Jumanne, Mei 10, 2016
Leo ni Jumanne tarehe 3 Shaaban 1437 Hijria sawa na Mei 10, 2016.
Katika siku kama ya leo miaka 1433 iliyopita, alizaliwa Imam Hussein (as) mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Kipindi bora zaidi cha maisha ya Imam Hussein ni kile ambacho alikuwa pembeni ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw), kipindi ambacho kilidumu kwa muda wa miaka sita. Imam alilelewa katika familia ambayo ilikuwa chimbuko la ukamilifu na fadhila za irfani na maadili bora. Kuwa na baba kama Imam Ali (as) na mama kama Fatimat az-Zahra (sa) ambao wote wawili walilelewa na Mtume Mtukufu (saw) kulimuwezesha Imam Hussein (as) kupambika kwa matukufu na maarifa ya juu kuhusu Mwenyezi Mungu. Mtukufu huyo alikuwa katika kila uwanja wa mapambano dhidi ya maadui wa Uislamu. Mwaka wa 50 Hijria Imam Hussein (as) alichukua hatamu za kuungoza Umma wa Kiislamu baada ya kuuawa shahidi kaka yake, Imam Hassan (as), jukumu ambalo alilitekeleza kwa busara ya hali ya juu hadi naye mwenyewe alipouawa shahidi kinyama na kidhulma huko katika ardhi ya Karbala nchini Iraq mwaka 61 Hijiria. Kwa tukio hilo aliwafundisha Waislamu na wasiokuwa Waislamu somo muhimu la kutosalimu amri mbele ya watawala dhalimu wasioheshimu dini wala misingi ya utu. Tunawapongeza Waislamu wote duniani na hasa wapenda haki na Watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu (saw), kwa mnasaba huu adhimu wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hussein (as).
Siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 10 Mei 1975 ilianzishwa Harakati ya Polisario kwa shabaha ya kulikomboa eneo la Sahara ya Magharibi. Harakati hiyo ilizidisha harakati zake katika kupambana na mkoloni Mhispania, na hatimaye mkoloni huyo kulazimika kuondoka kwenye eneo hilo mwaka 1975. Lakini kabla ya mkoloni Mhispania kuondoka kwenye eneo la Sahara Magharibi, alilikabidhi kwa serikali za Morocco na Mauritania.
Na tarehe 10 Mei miaka 22 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Mei 1994, Nelson Rolihlahla Mandela aliapishwa kuwa rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini baada ya kupita zaidi ya karne tatu za utawala wa makaburu wachache nchini humo. Chama cha African National Congress (ANC) kilijipatia viti 252 kati ya jumla ya viti 400 vya Bunge la Afrika Kusini, kwenye uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia na wa kihistoria nchini humo. Baada ya kuchaguliwa, Rais Mandela alimteua Thabo Mbeki kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na FW de Klerk kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Afrika Kusini.