Jan 05, 2019 07:52 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur'ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur'ani. Hii ni darsa ya 816, na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 37 ya Ass 'Affat. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 123 hadi126 ambazo zinasema:

وَإِنَّ إِلْيَاسَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ

Na hakika Ilyas bila ya shaka alikuwa miongoni mwa Mitume.

إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَلَا تَتَّقُونَ

Alipo waambia watu wake: Hamna taqua?

أَتَدْعُونَ بَعْلًا وَتَذَرُونَ أَحْسَنَ الْخَالِقِينَ

Mnamwomba Baa'li na mnamwacha Mbora wa waumbaji,

اللَّـهَ رَبَّكُمْ وَرَبَّ آبَائِكُمُ الْأَوَّلِينَ

Mwenyezi Mungu, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa zamani? 

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia habari za manabii Ibrahim na Musa (as), aya tulizosoma zinaashiria habari za Nabii Ilyas (as) na kueleza kwamba: Kauli ya mwanzo aliyotoa kwa watu wa kaumu yake ilikuwa ni kuwataka wajiepushe na shirki, kuabudu masanamu na kutenda aina yoyote ya dhulma na ufisadi, hali waliyonayo watu wasio na taqwa, ambayo athari zake ni kuwafanya watende mambo maovu na machafu. Alizilenga dhamiri za waabudu masanamu wa kaumu yake na kuwaambia: Inakuwaje mnayaabudu na kuyaomba masanamu mliyoyatengeza kwa mikono yenu, lakini mnamsahau Mola aliyekuumbeni nyinyi wenyewe?! Je hayo masanamu yanao uwezo wa kuumba kitu chochote, hata mnayatukuza na kuonyesha heshima na taadhima mbele yao?! Kwani hayo ndiyo yaliyokuumbeni nyinyi na baba zenu au watoto wenu?! Kwa nini mnamwacha Mwenyezi Mungu, ambaye ni Mola wenu nyinyi na baba zenu, ambaye ndiye mwendeshaji wa mambo yote ya ulimwengu, na badala yake mnayaelekea maumbo yasiyo na uhai wala chochote cha maana? Kwa kuwa pengine waabudu masanamu hao walitetea na kuhalalisha wayafanyayo kwa kusema wanafuata mwenendo wa wazee wao waliotangulia, Nabii Ilyas aliwajibu kwa kuwaambia: Baba zenu na wazee wenu waliopita, wao pia ni viumbe wa Mwenyezi Mungu, hawakuumbwa na masanamu. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba Mitume wote wa Allah waliwalingania watu Tauhidi, yaani kutomwabudu mwengine au chengine chochote kile ghairi ya Allah SW, Mola pekee wa haki. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuabudiwa ni jambo analostahiki mbora tu wa waumbaji, yaani Muumba wa ulimwengu na vyote vilivyomo ndani yake, Mwenyezi Mungu aliyetukuka na kutakasika na kila upungufu. Aya hizi aidha zinatuelimisha kwamba, mwongozo mkuu wa mafundisho ya Mitume na ambao ndio msingi wa sifa zote za ukamilifu ulikuwa ni taqwa na kumcha Mwenyezi Mungu. Vilevile aya hizi zinatutaka tuelewe kwamba, katika kuamiliana na watu wao, Mitume walitumia mbinu ya uulizaji masuali mepesi na ya kawaida kwa njia ya ulinganishaji na yenye kufahamika, ili kuwatoa kwenye usingizi wa mghafala. Mfano wake ni kuyalinganisha masanamu yasiyo na uhai wala chochote cha maana na Muumba aliye mweza na mjuzi wa kila kitu, mbinu ambayo huziamsha dhamiri zilizolala za watu.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 127 hadi 129 za sura yetu ya Ass 'Affat ambazo zinasema:

فَكَذَّبُوهُ فَإِنَّهُمْ لَمُحْضَرُونَ

Wakamkadhibisha. Basi kwa hakika watahudhurishwa; 

إِلَّا عِبَادَ اللَّـهِ الْمُخْلَصِينَ

Isipo kuwa waja wa Mwenyezi Mungu walio safishwa. 

وَتَرَكْنَا عَلَيْهِ فِي الْآخِرِينَ

Na tumemwachia (sifa nzuri) kwa walio kuja baadaye.

