Feb 11, 2019 02:49 UTC
  • Jumatatu, tarehe 11 Februari, 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 5 Jamadithani 1440 Hijria sawa na Februari 11 mwaka 2019.

Tarehe 11 Februari miaka 40 iliyopita Iran ikuwa katika siku ya kihistoria itakayokumbukwa siku zote. Siku hiyo wananchi waliokuwa wakipiga takbira na kutoa nara za kimapinduzi chini ya uongozi wa Ayatullah Ruhullah Khomeini walihitimisha kipindi cha giza totoro katika historia ya Iran kwa kuung'oa madarakani utawala wa kidikteta wa Shah Reza Pahlavi. Wananchi wanamapinduzi wa Iran, wanaume kwa wanawake, vijana kwa wazee na watu wa matabaka yote walisimama kidete wakipambana na mizinga na vifaru vya jeshi la Shah na kujisabilia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kiislamu. Mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran yalienea nchini kote huku wafuasi wa Imam Ruhullah Khomeini wakiwa katika juhudi za kumaliza kabisa mabaki ya utawala wa kidhalimu wa kifalme.

Siku ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiiislamu nchini Iran

Wakati ilipotangazwa habari kwamba vifaru vya majeshi ya Shah vilikuwa njiani kuelekea Tehran kwa ajili ya kukandamiza harakati za mapinduzi zilizokuwa zinaelekea kileleni, wananchi wa miji mbalimbali walijitokeza na kupambana na majeshi hayo huku wakifunga njia na kuzuia misafara ya vifaru hivyo. Baadhi ya makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la Shah waliuawa na wananchi katika mapambano hayo na kulilazimisha jeshi kutopendelea upande wowote. Siku hiyo pia wananchi wanamapinduzi walitwaa Shirika la Redio na Televisheni la Iran kutoka kwenye udhibiti wa jeshi. Muda mfupi baadaye lilitolewa tangazo katika redio ya taifa likitangaza kwamba "Hii ni Sauti ya Mapinduzi ya Kiislamu". Sauti hiyo ilitangaza ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuporomoka utawala wa kidhalimu wa kifalme uliotawala Iran kwa kipindi cha miaka 2500.

Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita Mzee Nelson Mandela kiongozi wa harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini aliachiwa huru baada ya kufungwa jela kwa kipindi cha miaka 27. Mandela alikamatwa na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela mwaka 1963 kwa sababu ya mapambano yake dhidi ya utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini. Mwaka 1991 alifikia makubaliano na makaburu wa nchi hiyo juu ya jinsi ya kukomesha utawala wa ubaguzi wa rangi na miaka kadhaa baadaye yaani mwaka 1994 alichaguliwa kuwa rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini.

Nelson Mandela

Siku kama ya leo miaka 8 iliyopita Hosni Mubarak aliyekuwa amejitangaza Rais wa maisha wa Misri aliondolewa madarakani kwa mapinduzi ya wananchi. Mubarak ambaye awali alikua makamu wa Rais Anwar Saadat wa Misri alishika madaraka ya nchi mwaka 1981 baada ya kuuawa kiongozi wa nchi hiyo. Saadat aliuawa kwa kumiminiwa risasi na Khalid Islanbuli kutokana na kutia saini makubaliano ya Camp David na utawala ghasibu wa Israel na kusaliti malengo ya taifa la Palestina. Baada ya kushika madaraka Mubarak alifuata nyayo za Saadat na hadi anang'olewa madarakani alikuwa kibaraka na mtekelezaji mkubwa wa siasa za Marekani na waitifaki wake katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika. 

Hosni Mubarak

Miaka 768 iliyopita katika siku kama ya leo sawa na tarehe 5 Jamadithani mwaka 672 alifariki dunia Jalaluddin Muhammad Balkhi maarufu kwa jina la Maulawi, mshairi mkubwa wa Iran katika mji wa Kunya ambao ni moja kati ya miji ya zamani ya Iran ulioko kusini mwa Uturuki ya leo. Maulawi alihesabiwa kuwa mshairi mkubwa na maarufu zaidi katika karne ya 9 Hijria Shamsia na miongoni mwa wanafikra na wachamungu wakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu. Maulawi alizaliwa mwaka 604 Hijria Shamsia katika mji wa Balkhi kaskazini mwa Afghanistan ya sasa na baada ya muda akahamia katika mji wa Konya akiandamana na baba yake. Baadaye alielekea Syria kwa ajili ya masomo ya juu. Miongoni mwa vitabu muhimu zaidi vya Maulawi ni Mathnawi Maulawi, Fihi ma Fihi, Maktubat Maualana na Rabaiyat.

Maulawi

Na siku kama ya leo miaka 2679 iliyopita mfalme wa kwanza wa Japan maarufu kwa jina la Jimmu alishika madaraka ya nchi. Kwa utaratibu huo mfumo wa kale zaidi na uliobakia kwa kipindi kirefu wa kifalme dunia ambao unaendelea hadi sasa, ulianzishwa. Wafalme wa Japan huwa na cheo cha heshima tu na Waziri Mkuu ndiye kiongozi wa masuala ya nchi.

Japan

 

Tags