

Katika hatua nyingine watafiti  Wairani  wa Chuo Kikuu cha Azad Islami cha Iran kwa kushirkiana na watafiti wa Chuo Kikuu cha Lille cha Ufaransa wamefanikiwa kuunda elektrodi ambazo zinaweza kutambua mjumuiko wa protini hata ambazo ziko katika muundo wa chembe chembe ndogo.

Baada ya ugonjwa wa Alzeima , ugonjwa wa Parkinson ndio ugonjwa ulioenea zaidi ambao huharibu mfumo wa neva. Kwa kifupi ugonjwa wa Parkinson ni ugonjwa unaoathiri ubongo na kumfanya mgonjwa kutetemeka, kupungua kwa uwezo wa kutenda na kutembea kwa kuchechemea. Kwa mujibu wa wataalamu, protini haribifu ambazo huenea katika seli za mwili na kuvuruga mfumo wa neva hatimaye husababisha ugonjwa wa Parkinson. Mbali na Parkinson mjumuiko huo  wa protini haribifu pia husababisha magonjwa mengine kama vile Alzeima na Kisukari. Ni kwa msingi huu ndio elektrodi zilizoundwa zinaweza kupima kiwango cha protini za lysozyme na kubaini protini hizo zilizojikusanya katika mwili.

Matokeo ya uchunguzi huo yamebaini kuwa, elektordi zilizofanyiwa marekebisho zinaweza kubaini kiwango cha mujumuiko wa protini hata zilizo katika muundo wa chembe chembe ndogo sana. Kati ya sifa za kipekee za elektordi hii  ni kupunguza gharama kutokana na utumizi wa mada za nano ambazo si ghali lakini zenye uwezo mkubwa wa kuvutia protini. Aidha elektordi hizo zina uwezo wa kutumiwa mara nyingine  baada ya kila kipimo. Mbinu hii mpya inaweza kusaidia kutibu magonjwa ya Kisukari, Parkinson na Alzeima na pia kusaidia katika utengenezaji wa dawa za kukabiliana na magonjwa hayo. Matokeo ya utafiti huo wa pamoja wa wanasayansi Wairani na Wafaransa yamechapishwa katika jarida la Electrochimica Acta.

Matibabu ya uziwi wa kuzaliwa nao

 

Hivi karibuni watafiti katika Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani  wamefanikiwa kutumia mbinu ya uhandisi wa kijenetiki kutibu uziwi wa kuzaliwa nao.

Watafiti wameweza kutumia panya wa maabara kuponya uziwi kwa kufanya marekebisho ya kijenetiki na hii ni mara ya kwanza kwa mbinu hii kutumika duniani. Kwa mafanikio hayo wameweza kutoa matumaini kuhusu matibabu ya uziwi wa kijenetiki.

Wataalamu wanasema karibu kesi zote za uziwi zina msingi wa kijenetiki na kwa sasa kuna vizingiti vingi katika matibabu. Lakini kwa kuibua mbinu mpya yenye uwezo wa hali ya juu wa marekebisho ya kijenetiki kama ile ya Crispr, kuna matumaini ya matibabu ambayo yanaweza kutatua tatizo la kimsingi la uziwi.

@@@@

Na Iran imeorodheshwa katika nafasi ya 15 duniani katika uga wa uzalishaji wa sayansi. Akizungumza mwezi Agosti, Naibu Waziri wa Sayansi, Utafiki na Teknolojia wa Iran Ibrahim Khodaei amesema hivi sasa  Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya 15 duniani kwa mtazamo wa uzalishaji wa kisayansi. Amesema kiwango cha uzalishaji sayansi Iran kimekuwa kikipanda katika miaka ya hivi kariubuni.

Akizungumza katika sherehe za maadhimisho ya mwaka wa 70 wa kuasisiwa Chuo Kikuu cha Tabriz amesema, "Iran ina asilimia moja ya watu wote duniani na nchi hii inazalisha asilimia 1.88 ya sayansi duniani.

Ameongeza kuwa ustawi katika uzalishaji sayansi ni kati ya mafanikio makubwa ya vyuo vikuu vya Iran.

Mwezi uliopita Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilitangazwa kuwa inayoongoza miongoni mwa mataifa ya Kiislamu duniani katika uga wa uzalishaji sayansi. Hayo yalidokezwa na mkuu wa Kituo cha Marejeo ya Sayansi katika Ulimwengu wa Kiislamu (ISC) Dkt. Mohammad Javad Dehqani.

Dehqani alisema kwa mujibu wa data ya Taasisi ya Taarifa za Kisayansi (ISI), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya kwanza miongoni mwa nchi za Kiislamu katika uzalishaji wa sayansi. Aliongeza kuwa Iran imeweza kuchangia asilimia 22 ya uzalishaji wa kisayansi katika nchi za Kiislamu. Hivi karibuni aidha, mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Iran Murtadha Barari alisema Iran inashika nafasi ya kwanza miongoni mwa nchi za eneo la Asia Magharibi katika uga wa sayansi za anga za mbali.