Alkhamisi tarehe 27 Agosti mwaka 2020
Leo ni Alkhamisi tarehe 7 Muharram 1442 Hijria sawa na Agosti 27 mwaka 2020.
Tarehe 7 Muharram mwaka 61 Hijria kamanda wa jeshi la Yazid bin Muawiya, Umar bin Sa'd aliliamuru jeshi lake kumzuia maji ya Mto Furati Imam Hussein (as) na watu waliokuwa katika msafara wake. Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kumzingira mjukuu wa Mtume (saw) akiwa na jeshi kubwa katika medani ya Karbala alimwandikia barua Umar bin Sa'd akimtaka amlazimishe Imam Hussein kutangaza utiifu wake kwa mtawala dhalimu na fasiki Yazid bin Muawiya. Vilevile alimwandikia barua nyingine akimtaka kumzuia Imam Hussein na wafuasi wake wasitumie maji ya Mto Furati. Imam Hussein, ndugu, watoto na masahaba zake waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka huo wakiwa na kiu tena kandokando ya maji ya Mto Furati.

Siku kama ya leo miaka 385 iliyopita, alifariki dunia Lope de Vega, mwandishi mkubwa wa Uhispania. Vega alizaliwa mwaka 1562 na baada ya kuhitimu masomo yake katika chuo kikuu, alijiunga na jeshi la kujitolea. Taratibu akaanza kuonyesha kipawa chake katika michezo ya kuigiza na masuala mengine na hivyo kuwavutia watu wengi. Lope de Vega anajulikana kuwa mwanzilishi wa michezo ya kuigiza kitaifa nchini Uhispani.
Siku kama ya leo miaka 250 iliyopita, alizaliwa Georg Wilhelm Friedrich Hegel mwanafalsafa mkubwa wa Ujerumani. Licha ya msomi huyo kufundisha katika vyuo mbalimbali na kuandika vitabu tofauti, lakini bado alikuwa masikini. Kufuatia uvamizi wa jeshi la Napoleon dhidi ya Ujerumani mwaka 1806, Hegel alivutiwa na shakhsia ya kamanda huyo Kifaransa. Alibainisha hatua za historia na kuamiani kuwa, muelekeo wa harakati ya kihistoria huainishwa na Mwenyezi Mungu na kwamba hata malengo ya historia ni hivyo. Katika kubainisha itikadi yake, Georg Wilhelm Friedrich Hegel aliandika vitabu kadhaa katika uwanja huo. Hegel alifariki dunia mwaka 1831.
Tarehe 27 Agosti mwaka 1896, yaani miaka 124 iliyopita katika siku kama hii ya leo, kulitokea vita vya muda mfupi zaidi duniani visiwani Zanzibar. Jengo la kihistoria mjini Unguja linalojulikana kwa jina la Beit al-Ajaib lililojengwa na Sultan Barghash bin Said huko Forodhani kisiwani Unguja, lilishambuliwa kwa mizinga ya manowari za Uingereza. Hatua hiyo ilichukuliwa kufuatia ugomvi uliozuka baina ya wana wawili wa Sultani wa Zanzibar. Watoto hao walijulikana kwa majina ya Said Barghash Khalid na Said Hamud bin Muhammed, na ugomvi wao ulihusiana na utawala na kwamba nani anapaswa kurithi kiti cha ufalme. Vita hivyo viliendela kwa dakika 45 tu na kuwa vita vifupi zaidi duniani.
Na katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, yaani tarehe 27 Agosti mwaka 1991, nchi ya Moldova iliyoko mashariki mwa Ulaya ilipata uhuru. Kwa mujibu wa kumbukumbu za historia nchi hiyo ilikaliwa kwa mabavu na tawala, kaumu na nchi mbalimbali zikiwemo, Ukraine, Russia, Romania na utawala wa Othmania. Baada ya mapinduzi ya kikomunisti nchini Russia, Moldova iliungana na Romania. Mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Moldova ilikaliwa kwa mabavu na Urusi. Hata hivyo baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti, nchi hiyo ikajikomboa na kupata uhuru.
