Jan 02, 2021 01:37 UTC
  • Jumamosi, Pili Januari, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 18 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1441 Hijria sawa na tarehe Pili Januari 2021 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 1114 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria alifariki dunia Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh mshairi na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Abdu Rabbuh alibobea mno katika mashairi. Athari mashuhuri zaidi ya msomi huyo ni kitabu cha al Iqdul Fariid ambacho kinahusiana na historia, lugha na mashairi. ***

Ahmad bin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibn Abdu Rabbuh

 

Miaka 992 iliyopita katika siku kama ya leo, Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa jina la Najjashi aliaga dunia huko Samarra, Iraq akiwa na umri wa miaka 78. Najjashi alikuwa alimu na msomi mkubwa katika karne ya tano Hijria na alibobea na kutabahari katika elimu ya hadithi na wapokezi wa hadithi. Kitabu cha Rijali ni miongoni mwa vitabu muhimu vya msomi huyo wa Kiislamu. ***

Abu al-Abbas Ahmad bin Ali maarufu kwa jina la Najjashi

 

Katika siku kama ya leo miaka 155 iliyopita leo, alizaliwa Gilbert Murray, mshairi na malenga wa Australia. Akiwa na umri wa miaka 11 Murray alielekea nchini Uingereza na baada ya kumaliza masomo ya juu katika Vyuo Vikuu nchini humo, alifundisha taaluma ya utamaduni na fasihi ya Kigiriki katika Chuo Kikuu cha Oxford. Murray alifariki dunia mwaka 1957 na kuacha athari za vitabu kadhaa kama vile, 'Historia ya Fasihi ya Ugiriki ya Kale' na 'Imani, Vita na Siasa'. ***

 

Katika siku kama ya leo miaka 101 iliyopita, alizaliwa Isaac Asimov, mwandishi na mkemia maarufu wa Kimarekani aliyekuwa na asili ya Russia. Asimov alivutiwa mno na elimu ya kemia na akafanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika taaluma hiyo. Msomi huyo alifanya utafiti na uhakiki mkubwa wa elimu ya kemia na taaluma nyingine. Hata hivyo jambo lililomtofautisha na wasomi wengine ni uwezo wake wa kuarifisha sayansi mbalimbali kwa lugha nyepesi kwa watu hususan tabaka la vijana. Isaac Asimov ameandika karibu vitabu 270 katika nyanja mbalimbali za sayansi, hisabati na sayansi za jamii. ***

Isaac Asimov

 

Miaka 42 iliyopita katika siku kama ya leo kulifanyika mkutano wa Guadeloupe kati ya viongozi wa serikali za Marekani, Uingereza, Ujerumani ya Magharibi na Ufaransa kwa ajili ya kuchunguza masuala kadhaa muhimu ya kimataifa hususan Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran. Mkutano huo ulifanyika katika kisiwa cha Guadeloupe kilichoko magharibi mwa Bahari ya Atlantic ambacho ni koloni la Ufaransa. Katika mkutano huo uliofanyika siku 40 kabla ya ushindi kamili wa harakati ya mapinduzi ya wananchi wa Iran washiriki wote walikiri kwamba, Mfalme wa wakati huo wa Iran Shah Pahlavi ataondolewa madarakani isipokuwa Jimmy Carter rais wa wakati huo wa Marekani ndiye pekee aliyekuwa na matumaini ya kubakia madarakani utawala wa Shah kwa msaada wa jeshi. Haya hivyo mkutano huo wa Guadeloupe haukuwa na mbinu ya kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu ya wanancdhi wa iran na iliishia kukiri nguvu kubwa ya mapinduzi hayo na mustakbali wake mwema. ***

mkutano wa Guadeloupe

 

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Dei 1367 Hijria Shamsia, ujumbe wa Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliwasilishwa kwa Mikhail Gorbachev kiongozi wa mwisho wa Umoja wa Kisovieti akimlingania dini ya Kiislamu na kumtaka aachane na fikra za Kimaksi. Katika sehemu moja ya ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tatizo kuu la nchi yako si suala la umiliki, uchumi wala uhuru, bali ni kutokuwa na imani ya kweli juu ya Mwenyezi Mungu; na tatizo hilo ndilo lililoitumbukiza au litakaloitumbukiza Magharibi katika mporomoko wa kimaadili na kuifanya igonge ukuta. Tatizo lenu kubwa ni kupigana vita visivyokuwa na faida dhidi ya Mwenyezi Mungu." Mwishoni mwa ujumbe huo Imam Khomeini alisema: "Tokea sasa Ukomonisti unapaswa kutafutwa kwenye majumba ya makumbusho ya kisiasa duniani; kwani hauwezi kukidhi mahitaji halisi ya mwanadamu." Imam Khomeini alimuusia Gorbachev akisema: "Nakutaka ufanye uchunguzi wa kina kuhusu Uislamu, sio kwa sababu Uislamu na Waislamu wanakuhitajia wewe, hapana, bali kutokana na thamani za hali ya juu na za ulimwengu mzima za dini hiyo ambayo inaweza kuwa wenzo wa ufanisi na uokovu wa mataifa mbalimbali na kukidhi matatizo makubwa ya mwanadamu."

