Jumapili tarehe 30 Agosti mwaka 2020
Leo ni Jumapili tarehe 10 Muharram mwaka 1442 Hijria sawa na Agosti 30 mwaka 2020.
Katika siku kama ya leo miaka 1381 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, katika hali ambayo, majeshi ya Yazid yalikuwa yamejiandaa kikamilifu kumshambulia Imam Hussein AS na masahaba zake katika ardhi ya Karbala, Imam alimtuma ndugu yake aliyesifika kwa ushujaa mkubwa yaani Abul Fadhl Abbas akawaombe maadui hao wampe fursa aupitishe usiku huo kwa Swala na kunong'ona na Mola wake. Usiku huo Imam Hussein aliwakusanya wafuasi wake na baada ya kumhimidi Mwenyezi Mungu na kumsalia Mtume, aliwaambia: ''Kila anayetaka, aitumie fursa iliyobakia ya giza la usiku kwa ajili ya kuyanusuru maisha yake, kwani hakuna atakayebaki hai hapo kesho tutakapokabiliana na jeshi la Yazid.'' Hata hivyo masahaba na wafuasi waaminifu na waumini wa kweli wa mtukufu huyo walikuwa wameshakata shauri la kujitolea mhanga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hadi tone la mwisho la damu zao. Usiku huo wa kuamkia Ashuraa yaani tarehe 10 Muharram, uwanja wa Karbala ulikuwa medani ya ibada kwa mashujaa ambao licha ya kuwa wachache kwa idadi lakini walisimama imara kama mlima na hawakumuacha Imam na kiongozi wao hata dakika moja.
Siku kama ya leo miaka 1375 iliyopita Ubaidullah Bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa Iraq, na aliyehusika na umwagaji damu mkubwa katika mauaji ya Karbala, aliuawa na jeshi la Mukhtar al-Thaqafi. Katika siku ya Ashura mwaka 67 Hijiria, yaani miaka sita baada ya kujiri tukio la mauaji ya Karbala na katika siku sawa na ile aliyotoa amri kwa jeshi lake kumuua Imam Hussein na wafuasi wake, naye (Ubaidullah Bin Ziyad) aliuawa na jeshi la Mukhtar chini ya kamanda Ibrahim Bin Malik al-Ashtar, katika pwani ya mto wa 'Khadhir' karibu na mji wa Mosul. Katika vita hivyo kati ya jeshi la watu wa Sham lililokuwa likiongozwa na Ubaidullah Bin Ziyad na jeshi la Mukhtar, majeshi elfu 70 ya Sham yalishindwa vibaya na Ibahim na kupelekea Ibn Ziyad kuangamizwa.
Siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, alizaliwa Ernest Rutherford, mtaalamu mkubwa wa fizikia wa nchini Uingereza maarufu kwa jina la baba wa nishati ya nyuklia. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali eneo alikozaliwa, Ernest alielekea katika mji wa kielimu wa Cambridge na kujiunga na chuo kikuu cha mji huo. Kuanzia mwaka 1919 Rutherford alitokea kuwa mhadhiri mwenye tajriba katika uga wa fizikia chuoni hapo, huku akijiunga na jumuiya ya kifalme ya mjini London hapo mwaka 1903. Mwaka 1904, msomi huyo alisambaza kitabu chake alichokipa jina la ‘Shughuli za Mionzi’. Baadaye Ernest Rutherford aliongoza kundi la utafiti katika chuo kikuu cha Manchester, kundi ambalo haraka liliweza kuandaa nadharia mpya kuhusiana na muundo wa atomiki. Mwaka 1908 Miladia, msomi huyo alitunukiwa zawadi ya Nobel kutokana na shughuli zake hizo na kupata umaarufu mkubwa katika uga huo.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Jamhuri ya Azerbaijan ilitangaza uhuru wake kutoka Urusi ya zamani. Ardhi ya Azerbaijan ilitekwa na kukaliwa kwa mabavu na silsila ya Kiirani ya Wasasani tangu mwanzoni mwa karne ya Tatu Miladia na katika kipindi kikubwa cha historia yake ilikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Vita kati ya Urusi ya zamani na Iran vilijiri mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia, kufuatia kupenda kujitanua kwa utawala wa kifalme wa Tsar huko katika Umoja wa Kisovieti. Iran ilipata pigo katika vita hivyo na kupelekea sehemu moja ya ardhi ya kaskazini ya Azerbaijan kukaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani mwaka 1813 kwa mujibu wa mkataba wa Golestan.
Na siku kama ya leo miaka 21 iliyopita, wananchi wa Timor ya Mashariki huko kusini mashariki mwa bara Asia walishiriki katika kura ya maoni na kuchagua kujitenga nchi hiyo na Indonesia. Kisiwa cha Timor ya Mashariki sambamba na visiwa vingine vya Indonesia kilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kireno mwaka 1511 Miladia. Timor Mashariki iliunganishwa na Indonesia mwaka 1976.