Jul 01, 2019 07:07 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Julai Mosi

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kuanzia Michuano ya AFCON hadi Kombe la Dunia kwa Wanawake....

Voliboli: Iran yaicharaza Bulgaria

Timu ya taifa ya voliboli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeendeleza ubabe wake katika Wiki ya 5 ya Mashindano ya Ligi ya Mataifa ya mchezo huo katika mji wa Plovdiv, kusini mwa Bulgaria. Timu hiyo ya wanaume ya Iran siku ya Jumamosi iliisasambua Bulgaria kwa kuizaba seti 3-0 za (25-23, 25-23, 25-21). Mohammadjavad Manavinejhad ndiye aliyeongoza kwa kuifungia Iran pointi nyingi katika mchezo huo ambapo alifunga alama 14.

Iran ikipambana na Marekani

 

Kabla ya mpambano huo, Iran iliitandika Serbia seti 3-1 na pia ikafanikiwa kumkandamiza mwenyeji Bulgaria seti 3-0. Hata hivyo siku ya Jumapili, timu hiyo ya Iran ilizabwa seti za moja kwa moja na Marekani, ingawaje katika mchuano wa kukamilisha tu ratiba. Katika mchezo huo uliopigwa huko huko Bulgaria, Iran ilikubalia kutandikwa na Marekani seti 3-0 za (27-25, 25-21 na 25-20).

Katika Wiki ya 4 ya mashindano hayo, Iran ambayo imeshinda mechi zake 12 kati ya 15 za awali, iliiadhibu Australia kwa kuizaba seti 3-0 za (25-19, 25-19, 25-14). Timu hiyo ya Iran inayonolewa na Igor Kolakovic ilikuwa ya kwanza kujikatia tiketi ya fainali inayofahamika kama Volleyball Nations League Final Six baada ya kuifanya vibaya Serbia. Mashindano haya yanaofahamika kama Volleyball Men's Nations League yanayosimamiwa na Shirikisho la Voliboli Duniani FIVB, yalianza Mei na yatamalizika mwezi huu wa Julai. Fainali ya mashindano haya itafanyika katika Ukumbi wa Credit Union 1 Arena mjini Chicago nchini Marekani kati ya Julai 10 na 14.

Ligi ya Wanawake Iran; Shahdari Bam yatwaa ubingwa

Klabu ya soka ya Shahdari Bam imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ya Iran. Timu hiyo ilitwaa ubingwa huo siku ya Alkhamisi baada ya kuichabanga Zob Ahan mabao 2-1 katika mchezo wa aina yake uliopigwa katika Uwanja wa Foolad Shahr mjini Isfahan. Na kwa kuwa kutangulia sio kufika, bao la mapema la Safoora Jafari katika kipindi cha kwanza halikutosha kuipa Zob Ahan ushindi, kwani mambo yalipinduliwa juu chini katika kipindi cha pili.

Wachezaji wa klabu ya Shahrdari Bam iliyotwaa ubingwa

 

Zahra Ghanbari aliipa Shahdrari Bam bao la kusawazisha mambo katika kipindi cha pili kabla ya Mona Amoudi kulizamisha mzima mzima jahazi la Zoba Ahan. Klabu ya Shahdrai Bam inaongoza kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake ya Iran, kwani imebeba taji hilo mara sita sasa.

Michuano ya Afcon

Timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars ilipata ushindi wake wa kwanza, katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Afcon inayoendelea nchini Misri, baada ya kuwacharaza vijana wa Taifa Stars wa Tanzania mabao 3-2. Harambee Stars ilitoka nyuma na kupata ushindi huo muhimu, katika pambano hilo la timu hizo za Afrika Mashariki. Michael Olunga alikuwa nyota wa Kenya, baada kuifungia mabao mawili, baada ya Johanna Ommolo kuisawazishia nchi yake bao la pili. Tanzania walianza vema kwa kupata bao la mapema kupitia Simon Msuva, huku nahodha Mbwana Samatta akifunga bao la pili kabla ya kipindi cha mapumziko na hatimaye mchuano ukaishia kwa Taifa Stars kunyukwa maba 3-2 na Harambee Stars.

Wakenya wakishangilia ushindi goli la Harambee Stars

 

Kenya itacheza na Senegal usiku wa kuamkia Jumanne, kutafuta ushindi au sare ili ifuzu katika hatua ya 16 bora; huku Tanzania ambayo imepoteza mechi mbili, ikisalia na mechi ya kukamilisha ratiba (heshima) dhidi ya Algeria. Taifa Stars ilishuka dimbani kuvaana na Harambee Stsrs ikiwa na makovu ya masaibu iliyoyapata katika Uwanja wa Juni 30 mjini Cairo katika mechi yake ya ufunguzi ambapo walikubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka Senegal. Timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars ambao waliangukia pua pia katika mchuano wao wa ufunguzi kwa kuchabangwa mabao 2-0 na Algeria, walilazimika kucheza mchezo wa kasi ili kuhuisha matumaini ya kusonga mbele.

Uganda Cranes ambayo ilianza vyema mashindano haya kwa kuisasambua Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mabao 2-0 mjini Cairo, na kuwa matumaini ya nchi za Afrika Mashariki, ilidhalilishwa na mwenye Misri kwa kuzabwa mabao 2 bila jibu. Mabao ya Mohamed Salah ambaye pia anakipiga Liverpool katika (36) na Ahmed al-Mohammady wa Aston Villa dakika chache kabla ya mapumziko, yalitosha kulizamisha jahazi la vijana wa The Cranes katika mchuano huo.

Burundi imeendelea kuonyesha matokeo mabaya kwa kugaragazwa na Guinea mabao 2-0, huku mchuano wa Benin na Guine-Bissau ukiishia kwa sare tasa. Madagascar ambayo hii ndo mara ya kwanza inashiriki Afcon, imeendelea kuwashangaza wengi kwa matokeo yake mazuri. Siku ya Jumapili iliinyoa kwa chupa Nigeria, ambayo ni katika miamba ya soka ya Afrika. Super Eagles walicharazwa bila huruma mabao 2-0 na vijana wa kisiwa hicho cha kusini mashariki mwa Afrika, uwanjani Alexandria.

Wachezaji wa Madagascar wakishangilia goli na mkufunzi wao

 

Kwa matokeo hayo, Madagascar imetulia na kutuama kileleni mwa Kundi B ikifikisha pointi saba kufuatia kushinda mechi mbili na sare moja, ikifuatiwa na Nigeria iliyomaliza na pointi sita na zote zinasonga hatua ya 16 Bora. Zimbabwe kwa upande wake imeendelea kugeuzwa kichwa cha mwendawazimu, ambapo siku ya Jumapili ilisasambuliwa mabao 4-0 na Kongo DR. Mabao ya Batoto ba Kongo yalifungwa na Cedric Bakambu ambaye alicheka na nyavu mara mbili, huku mengine mawili yakitiwa kimyani na Jonathan Bolingi na Britt Assombalonga. DRC awali ilikuwa imepokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Uganda.

Kombe la Dunia la Wanawake

Uholanzi na Sweden zinatazamiwa kukutana katika mchezo wa aina yake wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Dunia kwa uande wa wanawake siku ya Jumanne. Uingereza pia itatoana jasho na Marekani kati mechi ya pili ya nusu fainali ya mashindano hayo yanayoendelea nchini Ufaransa. Hii ni baada ya timu hizo nne kufanya vyema katika mechi zao za robo fainali. Katika michuano hiyo ya robo fainali ya kuwania Kombe la Dunia katika mchezo wa soka kwa upande wa wanawake, Norway ilishuka dimbani kuvaana na Uingereza, katika uwanja wa Oceane, mjini Le Havre, ambapo Waingereza walipata ushindi wa magoli 3 kwa nunge.

Sweden ilijakatia tiketi Jumamosi baada ya kuichakaza Ujerumani mabao 2-1, wakati ambapo Italia ilikuwa inachezea mkong'oto, ambapo ilichabangwa mabao 2-0 na Uholanzi. Marekani ilipata ushindi hafifu wa mabao 2-1 ilipotoana udhia na mwenyeji Ufaransa. Fainali hizo za Kombe la Dunia la Wanawake zilizoanza Juni 7 zitafikia tamati Julai 7.

…………………TAMATI….…………