Apr 17, 2021 02:40 UTC
  • Jumamosi, 17 Aprili, 2021

Leo ni Jumamosi tarehe 4 ya mwezi mtukufu wa Ramadhani 1442 Hijria ambayo inasadifiana na tarehe 17 Aprili 2021 Miladia.

Katika siku kama ya leo miaka 834 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria aliaga dunia Abul-Qassim, Hibbatullah bin Jaafar, mwanafasihi na mshairi mashuhuri wa Kimisri. Msomi huyo ambaye alijulikana pia kwa lakabu ya Kadhi Said ibn Sanai al-Mulk alizaliwa huko Cairo Misri mwaka 545 Hijria katika familia ya Kiislamu. Alijifunza Qur’ani na elimu ya Nahw katika mji wa Cairo na kusoma elimu ya hadithi na elimu nyingine huko Alexandaria nchini Misri kwa walimu mahiri wa zama hizo. Ibn Sanai al-Mulk alionyesha kipaji na umahiri mkubwa katika uga wa utunzi wa mashairi na fasihi akiwa katika rika la ujana. Miongoni mwa athari zake ni diwani ya mashairi ambayo ina madhumuni mbalimbali ambapo ndani yake mnapatikana pia beti za mashairi zinazoelezea tukio la Ashura na kuuawa shahidi kidhulma Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as). ***

Kadhi Said ibn Sanai al-Mulk

 

Siku kama ya leo miaka 106 iliyopita kwa mara ya kwanza kabisa duniani ilitumiwa gesi ya kubana pumzi ya wanadamu vitani. Hatua hiyo ya kinyama ilichukuliwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia. Ujerumani ilitumia gesi hiyo ya kubana pumzi dhidi ya askari wa Uingereza na Ufaransa na kuua askari wengi wa vikosi vya waitifaki. Wajerumani walipata ushindi katika vita hivyo vilivyokuwa mashuhuri kwa jina la Vita vya Gesi.***

Silaha za kemikali

 

Katika siku kama ya leo miaka 95 iliyopita, raia wa Scotland, John Logie Baird, alifanikiwa kuvumbua televisheni ambayo hii leo imekuwa na umuhimu mkubwa katika upashaji habari duniani. Baird alikuwa mmoja wa wavumbuzi wakubwa wa enzi zake. Baada ya hapo mtu wa kwanza kutengeneza televisheni iliyoimarika zaidi alikuwa ni Giovanni Caselli, raia wa Italia ambaye mnamo mwaka 1862 alifanikiwa kutengeza chombo ambacho kwa kutumia mfumo wa telegrafi kiliweza kutoa ramani na picha. Televisheni ya kwanza ambayo ilionyesha picha kwa ufasaha, ilionyeshwa tarehe 17 mwezi April mwaka 1926 kwa ajili ya klabu ya kifalme nchini Uingereza. ***

 

Miaka 75 iliyopita inayosadifiana na tarehe 17 Aprili 1946, Syria ilipata uhuru kutoka kwa askari wa kigeni waliokuwa wakiitawala nchi hiyo. Syria na baadhi ya ardhi zinazoizunguka awali ilikuwa ikijulikana kwa jina la Sham, na kabla ya kudhihiri dini tukufu ya Kiislamu ilikuwa chini ya udhibiti wa Iran, Ugiriki, Misri na Rome. Ardhi hiyo ilikuwa makao ya utawala wa Ugiriki na baada ya kukaliwa kwa mabavu na Misri, baadaye ilichukuliwa na utawala wa Othmaniya. Baada ya Vita vya Kwanza vya Dunia na baada ya kuporomoka utawala wa Othmaniya, Syria ilikoloniwa na Ufaransa. Kufikia Juni 1941, wakati wa vita vya pili vya dunia, askari wa Uingereza na Ufaransa waliikalia kwa mabavu nchi hiyo, hadi kufikia mwaka 1946 wakati ilipojipatia uhuru wake. ***

Bendera ya Syria

 

Na siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, mwafaka na tarehe 17 Aprili 2004, helikopta za utawala wa Kizayuni wa Israel zilishambulia gari lililokuwa limembeba Dakta Abdulaziz Rantisi, aliyekuwa mwanaharakati wa Palestina na kiongozi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas, na kumuuwa shahidi. Dokta Rantisi alichaguliwa kuiongoza harakati ya Hamas baada ya kuuawa shahidi Sheikh Ahmad Yassin, mwasisi na kiongozi wa harakati hiyo. Rantisi alizaliwa mwaka 1947 katika mji wa Yafa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu na alihitimu elimu ya tiba kama daktari katika Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri.