Jun 24, 2019 06:36 UTC
  • Ulimwengu wa Spoti, Juni 24

Hujambo mpenzi msikilizaji wa na karibu tutupie jicho baadhi ya matukio muhimu ya spoti yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa…..karibu.....

Voliboli: Iran yaendelea kupeta

Timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendeleza ubabe wake katika Wiki ya 4 ya Mashindano ya Ligi ya Mataifa ya mchezo huo katika eneo Azarbaijan, kaskazini magharibi mwa nchi. Timu hiyo ya wanaume ya Iran siku ya Jumamosi iliipa kichapo cha mbwa Australia kwa kuizaba seti 3-0 za (25-19, 25-19, 25-14). Kama ada, mchezaji Amir Ghafour ndiye aliyeongoza kwa kuifungia Iran pointi nyingi katika mchezo huo uliopigwa katika Ukumbi wa Michezo wa Rezazadeh katika mji wa Ardabil, kaskazini magharibi mwa nchi. Kwa ushindi huo Iran imekuwa timu ya kwanza kujikatia tiketi ya fainali inayofahamika kama Volleyball Nations League Final Six.

Iran yapigwa 'STOP' na Ufaransa

 

Siku ya Jumapili, Iran ilishuka dimbani kuvaana na Ufaransa, ambapo rekodi yake ya ushindi ilitiwa doa. Hii ni baada ya kuzabwa seti 3-0 na Wafaransa.

Kabla ya michuano hii ya Wiki ya Nne, Iran ilikuwa imeng'ara pia katika mechi zake za Wiki ya Tatu mjini mjini Oroumiyeh. Timu hiyo ya wanaume ya Iran iliipa kichapo cha mbwa Russia, kwa kuizaba seti 3 kwa mtungi, za 25-20, 26-24 na 25-23 katika mchezo uliochezwa katika Ukumbi wa Michezo wa Ghadir, kabla ya kuikung'uta Poland seti 3-2 za (25-20, 21-25, 18-25, 25-17, 15-8). 

Mashindano haya yanaofahamika kama Volleyball Men's Nations League yanayosimamiwa na Shirikisho la Voliboli Duniani FIVB, yalianza Mei na yatamalizika mwezi ujao wa Julai. Duru ya mwisho ya mashindano haya yatafanyika katika Ukumbi wa Credit Union 1 Arena mjini Chicago nchini Marekani.

Futsal: Iran yamaliza ya 3

Timu ya taifa ya vijana ya mchezo wa futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeibuka ya tatu katika mashindano ya mabingwa wa mchezo huo wa soka la ukumbini yaliyofanyika hapa nchini. Timu hiyo ya taifa ya Iran ya futsal kwa vijana wenye chini ya umri wa miaka 20 iliigaragaza Indonesia kwa mabao 9-1 katika mchezo wa Jumamosi wa kutafuta mshindi wa tatu katika Uwanja wa Pour Sharifi mjini Tabriz, makao makuu ya mkoa wa Azerbaijan Mashariki.

Timu ya taifa ya vijana ya mchezo wa futsal ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Iran ililazimika kuwapoza mashabiki wake kwa ushindi huo wa tatu, kwani ilikuwa imewaghadhabisha kwa kuchachawizwa mabao 8-4 na Japan katika mchuano wa nusu fainali. Barobaro wa Iran, Salar Aghapour ametawazwa kuwa mfungaji wa mabao mengi katika mashindano hayo, kwani alifanikiwa kucheka na nyavu mara 8. Mjapani, Osawa Masashi ameteuliwa kuwa mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi kwenye michuano hiyo ya kikanda. Iran mara ya mwisho kutwaa taji la mashindano hayo ya AFC U-20 Futsal Championship ilikuwa mwaka 2017.

Michuano ya Afcon yang'oa nanga kwa kishindo Misri

Mafarao wa Misri, ambao ni wenyeji wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Afcon wameanza michuano hiyo kwa ushindi hafifu wa bao 1-0 licha ya kucheza na timu chovu ya Zimbabwe. Katika mchuano huo uliopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Cairo, kiungo Mahmoud Trezeguet ndiye alifunga bao la pekee la mechi kabla ya muda wa mapumziko.

Mshambuliaji wa Liverpool Mo Salah alikaribia kutia kimyani bao la pili katika kipindi cha pili lakini kipa wa Zimbabwe Edmore Sibanda akaupangua mkwaju wake. Salah alivurumisha makombora ya hapa na pale katika kipindi cha kwanza lakini hakuna lililoweza kuzibusu nyavu.

Kombe la AFCON

 

Zimbabwe walionekana kucheza kwa kujiamini lakini tatizo likawa ni mashambulizi dhaifu. Siku ya Jumapili wawakilishi wa Afrika Mashariki katika michuano hiyo, Tanzania na Kenya walianza vibaya kampeni yao ya angalau kufika hatua ya 16 bora. Hii ni baada ya kucharazwa mabao 2-0 kila mmoja katika mchezo wake.  Timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars ilishuka dimbani katika Uwanja wa Juni 30 katika mechi yake ya ufunguzi dhidi Senegal, ambapo walikubali kichapo cha mabao 2-0, licha ya kushangiliwa moja kwa moja uwanjani hapo na makumi ya mashabiki na wabunge kadhaa. Magoli ya Senegal yalifungwa na fowad wa Inter Milan Keita Balde kwenye dakika ya 28 huku la pili likifungwa kwenye dakika ya 64 na Keprin Diatta aliyechangia kupatikana bao la kwanza.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike na wachezaji wake wanahisi wangali wana fursa ya kurekebisha kasoro na mapungufu na kufanya vizuri katika mechi zijazo, huku wakikiri kuwa Senagal ni miamba.