Mikhail Gorbachev

 

Katika siku kama ya leo miaka 5 iliyopita yaani tarehe Pili Januari 2016 utawala wa Saudi Arabia ulimuua mwanazuoni wa Kiislamu Sheikh Nimr Baqir al-Nimr. Baqir al Nimr aliyekuwa mwanazuoni wa Kiislamu wa madhehebu ya Shia alizaliwa tarehe 21 Juni mwaka 1959 katika mji wa Awwamiyya huko mashariki mwa Saudi Arabia. Alipata elimu ya msingi katika mji huo na mwaka 1400 Hijria yaani mwaka 1989 alielekea Tehran nchini Iran na kupata elimu katika chuo cha kidini cha Qaim kilichoasisiwa na Ayatullah Sayyid Muhammad Taqi Mudarrisi. Baada ya kupata elimu katika chuo hicho kwa kipindi cha miaka 10 Sheikh Nimr alikwenda Syria na kuendelea kutafuta elimu zaidi katika Chuo cha Kidini cha Bibi Zainab (as). Aliporejea Saudi Arabia, Sheikh Nimr aliasisi kituo cha kidini cha al Imam al Qaim katika mji wa Awwamiyya ambacho kiliweka jiwe la msingi la kuanzishwa Kitiuo cha Kiislamu hapo mwaka 2011. Mwanazuoni huyo wa Kiislamu daima alikuwa akikosoa siasa za ukandamizaji na kibaguzi za utawala wa kifalme wa Saudia na alifungwa jela mara kadhaa kutokana na kusema haki na kweli. Mara ya mwisho Sheikh Baqir Nimr alikamatwa tarehe 8 Julai mwaka 2012 katika maandamano makubwa ya Waislamu wa Kishia ya kupinga ubaguzi na ukandamizaji wa utawala wa Aal Saud na tarehe 15 Oktoba msomi huyo wa Kiislamu alihukumiwa kifo cha kukatwa kichwa kwa panga na kusulubiwa kadamnasi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kula njama dhidi ya utawala wa nchi hiyo. Hukumu hiyo ilitekelezwa tarehe Pili Januari mwaka 2016. Kuuawa kwa msomi na mwanaharakati huo kulipingwa vikali na jumuiya za kikanda na kimataifa za kutetea haki za binadamu. ***

Sheikh Nimr Baqir al-Nimr.

 

Na mwaka mmoja uliopita katika siku kama ya leo, Luteni Jenerali Qassem Suleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, aliuawa shahidi katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad nchini Iraq kwa amri ya moja kwa moja ya Rais Donald Trump wa marekani. Shahidi Qassim Suleimani alizaliwa tarehe 20 Isfand 1335 Hijria Shamsia katika mji wa Kerman.  Wakati wa utoto na kuinukia kwake aliupitisha akiwa pamoja na baba yake. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuundwa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH alijiunga na kikosi hicho. Wakati wa kuanza vita vya kulazimishwa vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran, Qassim Suleimani akawa akitoa mafunzo kwa brigedi za kijeshi mjini Kerman na kuzituma katika medani ya vita. Mwaka 1360 Qassim Suleimani akateuliwa kuwa kamanda wa kikosi cha 41 cha Tharallah. Kikosi hicho chini ya uongozi w Qassim Suleimani kilitekeleza operesheni nyingi wakati wa vita vya kujihami kutakatifu kama Walfajr 8, Karbala 4, Karbala 5 na kadhalika. Mwaka 1389 akateuliwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuwa, Kamnada wa Kikosi cha Qusd cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH. Baada ya kuibuka kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq na Syria, Luteni Jenerali Qassim Suleimani alihudhuria katika medani za vita za mataifa hayo akiitikia wito wa viongozi wa nchi hizo na kuwa na nafasi kubwa katika kuliangamiza kundi hilo la kigaidi. Hatimaye aliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Ijumaa ya tarehe 3 Januari 2020 pamoja na Abu Mahdi al-Muhandis, aliyekuwa Naibu Mkuu wa Al-Hashdu-Sha'abi pamoja na wenzao wengine wanane katika shambulio la anga lililofanywa na jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani kwa amri ya rais wa nchi hiyo Donald Trump.*** 

Shahidi Qassem Suleimani,

 

Tags