Feb 19, 2019 14:01 UTC
  • Hadithi ya Uongofu (138)

Assalaamu alaykum, wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Hadithi ya Uongofu.

Kipindi chetu kilichopita kilizungumzia na kujadili maudhui ya kukufuru neema.  Tulisema kuwa, kukufuru neema ni kitendo ambacho kiko mkabala wa kitendo cha kushukuru neema. Kukufuru neema kunahesabiwa kuwa moja ya sifa mbaya. Aidha tulibainisha kwamba, kutoshukuru neema ambayo mja ametunukiwa na kuruzukiwa na Mwenyezi Mungu ni kama dhambi ambayo haina msamaha na magufira isipokuwa adhabu. Kadhalika tulieleza kwamba, kukufuru neema huwa chanzo cha kuondoka neema ambazo mwanadamu ameruzukiwa na Allah. Tulimalizia kipindi chote cha juma lililopita kwa kueleza kwamba, kukufuru neema ni miongoni mwa madhambi ambayo adhabu yake hutekelezwa haraka na hapa hapa duniani. Kipindi chetu cha leo ambacho ni sehemu ya 138 ya mfululizo huu kitazungumzia ujinga na ujahili ambao ni moja ya sababu za kutoshukuru na kukufuru neema za Allah. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Akili ni neema kubwa zaidi miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu ambayo Mola Muumba amemtunuku na kumruzuku mwanadamu. Hata hivyo watu ambao hawashukuru neema za Mwenyezi Mungu na kutozitumia kwa njia sahihi, hupelekea kuondoka na kutokomea neema hizo na siku baada ya siku, hukumbwa na ujinga na ujahili, kiasi kwamba, yumkini akafikia hatua ya kuikana kikamilifu haki. Imam Ali bin Abi Twalib AS amenukuliwa akitoa wasifu wa wajinga na majahili na hatua yao ya kukana na kuikataa haki kwa kusema kuwa:

Kwa hakika jahili na mjinga ni mtu ambaye anajiona msomi katika kitu ambacho hana elimu nacho na anatosheka na rai na mtazamo wake. Huwahesabu watu wenye mtazamo tofauti na yeye kwamba wanakosea. Kila anapokumbana na jambo ambalo halifahamu, hulikana na kulihesabu kuwa ni urongo. Husema kwa ujinga wake kwamba, mimi sikitambui kitu kama hiki na sikiamini! Mtu wa aina hii hana habari na ujahili wake. Kutokana na ujahili wake, hubakia katika ujahili na kukana haki. Hubakia akitangatanga katika ujahili na ujinga na huona na hufanya kiburi katika kutafuta elimu.

Katika Uislamu na Kitabu Kitakatifu cha Qur’ani ujinga na ujahili inatajwa kuwa sifa mbaya na isiyofaa na waumini wanatakiwa wajipambe na elimu na maarifa na hivo kujiweka mbali na madhara haribifu ujinga na ujahili. Hasa kwa kuzingatia kuwa, ujinga na ujahili hauna madhara katika maisha ya hapa duniani tu, bali ni hatari pia kwa ajili ya kesho akhera na humfanya mtu akumbwe na hatima mbaya.

Bwana Mtume SAW anaashiria nukta hii kwa kusema: Kheri ya dunia na akhera ni kwa akili na elimu na shari ya dunia na akhera ni kwa ujahili na ujinga.

Kwa hakika saada na ukamilifu wa mwanadamu una mafungamano makubwa na akili na maarifa yake. Uhusiano na mafungamano haya yanadhihiri na kuonekana zaidi katika maarifa na masuala ya kidini. Mwanadamu kwa kuondokana na ujinga na ujahili, anaweza kufahamu na kuainisha baya na zuri, jema na ovu na hivyo kufanya harakati katika njia sahihi. Ni kwa kuzingatia ukweli huu, ndio maana Imam Ali bin Abi Twalib AS analitambua suala la uongofu na upotovu wa mwanadamu kwamba, lina uhusiano na mafungamano na akili na ujinga wake. Anasema: Akili inatoa mwongozo na wokozi na ujinga utapoteza na kuangamiza. Hii ni kutokana na kuwa, akili inamuongoza na kumlingania mtu kuelekea upande wa imani, mambo mazuri ya kimaadili, kheri na ukamilifu. Kupitia akili, mwanadamu huweza kupambanua haki kutoka katika batili, kheri kutoka katika shari na njia sahihi katika hali ya kutangatanga na kutofahamu njia. Ukweli wa mambo ni kuwa, akili ni nuru ambayo kupitia kwayo Mwenyezi Mungu anaabudiwa na kupitia akili pepo hupatikana.

