Mar 05, 2021 23:23 UTC
  • Jumamosi, Machi 6, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 22 Rajab 1442 Hijria, mwafaka na tarehe 6 Machi 2021 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 546 iliyopita, alizaliwa Michelangelo, mchoraji na mhunzi wa masanamu wa Italia katika mjini Caprese. Licha ya upinzani mkubwa wa baba yake dhidi ya sanaa hiyo ya uhunzi na uchoraji, Michelangelo alijiendeleza katika taaluma hiyo na kupata umahiri mkubwa. Uhodari wake ulionekana miaka michache baadaye ambapo alifanikiwa kuchonga masanamu mengi ya kuvutia. Michelangelo, alitokea kuwa mhunzi hodari wa karne ya 16 Miladia. Mwaka 1505, wakazi wa mji wa Roma walimwalika Michelangelo, ili aende kuwachongea sanamu la papa kwenye kaburi lake. Baadaye papa wa wakati huo, alimtaka mtaalamu huyo kupamba paa la kanisa la Sistine, kazi iliyoanza hapo mwaka 1508 na kumalizika mwaka 1512. Mbali na hayo, Michelangelo alichonga sanamu kubwa la Nabii Issa (as), ambalo lipo mjini Roma hadi leo.***

Michelangelo

 

Miaka 214 iliyopita, inayosadifiana na 22 Rajab (au rajab 27) 1228 Hijria, alifariki dunia Allamah Sheikh Jaafar Kaashiful Ghitwa, mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu mjini Najaf, Iraq. Allamah Kashiful Ghitwa alikuwa mwanachuoni aliyebobea kwenye taaluma mbalimbali za kielimu kama fiqhi, usulul fiqh, tafsiir ya Qur'ani na Hadith. Mwanachuoni huyo ameandika vitabu vingi vikiwemo, Kashful Ghitwaa na al A'qaaidul Jaafariyya.***

alifariki dunia Allamah Sheikh Jaafar Kaashiful Ghitwa

 

Katika siku kama ya leo Miaka 121 iliyopita, aliaga dunia mvumbuzi wa Kijerumani Gottlieb Daimler akiwa na umri wa miaka 64. Daimler alizaliwa mwaka 1834 na kazi yake ya mwanzo ilikuwa utengenezaji bunduki. Tangu akiwa kijana mvumbuzi huyo alivutiwa sana na kazi za viwandani na alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo hadi alipofanikiwa kutengeneza pikipiki. Gottlieb Daimler pia alikuwa miongoni mwa watu walioweka misingi ya utengenezaji wa magari madogo na hata mabasi. ***

Gottlieb Daimler

 

Siku kama ya leo, miaka 84 iliyopita, alizaliwa, Valentina Tereshkova, mwanamke wa kwanza mwanaanga wa dunia. Akiwa kijana na baada ya kushiriki katika mashindano ya kuruka kwa mwavuli, Tereshkova aliibuka mshindi na hivyo kufikia daraja la ukapteni katika kikosi cha anga cha jeshi la Urusi ya zamani. Ni baada ya hapo ndipo akajifunza urubani wa ndege. Hatimaye tarehe 16 mwezi Juni, mwaka 1963 na akiwa na umri wa miaka 22, aliweka rekodi ya dunia kwa kuwa mwanamke wa kwanza mwanaanga, baada ya kuanza safari ya mwezini na chombo cha Vostok 6. ***

Valentina Tereshkova

 

Miaka 70 iliyopita, aliuawa Ali Razmara, Waziri Mkuu wa Iran aliyekuwa kibaraka wa Uingereza. Razmara aliyekuwa jenerali wa jeshi katika utawala wa kifalme aliuawa na mwanamapinduzi wa Kiislamu aliyejulikana kwa jina la Khalil Tahmasbi. Usaliti na uovu wa wazi wa Ali Razmara katika siasa za kuiongoza nchi, ulizusha upinzani mkubwa wa wananchi dhidi ya Waziri Mkuu huyo na kutayarisha mazingira ya kuangamizwa kwake. ***

Ali Razmara

 

Tarehe 6 Machi miaka 64 iliyopita inayosadifiana na leo, nchi ya Ghana ilifanikiwa kupata uhuru chini ya uongozi wa Dakta Kwame Nkurumah. Ghana ilitumbukia katika makucha ya mkoloni wa Kireno kuanzia karne ya 15. Baada ya Wareno, Waingereza waliidhibiti na kuikoloni nchi hiyo iliyokuwa mashuhuri kwa jina la "Pwani ya Dhahabu" kutokana na utajiri wake mkubwa wa madini hayo. ***

Bendera ya Ghana

 

Na miaka 46 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe 6 Machi 1975, kulitiwa saini mkataba wa kukomesha hitilafu za mpaka baina ya Iran na Iraq. Mkataba huo ulitiwa saini huko Algiers, mji mkuu wa Algeria. Katika fursa ya kufanyika mkutano wa wakuu wa nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi, uliofanyika Algeria,  nchi za Iran na Iraq zilitoa tangazo la pamoja katika siku kama ya leo zikitangaza kuwa, zimefikia makubaliano ya kumaliza hitilafu za mpaka na kwamba, usalama na kuaminiana pande mbili vitashuhudiwa katika mipaka ya pamoja ya nchi hizo. Mkataba huo uliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la Mkataba wa Algeria, haukudumu kwazaidi ya miaka 5; kwani tarehe 21 Septemba 1980, Saddam dikteta wa zamani wa Iraq aliukiuka baada ya kushambulia ardhi ya Iran na kulilazimisha taifa hili kupigana vita vya miaka minane. Hatimaye mwishoni mwa vita hivyo baada ya Iraq kushindwa kwa fedheha, Saddam akautambua rasmi tena mkataba huo. ***

Mkataba wa Algeria