Ijumaa tarehe 11 Septemba 2020
Leo ni Ijumaa tarehe 22 Muharram 1442 Hijria sawa na tarehe 11 Septemba 2020.
Siku kama ya leo miaka 982 iliyopita alifariki dunia msomi mkubwa wa Kiislamu, Sheikh Muhammad bin Hassan Tusi, ambaye ni mashuhuri kwa jina la Sheikhul Twaaifa. Sheikh Tusi alizaliwa katika mji wa Tus kaskazini mwa Iran na akaelekea Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu ya juu baada ya kukamilisha elimu ya msingi. Alipata elimu kwa wanazuoni mashuhuri wa Iraq na miaka kadhaa baadaye akaweka msingi wa chuo kikuu cha kidini cha Najaf. Kituo hicho cha kidini kina historia ya miaka elfu moja na ni moja ya vituo muhimu mno vya elimu ya Kiislamu. Sheikh Tusi ameandika vitabu vingi sana katika taaluma mbalimbali. Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya mwanazuoni huyo wa Kiislamu ni tafsiri ya Qur'ani tukufu ya al Tibyan na vitabu vya hadithi na fiqhi vya al Istibsar na al Tahdhiib.
Miaka 72 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Muhammad Ali Jinnah, mwasisi wa Pakistan. Jinnah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Jinnah alikuwa miongoni mwa shakhsiya walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kitamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu wa India.
Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, Jenerali Agustino Pinoche kamanda wa wakati huo wa vikosi vya majini vya Chile aliipindua serikali halali ya Salvador Alande katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani. Alande ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Chile, alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1970.
Miaka 19 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 11 Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York huku ndege moja ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington. Ndege ya nne ililengwa ikiwa katika anga ya Pensylvania na kuangushwa. Baadhi ya ghorofa za jengo la Biashara ya Kimataifa ziliporomoka na sehemu ya jengo la Pentagon pia ikaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Karibu watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa mtandao wa al Qaida uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia, ndio uliohusika na mashambulizi hayo. Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi.