Feb 21, 2021 02:40 UTC
  • Jumapili, 21 Februari, 2021

Leo ni Jumapili tarehe 9 Rajab 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 21 Februaria 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 521 iliyopita, alizaliwa Abdi Bik Shirazi, mtaalamu mkubwa wa historia wa Iran maarufu kwa jina la Navidi, huko mjini Shirazi. Abdi Bik Shirazi alikuwa miongoni mwa waandishi wa historia ya Tahmasp Safavid, huku akiwa na utaalamu pia katika elimu ya fasihi. Athari kubwa ya mwanahistoria huyo ni kitabu kinachozungumzia silsila ya utawala wa Safavi nchini Iran. Katika kitabu hicho Abdi Bik Shirazi alifafanua habari za utawala huo kuanzia mwaka 978 Hijiria. ***

Abdi Bik Shirazi,

 

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, inayosadifiana na 21 Februari 1916 vilianza vita vikubwa vya umwagikaji damu vilivyojulikana kwa jina la 'Verdun' kati ya Ujerumani na Ufaransa. Vita hivyo vilivyoendelea kwa muda wa miezi kumi vilimalizika kwa kushindwa vikosi vya jeshi la Ujerumani na wanajeshi karibu milioni moja wa nchi hizo mbili kuuawa. Tukio hilo ni miongoni mwa sababu za kushindwa Ujerumani kwenye Vita vya Kwanza vya Dunia. ***

Vita vya Verdun

 

Katika siku kama ya leo miaka 100 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 3 Isfand mwaka 1299 Hijria Shamsia, Uingereza ilitekeleza siasa zake za kikoloni kwa kufanya mapinduzi ya kijeshi nchini Iran. Njama hiyo ya mapinduzi ilipangwa na maafisa wa serikali ya Uingereza waliokuwa mjini Tehran wakishirikiana na baadhi ya maafisa usalama wa mji huo. Wafanya mapinduzi waliudhibiti mji mkuu baada ya mapigano ya muda mfupi, na Ahmad Shah Qajar akalazimika kumteua Reza Khan kuwa Kamanda Mkuu wa majeshi. Miaka minne baadaye Reza Khan ambaye alikuwa akiungwa mkono na kusaidiwa sana na Waingereza kutokana na kukandamiza harakati za ukombozi za wananchi alifanywa mfalme wa Iran hadi mwaka 1320 Hijria Shamsia, ambapo aliondolewa madarakati na Waingereza wenyewe na kupelekwa uhamishoni baada ya kuegemea upande wa Ujerumani katika Vita  Vikuu vya Pili vya Dunia. ***

 

Siku kama ya leo miaka 63 iliyopita, wananchi wa Misri na Syria walishiriki kwenye kura ya maoni ya kuunganisha nchi mbili hizo chini ya Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Wananchi wa nchi hizo mbili walimchagua Jamal Abdul-Nasser kiongozi wa wakati huo wa Misri, kuwa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu. Baada ya kupita miezi kadhaa, Yemen nayo ilijiunga kwenye muungano huo. Hata hivyo muungano huo haukudumu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwani Syria ilitangaza kujitoa kwenye muungano huo kutokana na kutoridhishwa na uongozi wa Jamal Abdul-Nasser.***

Marais wa Misri na Syria wakati huo wakitia saini makublaiano ya kuanzisha Jamhuri ya Muungano wa Kiarabu.

 

Miaka 55 iliyopita katika siku kama ya leo, Malcolm X, Mmarekani mweusi aliuawa baada ya kushambuliwa na magaidi nchini humo. Malcolm X alizaliwa mwaka 1925, na wakati alipokuwa kwenye rika la ujana alifahamiana na makundi ya vijana wa Kiislamu na hatimaye kusilimu. Itikadi za mwanaharakati huyo wa Kiislamu ziliwachukiza watawala wa Marekani na makundi ya ubaguzi wa rangi nchini humo. Malcolm X aliuawa akihutubia mkutano. Alikuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa, Wamarekani weusi ambao wanakandamizwa na kubaguliwa na serikali ya Marekani wanaweza kujipatia uhuru na uadilifu chini ya mwavuli wa utawala wa Kiislamu. ***

Malcolm X

 

Siku kama ya leo miaka 37 iliyopita, wapiganaji shupavu wa Iran walianzisha operesheni ya 'Khaybar' dhidi ya majeshi ya Iraq, kwenye vita vya kulazimishwa vilivyoazishwa na utawala wa Baath wa Saddam Hussein. Katika operesheni hiyo iliyofanyika katika eneo la Hoor al Hoveyzah kusini magharibi mwa Iran, wapiganaji shupavu wa Iran walifanikiwa kuvuka maji na kukiteka kisiwa chenye utajiri mkubwa wa mafuta cha Majnoon, kilichoko karibu na mji wa Basra kusini mashariki mwa Iraq.  Mbinu tata za kijeshi zilizotumika katika oparesheni hiyo ya majini na nchi kavu ya Khaibar ziliwashangaza weledi wa masuala ya kijeshi duniani.  ***

 

Na miaka 21 iliyopita kwa mara ya kwanza "Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama" iliadhimishwa. Uamuzi wa kuitangaza siku hii kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama ulichukuliwa Novemba 1999 na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ambapo mwaka 2008 ulipewa pia jina la 'Mwaka wa Kimataifa wa Lugha". Sisitizo la kulinda na kuimarisha lugha ya mama linatokana na kuwa, takribani nusu ya lugha 6,000 zinazotambuulika duniani zimo katika hatari ya kutokomea kutokana na sababu mbalimbali hususan uingiaji na utwishaji wa lugha za kimataifa kwa kutumia mbinu mbalimbali.***

Siku ya Kimataifa ya Lugha ya Mama