Kama zilivyokuwa kaumu nyingi zilizopita, akthari ya watu wa kaumu ya Nabii Ilyas, nao pia waliukadhibisha wito wake na hawakuwa tayari kuyakubali mawaidha na nasaha zake za kuwataka waache kuabudu masanamu. Qur'ani tukufu inasema: Hatima ya ukadhibishaji wa aina hiyo ni kuchafuka nafsi kwa anuai za madhambi na matendo maovu na kufikwa na adhabu kali ya Mola. Ni watu wachache tu waliomwamini Nabii Ilyas, ambao walikuwa wakimwabudu Allah kwa ikhlasi, hao ndio waliookoka. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: Mwenyezi Mungu anawalipa malipo mema Mitume kwa kazi yenye mashaka na tabu kubwa waliyofanya na kuyataja majina yao kwa wema ili fikra na sira ya waja hao wateule iendelee kubakia milele katika historia. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, kipimo cha saada na kufuzu si maisha ya kidunia ya watu, bali ni jinsi hatima yao itakavyokuwa Siku ya Kiyama, kwamba, je wao watafuzu na kuokoka huko akhera au watahasirika kwa kuishia motoni. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kumwabudu Allah kwa ikhlasi kiimani na kimatendo ndio njia itayomwezesha mtu kufuzu na kuokoka na kunusurika na adhabu ya Moto. Kutokuwa na ikhlasi katika kufuata njia ya Mwenyezi Mungu kutamkosesha mtu kuifikia saada.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 130 hadi 132 ambazo zinasema:

سَلَامٌ عَلَىٰ إِلْ يَاسِينَ

Amani kwa Ilyasin.

إِنَّا كَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ

Kwa hakika hivyo ndivyo tunavyo walipa watendao mema.

إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُؤْمِنِينَ

Hakika yeye ni katika waja wetu walio waumini.

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia habari za Nabii Ilyas, aya tulizosoma zinasema: Mwenyezi Mungu anamtakia rehma na amani Mtume wake huyo. Tab'an katika aya ya 130, badala ya jina Ilyas limetajwa jina la Alyasin, lakini yote hayo mawili ni majina ya Mtume mmoja, kama ilivyo kwa Sina na Sinin, ambayo yote mawili ni majina ya ardhi moja. Katika aya mbalimbali zilizotangulia za sura hii zimezungumziwa habari za baadhi ya Mitume. Na katika kuhitimisha uzungumziaji wa visa vya maisha ya kila mmoja wao, Allah SW amezitaja imani za daraja ya juu kabisa, thabiti na za ikhlasi za waja hao watukufu, na kuzienzi juhudi na mema waliyofanya na kusema: Huu ndio utaratibu wetu wa kuwalipa malipo mema na thawabu waja wetu wafanyao mema. Katika sehemu ya mwisho ya aya zinazozungumzia habari za Nabii Ilyas, Qur'ani tukufu imeashiria pia nukta hiyo na kueleza kwamba: Jitihada, tabu na usumbufu wanaopata wale wote wanaoshika njia ya Allah na wakashughulika kufanya mema na kuwatendea watu mambo ya kheri, havitasahauliwa. Hii ni kaida na utaratibu wa Allah, wa kuwalipa ipasavyo wafanyao mema, wawe ni Mitume au watu wa kawaida. Tab'an kwa sharti kwamba, wawe ni waja waumini na wayafanye hayo katika njia ya Allah. Vinginevyo, kama mtu anakanusha kuwepo kwa Mwenyezi Mungu na hayuko tayari kujisalimisha na kunyenyekea kwa Muumba wake, hata kama atafanya jambo jema na la kheri, jema hilo atakuwa amewafanyia walimwengu, na malipo yake atayapata hapa duniani kwa njia hiyo hiyo ya kilimwengu, ya kusifiwa na kushukuriwa na aliowafanyia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, tujifunze kwa Allah kuwasalia na kuwatakia rehma na amani Mitume na mawalii wake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kupata rehma na fadhila za Allah SW waja wafanyao mema na ihsani ni utaratibu wa kudumu na wa kuendelea aliojiwekea Yeye Mola. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba kila mtu atakayekuwa mja wa kweli wa Allah, muumini na mtenda mema ataendelea kupata amani na rehma za Allah katika zama zote za historia. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 816 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atupe mema duniani na atupe mema akhera na atulinde na adhabu ya moto. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

Tags