SPOTI DEC 30
Ulimwengu wa Michezo, Disemba 30
Hujambo mpenzi msikilizaji na karibu katika dakika hizi chache za kutupia jicho baadhi ya matukio muhimu ya michezo yaliyojiri ndani ya siku saba zilizopita, kitaifa na kimataifa.
Sataranji: Iran yatwaa Kombe la Mataifa ya Asia
Timu ya taifa ya vijana ya mchezo wa sataranji (chesi) ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Asia katika mashindano yaliyofanyika nchini China. Timu hiyo ya mabarobaro wa Iran ilitwaa taji hilo Jumatano baada ya kuzoa jumla ya alama 16 katika duru tisa ilizoshiriki kwenye mashindano hayo ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 14. Timu hiyo ya chesi ya vijana wa Iran inaundwa na Sayyid Kian Pour Mousavi, Bardia Daneshavr, Abtin Atakhan, Mohammad Javad Khorshidi, na Hamid Reza Ebrahimi. Mongolia A imemaliza ya pili kwa kuchota pointi 15 huku China A ikifunga orodha ya tatu bora kwa alama 14 kwenye duru ya pili ya Kombe la Mataifa ya Asia. Mashindano hayo ya kikanda yalifanyika katika jiji la Shenzhen mkoani Guangdong nchini China kati ya Disemba 18 na 27.

Wakati huohuo, mwanasataranji nyota wa Iran, Alireza Firouzja ametawazwa kuwa mchezaji chesi kijana nambari mbili duniani, baada ya kushinda jumla ya michezo minane na kutoa sare katika michezo mitano. Firouzja alimzidi maarifa hasimu wake kutoka Azerbaijan katika kategoria ya kasi ya juu, na kutangazwa kuwa bingwa nambari mbili duniani baada ya kuzoa alama 10.5. Kwa ushindi huo, Alireza Firouzja anakuwa miongoni mwa wachezaji chesi 30 mabingwa wa dunia.

Kijana kutoka Ubelgiji ametwaa ubingwa katika kategoria hiyo. Huku hayo yakiarifiwa, binti wa Kiirani, Sara Sadat Khadem al-Sharieh ametwaa medali mbili za fedha katika kategoria ya kasi ya juu na blitz kwenye mchezo wa chesi.
Soka: Iran yatoa sare na Qatar
Timu ya vijana wenye chini ya umri wa miaka 23 ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku ya Jumamosi ililazimishwa sare ya mabao 2-2 iliposhuka dimbani kuvaana na Qatar katika mchezo wa kupasha moto misuli, kuelekea Mashindano ya Mabingwa wa Soka Asia 2020 nchini Thailand. Iran ilianza vizuri mchezo huo wa ugenini jijini Doha, kwani walikuwa kifua mbele kwa mabao mawili kwa nunge katika kipindi chote cha kwanza. Bao la kwanza la Iran lilifungwa na Reza Shekari kunako dakika 28, na dakika sita baadaye, Mehdi Ghaedi alifanya mambo kuwa mawili kwa mtungi kwa bao alilolifunga kupitia mkwaju wa ikabu.
Hata hivyo matokeo hayo yalipinduliwa na wenyeji katika kipindi kipindi cha pili kupitia magoli ya dakika za lala salama yaliyofungwa na Abdulrasheed Umaru Ibrahim. Mkufunzi wa timu hiyo ya Omid (Matumaini) ya Iran, Hamid Estili anasisitiza kuwa, mchezo ulikuwa mzuri na wanajiandaa kufanya vizuri zaidi katika mechi zijazo.

Iran imepangwa Kundi C pamoja na Uzbekistan, China na Korea Kusini katika mashindano hayo ya Asia ya mwaka ujao 2020 yanayofahamika kama AFC Under 23 Championship. Mashindano hayo yatafanyika nchini Thailand kati ya Januari 8 na 26. Nchi tatu zitakazoibuka kidedea zitajikatia tiketi ya kushiriki Michezo ya Olimpiki ya Julai mwaka ujao 2020 jijini Tokyo Japan. Timu hiyo ya soka ya vijana ya Iran inayonolewa na Hamid Estili na ambayo ilishiriki michezo ya Olimpiki mara ya mwisho mwaka 1976 jijini Munich, itaanza kampeni za kusaka tiketi ya Oimpiki ya Tokyo 2020 Januari 9 itapovaana na Uzbekistan.
Wachezaji wa Eritrea wazama Uganda
Jeshi la polisi nchini Uganda linaendelea kuwasaka wachezaji wa timu ya taifa ya soka ya Eritrea waliotokomea kusikojulikana baada ya kumalizika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ya Mashariki na Kati (CECAFA) iliyopigwa jijini Kampala. Msemaji wa CECAFA, Rogers Mulindwa amesema kwamba polisi inaendelea kuwatafuta wachezaji hao waliopotea kusikojulikana. Eritrea walifanikiwa kuingia hatua ya fainali ya michuano hiyo ambapo walipoteza kwa magoli 3-0 dhidi ya wenyeji wa michuano Uganda Alkhamisi ya wiki iliyopita.

