Apr 16, 2019 04:35 UTC
  • Jumanne tarehe 16 Aprili, 2019

Leo ni Jumanne tarehe 10 Sha'aban 1440, Hijiria, sawa na tarehe 16 Aprili 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1018 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Abu Abdillah Abdul-Baqi, mmoja wa malenga mashuhuri wa karne ya tano Hijiria. Mbali na kusoma kwa maulama wakubwa wa fasihi, pia alipata fursa ya kushiriki masomo ya kidini kwa maulama wakubwa wa mji huo na kuweza kustafidi  na elimu tofauti, hususan elimu ya hadithi na kadhalika. Mashairi ya Abu Abdillah Abdul-Baqi yalikuwa ya kipekee kiusomaji mashairi na ameacha athari nyingi katika uwanja huo.

Abu Abdillah Abdul-Baqi

Siku kama ya leo miaka 686 iliyopita, alifariki dunia Majdud-Din Abul-Fawaaris, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa nchini Iraq na baada ya kuhitimu elimu ya msingi, alianza kusoma kwa maulama wakubwa na kufanikiwa kufikia daraja ya juu kielimu na kutokea kuwa mwalimu. Majdud-Din Abul-Fawaaris, alitabahari sana katika elimu za fiqhi, usulu fiqhi, hadithi, theolojia, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Kuna athari nyingi kutoka kwa msomi huyo mkubwa wa Kiislamu na mojawapo ni kitabu kinachoitwa 'Kanzul-Fawaaidi.'

Majdud-Din Abul-Fawaaris

Siku kama ya leo miaka 175 iliyopita, alizaliwa mjini Paris Anatole France, mwandishi na malenga wa Kifaransa. Tangu akiwa kijana alivutiwa na elimu ya fasihi na uandishi ambapo kutokana na kipawa alichokuwanacho akatokea kupata umashuhuri katika uga wa mashairi na fasihi. Anatole France ameacha athari mbalimbali kikiwemo kitabu kinachoitwa 'Mfalme wa Sabai.' Mwaka 1914 Anatole France alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na kuandika kitabu alichokipa jina la 'Uasi wa Malaika' huku akifariki dunia mwaka 1924.

Anatole France

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita, Charles Spencer Chaplin mcheza filamu na msanii mashuhuri wa tasnia ya filamu alizaliwa katika viunga vya mji wa London  Uingereza. Alipokuwa mdogo, alianza na michezo ya kuigiza na kupata umashuhuri hatua kwa hatua. Mwanzoni mwa ujana wake, Chaplin alielekea nchini Marekani kwa lengo la kutengeneza filamu. Lakini kutokana na kutengeneza filamu ya ukosoaji na yenye kuonyesha mshikamano wake na matabaka ya kimasikini katika jamii ya Marekani, serikali ya nchi hiyo ilitoa amri ya kubaidishwa kwake mnamo mwaka 1952. Chaplin alikumbana na mazingira magumu ya kufanya shughuli zake nchini Marekani na hivyo akahamia Uswisi pamoja na mkewe. Msanii huyo katika tasnia ya filamu alifariki dunia mwaka 1977.

Charles Spencer Chaplin

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, Wazayuni waliokuwa na silaha walishambulia kambi ya zamani wa askari wa Uingereza huko Palestina na kuua Wapalestina 90 na kujeruhi wengine wengi. Kwa upande mmoja, maafa hayo yalitokea wakati askari wa Uingereza walipokuwa wakiondoka katika kambi hiyo na kurejea nchini kwao; na kwa upande wa pili, Wazayuni walikuwa wameshadidisha mauaji hayo ya Wapalestina wasio na hatia kwa lengo la kuasisi dola haramu la Israel. Matokeo ya mauaji hayo yaliyofanyika kwa uratibu wa Uingereza, yalikuwa kuuawa idadi kubwa ya Waislamu wa Palestina na kutangazwa dola bandia la Israel mwezi mmoja baadaye.

Jinai za Wazayuni dhidi ya wakimbizi wa Palestina

Siku kama ya leo miaka 22 iliyopita ulitokea mlipuko mkubwa ulisababishwa na mtungi wa gesi na kusambaza moto kwenye mahema ya Mahujaji huko Mina kilomita 10 kutoka katika mji mtakatifu wa Makka. Mahujaji wasiopungua 343 walifariki dunia na wengine 1,290 kujeruhiwa katika tukio hilo. Aidha mahema yasiyopungua elfu sabini yaliteketea katika moto huo. Hilo linahesabiwa kuwa tukio kubwa la pili la janga la moto kutokea wakati wa msimu wa Hija. Mnamo mwaka 1975, ulitokea moto mkubwa huko Mina nchini Saudi Arabia uliosababisha vifo vya maelfu ya Mahujaji na wengine wengi kujeruhiwa. Kutokana na matukio hayo, Saudi Arabia ililazimika kuweka katika eneo la Mina, mahema yasiyoshika moto ili kuepusha ajali za moto.

Mlipuko mkubwa ulisababishwa na mtungi wa gesi