Sayansi na Teknolojia Mpya (24)
Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya matukio muhimu katika uga wa sayansi na teenolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani.
Licha ya vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kiwanda kikubwa zaidi katika eneo la Magharibi ya Asia cha utengezaji dawa za kinga ya maradhi ya saratani kilifunguliwa wiki katika mji wa Karaj ulioko magharibi mwa mji mkuu Tehran.
Kiwanda hicho cha uzalishaji dawa za kinga ya kansa kilifunguliwa wiki iliyopita katika hafla iliyohudhuriwa na Waziri wa Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu, Daktari Seyyed Hassan Ghazizadeh Hashemi.
Kwa kuzingatia vikwazo ambavyo Marekani imeiwekea Iran, na kutokana na uwezekano wa kutokea matatizo ya kudhamini dawa kwa ajili ya raia wanaosumbuliwa na maradhi thakili, yakiwemo ya kansa, sklerosisi ya sehemu nyingi kwa kifupi MS na mengineyo, shirika moja la utengezaji dawa hapa nchini limeweza kuzalisha dawa zenye ubora wa kiwango cha juu kwa ajili ya wagonjwa wa saratani na MS, unaojulikana pia kama ugonjwa sugu wa njia za pumzi zilizofungana.
Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 8 Mei mwaka huu, rais wa Marekani, Donald Trump alichukua uamuzi wa upande mmoja wa kutangaza kujitoa nchi yake katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA sambamba na kurejeshwa tena katika awamu mbili vikwazo vya nyuklia vya nchi hiyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Vikwazo hivyo vya Marekani vinawalenga moja kwa moja raia wa kawaida wa Iran, licha ya madai ya Washington ya kuukana ukweli huo.
Hii ni pamoja na kwamba, mnamo tarehe 3 ya mwezi uliopita wa Oktoba, Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu, ICJ ilitangaza ustahiki ilionao wa kuchunguza mashtaka yaliyofunguliwa na Iran dhidi ya Marekani na kupitisha uamuzi wa kuitaka Washington ifute vikwazo ilivyoweka vya dawa, chakula, masuala ya kibinadamu na sekta ya usafiri wa anga dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.

Shirika moja la Iran limefanikiwa kuuza pea 14,000 za soksi zilizoundwa kwa teknolojia ya nano kila mwaka katika nchi jirani hasa Pakistan na Jamhuri ya Azerbaijan.
Kwa mujibu wa Baraza la Kitaifa la Iran la Ubunifu wa Teknolojia ya Nano, kuna shirika moja la Iran ambalo katika kipindi cha miezi sita iliyopita, limefanikiwa kuuza pea 14,000 za soksi za nano katika nchi hizo mbili.
Baraza hilo limesema kuwa awali soko kubwa la soksi za nano zilizoshonwa Iran lilikuwa ni Pakistan lakini soko hilo sasa limeenea katika Jamhuri ya Azerbaijan.
Mkuu wa shirika hilo, Gholamreza Khatibifard amesema soksi za nano za Iran zimeanza kupata umaarufu katika Jamhuri ya Azerbaijan na hivyo ana matumaini kuwa soko hilo litazidi kuimarika.
Soksi za nano zilizotengenezwa Iran zina uwezo wa kukabiliana na bakteria, ukungu, harufu mbaya na jasho. Amesema mali ghafi zote zinazotumika katika kushona soksi hizo hutengenezwa na mashirika ya Iran.
Kwa mujibu wa tarifa za Idara ya Forodha ya Iran, tani 214 za soksi za wanawake zenye thamani ya dola milioni mbili ziliuzwa katika masoko ya nchi jirani katika kipindi cha miezi mitano ya kwanza ya mwaka 2017.
Iran pia inauza soksi zake za nano katika nchi za Ulaya kama vile Uhispani na Norway.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, ustawi wa sayansi na teknolojia nchini Iran unafanyika kwa malengo ya amani na kibinadamu na katu hakuna malengo yasiyo ya kimaadili na haribifu. Ishaq Jahangiri Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyasema hayo Jumamosi mjini Tehran katika kikao cha kufunga Kongamano la Tatu la Kimataifa la Seli Shina. Aliongeza kuwa, katika kadhia ya nyuklia, Iran imetuhumiwa pasina haki na sasa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA, umetoa ripoti kadhaa ambazo zimethibitisha kuwa shughuli za nyuklia za Iran zinafanyika kwa malengo ya amani. Jahangiri ameashiria vikwazo vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran na kusema: "Wairani wamebadilisha vitisho kuwa fursa na hawataruhusu vizingiti vyovyote katika mkondo wao wa ustawi wa sayansi na teknolojia."Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran ina nguvu kazi yenye masomo ya juu na ya kipekee.
Ameongeza kuwa, Iran inakaribisha ushirikiano na vituo muhimu vya sayansi na teknolojia duniani.Pembizoni mwa mkutano huo kulizinduliwa mafanikio ya hivi karibuni ya Iran katika uga wa seli shina na tiba.Kongamano la Tatu la Kimataifa la Seli Shina lilianza Jumatano wiki iliyopita mjini Tehran na lilimaliza shughuli zake Jumamosi.
Wakati huo huo, akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Sorena Sattari Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya Sayansi na Teknolojia alisema mashirika ya Iran ambayo msingi wake ni elimu na utafiti au knowledge-based yamepelekea nchi hii kuongoza katika uga wa seli shina na tiba ya kukarabati seli na tishu za mwanadamu. Amesema ustawi huo wa Iran utaimarisha nafasi ya nchi hii katika uga wa sayansi na teknolojia. Aidha Sattari amesema ustawi wa sayansi na teknolojia utawawezesha vijana wa nchi hii kukuza utajiri na ajira kwa kuuza bidhaa zao nje ya nchi. Sattari amebaini kuwa hivi sasa Iran imeweza kuzishinda nchi zingine za Mashariki ya Kati hasa Uturuki na pia utawala bandia wa Israel katika uga wa teknolojia ya seli shina.
Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya Sayansi na Teknolojia alisema pia kuwa hivi sasa kuna mashirika 120 ya Iran yanayojishughulisha katika uga wa seli shina na kuongeza kuwa miaka michache iliyopita ilikuwa ni ndoto kuwa na mashirika mengi katika uga huo hapa nchini. Anasema hivi sasa serikali imeweka mkakati maalumu wa kustawisha teknolojia ili iwe sehemu ya utamaduni na kwa njia hiyo kuimarisha msingi wa sayansi na teknolojia nchini.

Na hivi karibuni Laurean Rugambwa Bwanakunu Mkurugenzi Mtendaji wa Bohari ya Dawa (MSD) alitangaza mpango wa idara yake wa kutumia ndege zisizo na rubani au droni kusambaza dawa katika maeneo ya ambali ambayo ni vigumu magari kufika. Akizungumza Alhamisi iliyopita, alisema hivi sasa wanatekeleza mradi wa majaribio wa kutumia droni ambazo zinateremesha dawa katika Kisiwa cha Ukerewe katika Ziwa Viktoria. Amesema lengo la kutumia teknolojia ya kisasa ya droni ni kuboresha huduma za afya kote Tanzania. Ameongeza kuwa hivi karibuni watatangaza shirika ambalo limeshinda zabuni ya kuiuzia droni Bohari ya Dawa.
@@@@
Naam na kwa habari hiyo ya mpango wa Tanzania kutumia teknolojia ya droni kusambaza dawa katika maeneo ya mbali ndio tunafika mwisho wa makala yetu ya mafanikio ya sayasni na teknolojia duniani.