Feb 18, 2022 02:30 UTC
  • Ijumaa, Februari 18, 2022

Leo ni Ijumaa tarehe 16 Rajab 1443 Hijria sawa na tarehe 18 Februari 2022 Milaadia.

Miaka 458 iliyopita katika siku inayofanana ya hii ya leo, Michelangelo di Lodovico Buonarroti mchoraji, mchongaji wa sanamu, msanifu majengo na malenga mkubwa wa Kiitalia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 89. Michelangelo alizaliwa mwaka 1475 na kuanza kujishughulisha na uchoraji na kuchonga sanamu licha ya upinzani wa baba yake. Malenga huyo wa Kiitalia alionyesha kipaji chake haraka katika uwanja wa uchoraji, uchongaji sanamu na usanifu majengo. Uchongaji wa sanamu za Manabii Isa na Musa huko Italia ni moja kati ya kazi kubwa za kisanaa zilizofanywa na Michelangelo katika zama zake hizo.

Michelangelo di Lodovico Buonarroti

Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita, ukoloni wa Ufaransa ambao ulianza mwaka 1830 dhidi ya Algeria, ulishindwa vibaya na wapiganaji wa Amir Abdelkader al-Djezairi, kiasi kwamba theluthi moja ya askari wa Ufaransa waliuawa na nusu nyingine ya waliobakia hai walikamatwa mateka. Wakati huo Wafaransa ambao ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kupata hasara kubwa ya namna hiyo barani Afrika, ili kukusanya nguvu waliamua kuomba suluhu. Hata hivyo Amir Abdelkader al-Djezairi alikataa ombi hilo, hadi baada ya kupita karibu miaka miwili na kuikomboa ardhi yote ya Algeria kutoka mikononi mwa Wafaransa hao wavamizi. Hata hivyo miaka kadhaa baadaye Ufaransa iliweza kuidhibiti tena nchi hiyo, baada ya kuongeza askari na zana za kijeshi sambamba na kuwatumia baadhi ya viongozi wahaini wa makabila ndani ya Algeria.

Amir Abdelkader al-Djezairi

Siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, askari wa Ufaransa na Uhispania, walivunja mapambano ya wapiganaji wa Morocco chini ya uongozi wa Abdel-Karim Rifi na shujaa huyo wa Muislamu akapelekwa uhamishoni kusini mwa Afrika. Abdel-Karim Rifi alianzisha mapambano yake sambamba na kuanza uvamizi wa Uhispania katika sehemu ya ardhi ya Morocco hapo mwaka 1912 Miladia. Hata hivyo na licha ya mkoloni huyo kuwa na nguvu kubwa na kutekeleza mauaji ya umati dhidi ya raia wa Morocco wasio na hatia, mwaka 1921 wapiganaji wa Abdel-Karim Rifi walipata ushindi mkubwa kiasi cha kuyafanya baadhi ya maeneo ya nchi hiyo kutangaza Jamhuri. Katika hali hiyo Wafaransa nao ambao walikuwa wakiyadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi hiyo walipatwa na hofu kufuatia ushindi wa wananchi dhidi ya Wahispania na kwa ajili hiyo mwanzoni mwa mwaka 1924 wakaanzisha hujuma kubwa dhidi ya wanamapambano hao. Jeshi la Ufaransa chini ya Jemadari Philippe Pétain hata kama mwanzoni lilishindwa vibaya na wanamuqawama wa Morocco, lakini mwezi Februari 1926 katika siku kama ya leo liliwashinda wapiganaji wa Abdel-Karim Rifi  baada ya kupata msaada wa kijeshi na kutekeleza jinai kubwa dhidi ya wananchi. Kwa utaratibu huo Ufaransa ikaweza kuendeleza ukoloni wake nchini Morocco.

Abdel-Karim Rifi

Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita yaani mnamo tarehe 18 mwezi Februari mwaka 1965, Gambia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Uingereza ilianza kuikoloni Gambia mwaka 1588 na kupora maliasi za nchi hiyo kwa karibu karne nne. Mwaka 1963, Uingereza iliipatia Gambia mamlaka ya ndani baada ya kudhoofika kisiasa na kiuchumi kutokana na Vita vya Pili vya Dunia na kushindwa kuendesha makoloni yake. Hatimaye ilipofika mwaka 1965 Gambia ilipatia uhuru wake.

Bendera ya Gambia

Miaka 55 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mwanafizikia na mtengenezaji wa bomu la atomiki wa Marekani Robert Oppenheimer. Kabla ya Vita vya Pili vya Dunia mtaalamu huyo alifanya utafiti kuhusiana na jinsi ya kupasua atomu na kupata nishati ya nyuklia. Wakati wa vita hivyo alipewa wadhifa wa kusimamia kitengo cha utafiti katika Wizara ya Vita ya Marekani na chini ya usimamizi wake yakatengenezwa mabomu matatu ya kwanza ya nyuklia. Hata hivyo, wakati Marekani ilipoishambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia mwaka 1945, makumi ya maelfu ya watu wasio na hatia waliuawa katika kipindi kifupi, hali iliyomfanya Oppenheimer kujutia kitendo chake hicho na akatoa wito wa kutumiwa nishati ya atomiki katika masuala ya amani.

Robert Oppenheimer

Miaka 44 iliyopita katika siku kama hii ya leo, wananchi Waislamu wa Tabriz huko kaskazini magharibi mwa Iran walikutana katika msikiti mmoja mkubwa katika mji huo kwa lengo la kuwakumbuka wananchi waliouawa shahidi tarehe 19 mwezi Dei mwaka 1356 Hijria Shamsiya huko Qum kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani. Wenyeji wa Tabriz walikutana hapo kufuatia wito uliotolewa na maulamaa na wanazuoni wa kidini. Mkutano huo ulibadilika na kuwa uasi wa kijamii kutokana na ukandamizaji mkubwa uliofanywa na askari wa utawala wa kidhalimu wa Shah. Harakati hiyo ya kimapinduzi iliutia kiwewe utawala wa Shah ambao ulitumia urongo kuhadaa wananchi kwa kudai kuwa, waliohusika na harakati hiyo walitoka nje ya Iran.

Maandamano ya watu wa Tabriz

Na siku kama ya leo miaka 23 iliyopita Ayatullah Sayyid Muhammad Swadiq al-Sadr mmoja wa maulamaa mashuhuri wa Iraq aliuawa kigaidi katika mji mtakatifu wa Najaf nchini humo. Wananchi Waislamu wa Iraq walifanya maandamano kadhaa kufuatia kuuawa kwa msomi huyo mkubwa na kuutaja utawala wa zamani wa Baath huko Iraq kuwa ndio uliomuuwa shahidi Ayatullah Sadr. Utawala wa zamani wa Baahi nchini Iraq ulifanya mauaji mengi dhidi ya maulamaa na wanazuoni wa Kiislamu katika siasa zake za kuidhoofisha Hauza na chuo kikuu cha kidini katika mji mtakatifu wa Najaf tangu uliposhika hatamu za uongozi nchini humo mwaka 1968 hadi ulipoondolewa madarakani.

Ayatullah Sayyid Muhammad Swadiq al-Sadr