Jumatano tarehe 25 Disemba 2019
Leo ni Jumatano tarehe 28 Rabiuthani 1441 Hijria sawa na tarehe 25 Disemba 2019.
Siku kama ya leo miaka 2020 iliyopita, Nabii Issa Masih (AS) alizaliwa katika mji wa Bait Laham (Bethlehem) huko Palestina. Nabii Issa Masih alipewa uwezo na Mwenyezi Mungu wa kufanya miujiza mingi. Issa Masih AS alianza kuzungumza akiwa mdogo na kujibashiria unabii. Mwenyezi Mungu anaashiria tukio la kuzaliwa kwa Nabii Issa katika Qur'ani Tukufu katika Suratu Aal Imran aya ya 45 kwa kusema: Kumbukeni waliposema Malaika: "Ewe Mariam! Mwenyezi Mungu anakubashiria mwana kwa neno litokalo kwake; jina lake ni Masih, Issa mwana wa Maryam, mwenye hishima katika dunia na Akhera na miongoni mwa waliokurubishwa." Inafaa kuashiria hapa kwamba, tarehe 25 Disemba kila mwaka inajulikana kote duniani hasa kwa Wakristo kuwa ni Sikukuu ya Krismasi. Redio Tehran inatoa mkono wa baraka na fanaka kwa wafuasi wa kweli wa Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu.

Miaka 803 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Arabi, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Damascus. Alizaliwa mwaka 560 Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka, Halab (Aleppo) na Baghdad na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".
Miaka 376 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Isaac Newton, mwanafizikia, mwanahisabati na mwanafikra wa Kiingereza. Akiwa na umri wa miaka 24, Isaac Newton alifanikiwa kugundua kanuni muhimu ya makanika na alitambuliwa kama mwanasayansi mkubwa aliyepata umashuhuri. Newton alibainisha pia sheria tatu za mwendo yaani (Three laws of motion) katika kitabu chake alichokipa jina la Mathematical Principles of Natural Philosophy. Ugunduzi wa Isaac Newton ulikuwa msingi mkuu wa ugunduzi wa wasomi wengine kuhusu kanuni kuu za hisabati na uhandisi.
Miaka 354 iliyopita katika siku kama ya leo, mwafaka na tarehe 25 Disemba 1665, Ufaransa ilianzisha French East India Company katika kipindi cha utawala wa Mfalme Louis II ili kushindana kisiasa, kiuchumi na kikoloni na serikali ya Uingereza huko India. Uingereza ilikuwa imeasisi British East India Company miaka 66 kabla ya hapo. Vilitokea vita kadhaa baina ya tawala hizo mbili za kikoloni kwa shabaha ya kuikoloni ardhi ya India.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita aliaga dunia Charles Spencer Chaplin mcheza filamu na msanii mashuhuri wa tasnia ya filamu. Alipokuwa mdogo, alianza na michezo ya kuigiza na kupata umashuhuri hatua kwa hatua. Mwanzoni mwa ujana wake, Chaplin alielekea nchini Marekani kwa lengo la kutengeneza filamu. Lakini kutokana na kutengeneza filamu ya ukosoaji na yenye kuonyesha mshikamano wake na matabaka ya kimasikini katika jamii ya Marekani, serikali ya nchi hiyo ilitoa amri ya kubaidishwa kwake mnamo mwaka 1952. Chaplin alikumbana na mazingira magumu ya kufanya shughuli zake nchini Marekani na hivyo akahamia nchini Uswisi pamoja na mkewe.
Na siku kama ya leo miaka 40 iliyopita inayosadifiana na tarehe 25 Disemba 1979, viongozi watatu wa ngazi za juu wa Palestina waliuawa kigaidi na Shirika la ujasusi la utawala haramu wa Israel MOSSAD. Viongozi hao walikuwa Ali Hassan Salamah, afisa wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) aliyeuawa Beirut baada ya kutegwa bomu ndani ya gari lake, Samir Touqan mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya PLO huko Cyprus na Ali Nasser Yassin, shakhsia mwingine wa Palestina aliyekuwa mwakilishi wa PLO nchini Kuwait. Jinai hiyo ilidhihirisha tena jinsi utawala katili wa Israel unavyotumia ugaidi katika maeneo mbalimbali dunia kwa ajili ya kufikia malengo yake haramu.