Hii si mara ya kwanza kwa wachezaji wa Eritrea kuzamia wanapocheza ugenini. Itakumbukwa wameshawahi kufanya hivyo Botswana, Kenya, Angola na Tanzania. Mwezi Oktoba mwaka huu wachezaji watano wa chini ya miaka 20 walipotelea mjini Jinja, Uganda siku moja kabla ya kumalizika kwa michuano ya CECAFA U-20. Inaelezwa kuwa, wengi wa wachezaji soka wa Eritrea wamekuwa wakikataa kurejea nyumbani na kuomba hifadhi baada ya kucheza mechi ugenini. Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa linaloangazia haki za kibinadamu limekuwa likiituhumu serikali ya Eritrea kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.
Mayweather aongoza kwa malipo bora zaidi miongoni mwa wachezaji
Bingwa wa masumbwi duniani kwenye uzito wa kati kutoka nchini Marekani Floyd Mayweather ndiye mwanspoti anayelipwa malipo ya juu zaidi kuliko wachezaji wote duniani. Hii ni kwa mujibu wa orodha ya jarida la Forbes la Marekani ya wachezaji 10 wanaolipwa pesa nyingi zaidi duniani. Mayweather ambaye alistaafu lakini ametangaza kurejea kwenye ndondi tena alilipwa jumla ya pauni milioni 706 (dola 915) ndani ya miezi 12 iliyopita.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mayweather amewashukuru mashabiki na wadau wote waliopelekea ateuliwe kuwa kuwa mwamamichezo anayelipwa pesa nyingi kwa msimu wa tano mfululizo. Kwa mujibu wa orodha hiyo ya Forbes, mshambuliaji wa klabu ya Juventus, Mreno Cristiano Ronaldo anashikilia nafasi ya pili akilipwa dola milioni 800. Mshambuliaji wa Barcelona raia wa Argentina Lionel Messi ambaye alikuwa anaongoza orodha hiyo mwaka jana, mwaka huu ameshika nafasi ya tatu kwa kulipwa dola milioni 750. Lewis Hamilton, bingwa wa mashindano ya magari ya langalanga anafunga orodha ya kumi bora kwa kulipwa dola milioni 308.
Ligi ya EPL
Na tunatamatisha kwa kutupia jicho matokeo ya baadhi ya mechi zilizopigwa wikendi hii katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Nguli wa soka wa Iran, Alireza Jahanbakhsh alibubujikwa na machozi baada ya kufunga bao lake la kwanza ndani ya klabu ya Brighton inayocheza kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Wing'a huyo Muirani alimaliza ukame wa magoli kwenye mchezo wa wikendi wa Ligi Kuu ya EPL, wakati Brighton ilipochuana na Burnemouth. Jahanbakhsh ambaye alisainiwa na klabu hiyo ya Uingereza msimu uliopita wa joto kwa kima cha pauni milioni 17 alidondokwa na chozi baada ya kutikisa nyavu dakika tatu tu baada ya kuanza ngoma. Aaron Mooy aliongeza la pili na kuihakikishia ushindi klabu ya Brighton almaarufu Seagulls. Jahanbakhsh anakuwa mchezaji wa tatu wa Iran baada ya Ashkan Dejagah and Andranik Teymourian kufunga bao katika Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza. Mchezaji huyo Muirani amewaahidi mashabiki wake mazuri zaidi katika siku za usoni.

Mbali na hayo, klabu ya Arsenal siku ya Jumapili walijikuta wakiangukia pua tena, baada ya kugaragazwa mabao 2-1 na Chelsea licha ya kuupigia nyumbani katika Uwanja wa Emirates. Gunners walipoteza mchezo huo licha ya kuwa wa kwanza kuona lango la The Blues, kupitia goli la kichwa la Pierre-Emerick Aubameyang lililofungwa dakika 13 baada ya kupulizwa kipenga cha kuanza mchezo. Na kwa kuwa kutangulia sio kufika, The Blues walipundia mambo katika dakika za lala salama, kupitia magoli ya Jorge Luiz Frello Joginho dakika ya 83 na Tammy Abraham dakika ya 87.
Aidha siku ya Jumapili timu ya Liverpool ndani ya uwanja wao wa nyumbani wa Anfield iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Wolves. Sadio Mane alipachika bao pekee la ushindi dakika ya 42 kipindi cha kwanza lililodumu mpaka dakika ya 90. Ushindi huo unaifanya Liverpool izidi kujikita kileleni ikiwa na pointi 55. Man City wakiupigia nyumbani katika Uwanja wa Etihad waliwatia skulini Sheffiled United kwa kuwachachafya mabao 2-0. Mabao ya City yalifungwa na Sergio Aguero (52) na Kevin De Bruyne (82).
Leister City wapo katika nafasi ya pili wakiwa na alama 42 huku City wakilazimika kutuama katika nafasi ya tatu wakiwa na alama 41. Chelsea wapo katika nafasi ya nne wakiwa na alama 35 huku Manchester United ambao watafufua uhasama wao wa jadi na Arsenal tarehe Mosi, wakifunga orodha ya tano bora kwa alama 31.
……………….…..TAMATI.....................