Jumatano, 10 Aprili, 2019
Leo ni Jumatano tarehe Nne Sha'aban 1440 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 10 Aprili 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1414 iliyopita, yaani tarehe 4 Shaaban mwaka 26 Hijria, alizaliwa Abbas bin Ali bin Abi Talib mashuhuri kwa lakabu ya Abul Fadhl. Mama yake ni Ummul Banina, ambaye aliolewa na Imam Ali bin Abi Twalib (A.S) baada ya kufariki dunia bibi Fatima Zahra AS. Abul Fadh al-Abbas alikulia katika familia ya watu adhimu kama baba yake Ali (as) kaka zake Imam Hassan na Hussein na dada yake mtukufu Zaynab (as). Alimpenda sana kaka yake Hussein Bwana wa mashahidi kiasi kwamba alisabilia roho na nafsi yake katika ardhi ya Karbala akimtetea yeye na risala yake. Abbas alifahamika mno kutokana na elimu, ukweli na uchaji Mungu wake. Kutabahari kwake kielimu kuliwafanya watu wengi warejee kwa ajili ya kutatuliwa masuala mbalimbali ya kielimu. Siku ya kumbukumbu ya kuzalIwa Abul Fadhl Abbas inatambuliwa hapa nchini Iran kama Siku ya Vilema wa Vita. ***
Miaka 206 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Joseph-Louis Lagrange, mwanahisabati maarufu wa Ufaransa. Lagrange alizaliwa mwaka 1736 Miladia huko mjini Turin, Italia. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni pamoja na kitabu cha 'Uchunguzi wa Umekanika' kwa kimombo Analytical mechanics ambacho alikiandika kwa kipindi cha miaka 25. ***
Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, aliuawa Emiliano Zapata mwanamapinduzi mashuhuri wa nchini Mexico kupitia njama maalumu dhidi yake. Wahindi Wekundu wa Mexico wanamfahamu Zapata kama mrekebishaji wa jamii na mwokozi wao. Tangu mwishoni mwa mwaka 1910 Miladia sanjari na kutoa nara za kupigania uhuru, alibeba pia silaha na kuwaongoza Wahindi Wekundu katika kupambana na wavamizi na kufanikiwa kuzikomboa ardhi za nchi hiyo zilizokuwa zimeporwa. ***
Miaka 73 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Aprili 1946, kundi la mwisho la wanajeshi wa Ufaransa liliondoka huko Lebanon. Ufaransa ilizikalia kwa mabavu Lebanon na Syria wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Lebanon ilipata uhuru mwaka 1945 na mwaka huo huo ikatia saini makubaliano ya kuondoka askari wa Uingereza na Ufaransa katika ardhi ya nchi hiyo ambayo yalianza kutekelezwa Aprili 1946. ***
Katika siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, sawa na tarehe 10 Aprili 1973, makachero wa Shirika la Ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD waliwaua maafisa watatu wa Palestina huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon. Katika kuendeleza jinai zake dhidi ya Wapalestina, miaka kumi baadaye utawala wa Kizayuni wa Israel yaani tarehe 10 Aprili 1983, ulimuuwa huko Ureno, Isam Sartawi aliyekuwa mshauri wa Yassir Arafat kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi ya Palestina (PLO). Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukitumia mauaji ya kigaidi dhidi ya viongozi wa mapambano ya ukombozi wa Palestina kwa ajili ya kuendelea kujipanua na kuzima mapambano ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina. ***
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita inayosadifiana na 21 Farvardin 1367 Hijria Shamsia, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia mji wa Marivan wa magharibi mwa Iran na kukilenga kijiji kimoja kwa mabomu ya kemikali. Raia kadhaa waliuawa shahidi na wengine kujeruhiwa katika jinai hiyo ya utawala wa Saddam Hussein. Jamii ya kimataifa na hasa nchi za Magharibi zilinyamazia kimya jinai hiyo na badala yake zilitoa misaada zaidi ya silaha za kemikali kwa nchi hiyo. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 20 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 21 Farvardin 1378 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Meja Jenerali Ali Sayyad Shirazi, Kaimu Kamanda Mkuu wa majeshi yote na mmoja kati ya makamanda shupavu wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baada ya kufyatuliwa risasi na vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqiin mjini Tehran. Meja Jenerali Shirazi alikuwa mwanaharakati wa mapinduzi, na alitupwa gerezani mara kadhaa wakati wa utawala wa Shah, na hatimaye aliachiliwa huru baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Meja Jenerali Sayyad Shirazi aliwahi kuwa Kamanda wa Jeshi la nchi kavu wakati wa vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. ***