Kuhusiana na nukta hii, Imam Ja’afar Swadiq (AS) anasema: Akili ni ile ambayo kupitia kwayo Mwenyezi Mungu anaabudiwa na pepo inatafutwa kupitia kwake.

Hadithi ya Uongofu

Kwa hakika hadhi, sharafu na heshima ya mwanadamu ni kulingana na akili na hekima yake. Kuna wakati ujahili humpelekea mwanadamu kufanya mambo ambayo humshusha na kumpunguzia hadhi mhusika na kumfanya duni na dhalili. Imam Ali bin Abi Twalib AS amenukuliwa akisema kuwa, kuna mtu azizi kiasi gani ambaye ujahili wake ulimdhalilisha. Ni kwa kuzingatia uhakika huo ndio maana ili kukabiliana na ujinga na ujahili kuna haja ya kuwa na elimu, maarifa na muono wa mbali.

Katika utamaduni wa Kiislamu pia, ujira na malipo ya watu na kujikurubisha kwao kwa Mwenyezi Mungu yameainishwa kulingana na akili zao. Bwana Mtume Muhammad SAW amenukuliwa akisema kuwa, Siku ya Kiyama Mwenyezi Mungu atawapandisha daraja waja kulingana na kiwango cha akili na hekima zao na kwa msingi huo ndipo watakapopata daraja ya kujikurubisha na Mwenyezi Mungu.

Qur’ani tukufu pia imetilia mkazo kuhusiana na thamani ya hali ya juu ya akili, hekima na busara na inayatambua madhambi ya akthari ya watu wa motoni kkuwa chimbuko lake ni kutotumia akili.

Kutumia akili na hekima kumepewa umuhimu mkubwa sana katika maneno na mafundisho ya Imam Kadhim (as) kwa kadiri kwamba, mtukufu huyo  anafungamanisha saada ya dunia na akhera na utumiaji wa akili. Mtukufu huyo anawausia wanadamu kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya akili akisema: "Mtu anayetaka kujitosheleza bila ya kuwa na utajiri, kuwa na utulivu wa moyo bila ya kuhusudiwa na watu wengine na anayetaka usalama katika dini yake, anapaswa kumwomba Allah akamilishe akili yake.

Utumiaji wa akili, kama ilivyo katika amali nyingine, unahitaji mazoezi na juhudi kubwa. Ili kuweza kutayarisha uwanja mzuri wa kutumia akili na hekima, mwanadamu anapaswa kufanya mambo kadhaa maishani ikiwa ni pamoja na kuketi na maulamaa na wanahekima na busara na kushauriana nao mara kwa mara. Kuhusu suala hilo Imam Kadhim (as) anasema: "Kuketi na watu wenye dini humpa mtu sharafu na heshima ya dunia na Akhera na kushauriana na watu wenye busara na hekima huzidisha baraka, ustawi na taufiki ya Mwenyezi Mungu..."

Imam Mussa al Kadhim (as) alikuwa akiwamihiza Waislamu kujiepusha kuketi na kusuhubiana na watu majahili na wajinga, akisisitiza kwamba suala hilo linamuweka mtu mbali na njia ya haki na ufanisi. Anasema: Jiepushe kuketi na kusuhubiana na wajinga na wakimbie kama unavyokimbia mnyama mkali anayewinda wanadamu."  

Tunakamilisha kipindi chetu cha leo kwa kusema kuwa, kawaida watu ni maadui wa yale ambayo hawajui.

Aya ya 39 katika Surat Yunus inasema:

Bali wameyakanusha wasio yaelewa ilimu yake kabla hayajawajia maelezo yake. Kadhaalika walio kabla yao walikanusha vile vile. Basi angalia jinsi ulivyokuwa mwisho wa madhalimu hao.

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu cha juma hili cha Hadithi ya Uongofu.

Hadi tunakapokutana tena wiki ijayo ninakuageni nikikutakieni kila la kheri.

Tags