Jun 26, 2019 02:48 UTC
  • Jumatano, tarehe 26 Juni, 2019

Leo ni Jumatano tarehe 22 Shawwal 1440 Hijria sawa na Juni 26 mwaka 2019.

Miaka 183 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, aliaga dunia Rouget de Lisle, malenga na mtunzi wa nyimbo za kimapinduzi wa Ufaransa. Rouget alihudumu pia jeshini na alikuwa akisoma mashairi ya kuwahamasisha wanamapinduzi wa Ufaransa na kutunga nyimbo za hamasa na za kusisimua. Rouget de Lisle alitunga wimbo wa kimapinduzi kwa jina "La Marseillaise" ambao baadaye ulikuwa wimbo rasmi wa taifa.

Rouget de Lisle

Miaka 74 iliyopita sawa na tarehe 26 Juni 1945, mkutano wa kimataifa wa San Fransisco ulimaliza shughuli zake katika mji unaojulikana kwa jina hilo huko Marekani kwa kupasishwa hati ya Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ambao ulikuwa wa kwanza wa kimataifa kuwahi kufanyika baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ulihudhuriwa na wawakilishi wa nchi 50 waitifaki katika vita hivyo.

Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita kisiwa cha Madagascar kilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Uingereza na Ufaransa zilianzisha ushindani wa kuidhibiti nchi hiyo ya Kiafrika katika karne ya 18. Mwishoni mwa karne ya 19 Ufaransa ilikidhibiti kikamilifu kisiwa cha Madagascar. Hata hivyo wananchi wa Madagascar waliendesha mapambano mengi ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Kifaransa, miongoni mwake ni yale ya mwaka 1947 ambapo karibu watu elfu 80 waliuawa.

Bendera ya Madagascar

Na tarehe 26 Juni miaka 22 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliitangaza kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Kuwatetea Wahanga wa Mateso kwa lengo la kufuta kabisa vitendo hivyo viovu duniani. Vitendo vya mateso vina historia ndefu duniani lakini ilitazamiwa kuwa maovu hayo yangehitimishwa kikamilifu katika zama hizi hususan baada ya kupasishwa nyaraka kadhaa zinazohusiana na haki za binadamu. Hata hivyo bado kuna nchi zinazotumia mateso kuwakandamiza wapinzani. Marekani ambayo inajinadi kuwa mtetezi mkubwa wa haki za binadamu ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kutesa wapinzani kote duniani. Vilevile utawala wa Kizayuni wa Israel unaosaidiwa na kuungwa mkono na nchi za Magharibi hususan Marekani umekuwa ukiwatesa na kuwanyanyasa raia wa Palestina katika korokoro na jela zake za kutisha.

Tags