Apr 13, 2016 02:28 UTC
  • Jumatano, Aprili 13, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 5 Rajab 1437 Hijria sawa na Aprili 13, 2015.

Tarehe 5 Rajab miaka 1193 iliyopita aliuawa shahidi Abu Yusuf Yaqub ibn Is'haq, maarufu kwa jina la Ibn Sikkit, msomi wa Kiislamu na mtaalamu mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Alizaliwa katika mji wa Khuzestan unaopatikana kusini magharibi mwa Iran. Ibn Sikkit alielekea mjini Baghdad na familia yake na kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Umaarufu wa Ibn Sikkit katika elimu ulimfanya Mutawakkil, mmoja kati ya watawala wa Abbasia kumwalika kwa lengo la kuwafundisha watoto wake. Ibn Sikkit alikuwa na mapenzi makubwa kwa Watu wa Nyumba ya Mtume (SAW); jambo hilo lilimkasirisha sana Mutawakkil na alichukua hatua ya kumuua. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyu ni kile kiitwacho "Islahul Mantik."

Siku kama ya leo miaka 97 iliyopita, kulijiri tukio la umwagaji damu mkubwa katika Bustani ya Jallianwala Bagh nchini India. Mwaka 1919 na kwa lengo la kuzuia uasi na mapambano ya wananchi, serikali ya kikoloni ya Uingereza ilipasisha sheria iliyowapa polisi haki ya kuwatia mbaroni wanaharakati wa India bila sababu yoyote na kuwashikilia kwa muda usiojulikana. Sheria hiyo iliwakasirisha mno wananchi wa India na katika siku kama ya leo zaidi ya Wahindi elfu tano waliokuwa wamekusanyika kwa amani katika Bustani ya Jallianwala katika mji wa Amritsar walimiminiwa risasi kwa amri ya kamanda mmoja wa Uingereza. Watu 1200 waliuawa na wengine 4000 kujeruhiwa katika tukio hilo. Baada ya mauaji hayo, harakati ya ukombozi wa India ikiongozwa na shujaa Mahatma Ghandhi ilipamba moto.

Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, shambulio la wanamgambo wa Kikristo wenye misimamo ya kufurutu ada wa kundi la Mafalanja lililolenga basi moja lililokuwa na Wapalestina na kuua watu 30 kati yao, lilipelekea kuibuka vita vya ndani nchini Lebanon. kufuatia mauaji hayo, Waislamu na wazalendo wa Lebanon walianzisha mapambano ya kukabiliana na Mafalanja hao. Muda mfupi baadaye harakati za wapiganaji wa Kipalestina pia ziliingia katika vita hivyo vya ndani vya Lebanon. Vita hivyo ambayo vilikuwa vikichochewa na utawala haramu wa Israel, viliisababishia hasara kubwa ya mali na roho serikali ya Beirut.

Na tarehe 25 Farvardin miaka 28 iliyopita serikali ya wakati huo ya Iraq ilikiri waziwazi kwamba ilitumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Katika kipindi chote cha miaka minane ya vita hivyo Iran iliwasilisha mashtaka katika jumuiya za kimataifa kwamba Iraq inatumia silaha za kemikali dhidi ya wapiganaji wa Jamhuri ya Kiislamu. Wakati huo Iraq haikukiri wala kukadhibisha habari hiyo. Hata hivyo katika siku kama hii ya leo wakati vita vilipokuwa vimepamba moto, serikali ya Baghdad ilikiri kwamba inatumia silaha za kemikali zikiwemo za gesi ya sumu na hatari ya haradali dhidi ya malengo ya kijeshi na kiraia ya Iran.

Takwimu zimeonesha kwamba utawala wa Baath wa Iraq ulifanya mashambulizi 3,500 kwa kutumia silaha za kemikali dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote cha vita hivyo.