Jumatano, Mosi Mei, 2019
Leo ni Jumatano tarehe 25 Sha'aban 1440 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe Mosi Mei 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 130, iliyopita yaani tarehe Mosi Mei 1889, ilitangazwa rasmi kuwa 'Siku ya Wafanyakazi Duniani'. Tarehe Mosi Mei 1886, zaidi ya wafanyakazi elfu 40 walifanya maandamano katika mji wa Chicago nchini Marekani kwa shabaha ya kudai haki zao. Wafanyakazi hao walitaka nyongeza za mishahara, kuboreshwa suhula za maeneo yao ya kazi na uadilifu kazini. Maandamano hayo yaliingiliwa na askari polisi, na matokeo yake yakawa ni idadi kadhaa ya wafanyakazi hao kuuawa na wengine kujeruhiwa. Inafaa kuukumbusha hapa kuwa, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, viongozi na maafisa wa serikkali hapa nchini wakizingatia daraja la mfanyakazi katika Uislamu, daima wamekuwa na uzingatiaji maalumu kwa tabaka hili la jamii. ***
Katika siku kama ya leo miaka 123 iliyopita, Naser al-Din Shah Qajar, mfalme wanne wa ukoo wa Qajar nchini Iran aliuawa na hivyo kuhitimisha kipindi cha giza cha miaka 50 cha historia ya Iran. Tukio hilo liliandaa uwanja wa kutokea Mapinduzi ya kupigania katiba. Naser al-Din Shah Qajar aliauawa kwa kupigwa risasi na Mirza Reza Kermani mpigania ukombozi. Reza Kerman alikuwa mmoja wa wafuasi wa Sayyid Jamal al-Din Asadabadi. Kipindi kirefu cha utawala wa Naser al-Din Shah Qajar kinahesabiwa kuwa kipindi muhimu cha historia ya Iran katika zama za utawala wa ukoo wa Qajar. ***
Miaka 104 iliyopita katika siku kama ya leo, wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia yalitokea mapigano makali kati ya majeshi ya Urusi na Ujerumani katika eneo la Krakow lililoko nchini Poland. Jeshi la Ujerumani lililoyashinda majeshi ya Urusi kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1914, katika vita hivyo kwa kutumia mizinga liliyashinda majeshi ya Urusi na hatimaye kulidhibiti eneo la Poland. Kushindwa kwa majeshi ya Urusi katika Vita vya Kwanza vya Dunia na hali kadhalika hali mbaya iliyokuwemo nchini humo, ni miongoni mwa sababu muhimu za kujiri mapinduzi ya Kikomonisti nchini humo mwaka 1917, na hatimaye nchi hiyo kujiondoa kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia. ***
Na siku kama ya leo miaka 15 iliyopita, nchi nyingine 10 za Ulaya zilijiunga na Umoja wa Ulaya na kufikisha jumla ya nchi 25 wanachama wa umoja huo. Nchi hizo ni Estonia, Latvia, Lithuania, Poland, Jamhuri ya Czeck, Slovakia, Hungary, Slovenia, Cyprus, na Malta. Licha ya kuwa kujiunga nchi hizo kulihesabiwa na jumuiya hiyo kuwa moja ya mafanikio, lakini kuna ufa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya nchi wanachama wa zamani na wapya. Vilevile mwaka 2007, nchi za Romania na Bulgaria zilijiunga na umoja huo na jumla ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kufikia 27. ***