Wakati huohuo, timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars pia waliangukia pua, na kuchabangwa mabao 2-0 katika uwanja ambao Tanzania walinyolewa mjini Cairo. Mkwaju wa penati wa dakika ya 37 uliopachikwa wavuni na mfungaji mabao bora wa Ligi Kuu ya Qatar, Baghdad Bounedjah, na bao la pili la kiungo wa kati wa Manchester City, Riyad Mahrez dakika tano baadaye yalitosha kulizamisha jahazi la Kenya katika mchuano wao huo wa kufungua ngoma.

Mo Salah ambaye pia anakipiga Liverpool

 

Uganda Cranes imeanza vyema mashindano haya kwa kuisasambua Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mabao 2-0 mjini Cairo. Mapema Jumapili pia, bao la kujifunga la dakika za majeruhi la Itamunua Keimuine wa Namibia lilitosha kuipa Morocco alama tatu za bwerere.  Madagascar ambayo ndiyo mara ya kwanza inatia guu katika michuano ya Afcon, ilitosheka na alama moja, baada ya kuambulia sare ya mabao 2-2 ilipoovaana na Guinea katika mchuano wake wa ufunguzi. Burundi licha ya kujitutumua muda mwingi katika mchezo wake wa awali, lakini ilishindwa kufurukuta mbele ya Nigeria, na kujikuta ikikubali kulazwa bao 1-0.

Michuano hiyo ya Afcon ambayo iling'oa nanga tarehe 21 mwezi huu inatazamiwa kumalizika Julai 19. Mshindi wa kwanza atapewa donge nono la dola milioni 4.5 huku akifuatiwa na mshindi wa pili ambae atapewa dola milioni 2. Wataofuzu nusu fainali watazawadiwa dola milioni 1, na timu zitakazotinga robo fainali dola laki 8.

Kombe la Dunia la Wanawake

Licha ya wawakilishi wa Afrika katika Kombe la Dunia la Wanawake, timu za Nigeria na Cameroon kufuzu hatua ya 16 bora ya fainali za michuano hiyo inayoendelea nchini Ufaransa, lakini zimeshindwa kufurukuta mbele ya mibabe ya soka duniani. Cameroon ilipata tiketi hiyo baada ya kushinda mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya New Zealand kwa mabao mawili kwa bila wakati Nigeria ilikuwa ikisubiri matokeo ya Thailand ambayo ilitandikwa mabao 2-0 kwa Chile na hivyo kuipa upenyo Nigeria wa kufuzu hatua hiyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa mataifa ya Afrika kufuzu hatua ya mtoano ya fainali za kombe la dunia kwa wanawake. Afrika Kusini ni wawakilishi pekee wa Afrika walioshindwa kufua dafu katika fainali hizo baada ya kufungwa michezo yote ya hatua ya makundi. Ujerumani imejikatia tiketi ya robo fainali baada ya kuisasambua Nigeria mabao 3-0 katika mchuano wa Jumamosi uliogaragazwa katika Uwanja wa Alpes. Kichapo kama hiki kiliwakumba Waafrika wenzao, Cameroon waliposhuka dimbani kuvaana na Uingereza siku ya Jumapili.

Fainali hizo za Kombe la Dunia la Wanawake zilizoanza Juni 7 zitafikia tamati Julai 7.

Dondoo za Hapa na Pale

Shirikisho la soka duniani FIFA limethibitisha kuwa katibu mkuu wake Fatma Samoura ameteuliwa kuwa 'Mjumbe mkuu wa Fifa kwa Afrika' katika jitihada za kuimarisha utawala kwenye mchezo wa soka barani Afrika. Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) hivi karibuni limekuwa likichunguzwa katika masuala tofuati yanayohusisha uongozi na usimamazi. Fatma, raia wa Senegal atachukua usukani kwa miezi sita kuanzia Agosti mosi, huku wadhifa huo 'ukiwa na uwezo wa kuidhinishwa upya kwa makubaliano ya taasisi zote mbili'. Rais wa CAF Ahmad Ahmad amekuwa akichunguzwa hivi karibuni kwa tuhuma za ufisadi, ukiukaji wa imani na udanganyifu, ikiwemo kuhojiwa na maafisa wa Ufaransa mjini Paris mapema mwezi huu kabla ya kuachiliwa huru bila kushtakiwa, huku kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 59 anayetoka Madagascar akisema tuhuma zote zinazomuandama ni za uongo. Rais wa shirikisho la soka duniani Gianni Infantino awali alikabiliwa na upinzani mkali, kutoka kwa mmoja wa makamu wake juu ya mpango wa kumteua katibu mkuu Fatma Samoura, kwenye majukumu ya ziada ya kulichunguza shirikisho la soka la afrika CAF.

Rais waFIFA, Gianni Infantino awali alikabiliwa na upinzani mkali wa kumteua Fatma Samoura

Mbali na hayo, Rais wa zamani wa chama cha soka Ulaya UEFA Michel Platini amejikuta katika wakati mgumu kufuatia kushikiliwa na kuhojiwa kwa tuhuma za rushwa nchini Ufaransa. Platini alijiuzulu nafasi yake ya Urais wa UEFA kwa tuhuma za rushwa. Uchunguzi unaondelea na uliomfanya Platini akamatwe unahusiana nafasi ya kupewa uenyeji Qatar wa Kombe la dunia 2022, kitu ambacho kinahisiwa kuwa kilipitishwa kwa rusha na sio halali, hivyo Platini ni miongoni wa wanaotuhumiwa kwa rushwa katika sakata hilo.

………………..TAMATI..…………..