Jumatatu tarehe 10 Agosti 2020
Leo ni Jumatatu tarehe 20 Dhulhija 1441 Hijria sawa na Agosti 10 mwaka 2020.
Siku kama ya leo miaka 1314 iliyopita alizaliwa Imam Mussa al Kadhim ambaye ni mmoja kati ya wajukuu watukufu wa Bwana wetu Muhammad (saw). Alilewa na baba yake Imam Ja'far Swadiq (as) na kuchota elimu na maarifa ya Kiislamu kutoka kwa mtukufu huyo kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Kadhim (as) alishika hatamu za Uimamu na uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35 na kukabiliana na mashaka mengi. Imam Kadhim (as) alipitisha kipindi kingi cha umri wake katika kuwazindua na kuwaelimisha Waislamu maarifa asili ya dini. Suala hili liliwatia hofu kubwa watawala wa Bani Abbas ambao walimkamata na kumfunga jela ili kumuweka mbali na Waislamu waliokuwa na kiu ya maarifa halisi ya dini yao. Imam Kadhim (as) alisifika kwa ukarimu mkubwa, uvumilivu na usamehevu. Tunatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kuadhimisha siku hii ya leo.

Siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, yalitiwa saini makubaliano yaliyojulikana kwa jina la The Treaty of Sèvres kati ya utawala wa Othmaniya uliokuwa umeshindwa katika Vita vya Kwanza vya dunia na waitifaki wake. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, utawala wa dola ya Othmaniya ulipoteza karibu asilimia 80 ya ardhi yake iliyokuwa ikiitawala, na kupunguza eneo ililokuwa ikilitawala kutoka kilomita mraba milioni tatu hadi kilomita mraba laki sita tu. Makubaliano hayo yalitambua rasmi makubaliano ya awali ya Ufaransa na Uingereza juu ya kugawana ardhi iliyokuwa ikitawaliwa na dola ya Othmania, ambapo Uingereza ilizitawala Iraq, Jordan na Palestina na Ufaransa nayo ilizitwaa na kuzidhibiti Syria na Lebanon.

Siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, vilianza vita vya miaka miwili kati ya Japan na China juu ya mzozo wa maeneo ya Yangtze na Canton ambayo yalikuwa maeneo ya kistratijia ya ardhi ya China. Canton ilikuwa bandari muhimu mno huko kusini mwa China ambayo Wachina walipigana vita vya miaka miwili kuilinda mbele ya uvamizi wa Wajapani. Hata hivyo na baada ya kupata hasara kubwa tarehe 25 Aprili 1939 bandari ya Canton ikatwaliwa na Japan. Utawala wa Japan uliendelea kujipanua katika ardhi ya China kwa kudhibiti maeneo mengine ya mashariki mwa nchi hiyo baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo Wajapani walilazimika kurudi nyuma kutokana na mapambano makali ya wananchi wa China.

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, kufuatia kushindwa kikamilifu Japan katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia na kwa mujibu wa maazimio ya Kongamano la Potsdam, maeneo ya kaskazini mwa Korea yalidhibitiwa na Jeshi Jekundu la Urusi ya Zamani. Kabla ya kushindwa Japan, maeneo hayo yalikuwa chini ya udhibiti wa nchi hiyo. Aidha baada ya siku chache maeneo ya kusini ya Korea yalidhibitiwa na Marekani. Kudhibitiwa maeneo ya kaskazini na kusini ya Korea ulikuwa utangulizi wa kugawanywa ardhi hiyo katika nchi mbili za Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini.
