Jumanne tarehe Pili Agosti mwaka 2022
Leo ni Jumanne tarehe 4 Mfunguo Nne Muharram 1444 Hijria sawa na tarehe Pili Agosti 2022.
Siku kama ya leo, miaka 1383 iliyopita, Ubaidullah bin Ziyad, mtawala dhalimu na fasiki wa mji wa Kufa, Iraq alitoa hotuba katika msikiti wa mji huo. Katika hotuba hiyo, Ibn Ziyad alitoa vitisho vikali dhidi ya wafuasi wa Imam Hussein (as), mjukuu wa Mtume Muhammad (saw) akiwataka wasimsaidie mtukufu huyo katika ardhi ya Karbala na kwamba atamuua mtu yeyote ambaye ataasi amri hiyo. Kwa kutumia fatwa ya hila iliyotolewa na Shuraihul-Qadhi ya kuhalalisha damu ya Imam Hussein (as), Ibn Ziyad alifunga njia zote za kuingia na kutoka mji wa Kufa na akawahonga kwa fedha wakazi wa mji huo kwa ajili ya kwenda kupambana na mjukuu huyo wa Mtume huko Karbala; tukio lililomalizika kwa kuuawa Imam Hussein na watu wa familia ya Mtume (saw).

Siku kama ya leo miaka 959 iliyopita, alifariki dunia Abul-Qasim Muhammad Baghdadi, maarufu kwa jina la Ibn Naqiya, malenga, mwandishi na fasihi mkubwa wa mjini Baghdad, Iraq. Umahiri aliokuwa nao Ibn Naqiya, ndio uliofanya kuwa mashuhuri ambapo hata wataalamu wa mashairi waliyatumia mashairi yake. Kitabu cha ‘Maqaamaat’ ni moja ya athari zinazonasibishwa kwa malenga huyo. Katika kitabu hicho Ibn Naqiya, alizungumzia maovu ya kijamii kupitia hekaya na tenzi. Athari nyingine inayonasibishwa kwa msomi huyo wa Kiislamu, ni kitabu kinachoitwa ‘Al-Jamaan fi Tashbiihaatil-Qur’an’ ambayo ni tafsiri nyepesi ya Qur’an Tukufu. Katika tafsiri hiyo Ibn Naqiya amefafanua Aya 226 za Qur'ani Tukufu.

Siku kama ya leo miaka 113 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 11 Mordad 1288 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi mjini Tehran Ayatullah Sheikh Fadhlullah Nouri mwanachuoni mkubwa ambaye alikuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na utawala wa kidikteta wa Qaajar hapa nchini Iran. Ayatullah Fadhlullah Nouri alikuwa mstari wa mbele katika kupigania mapinduzi ya katiba na alisimama kidete kupinga sheria zilizopitishwa bungeni ambazo zilikuwa zikikinzana na miongozo na mafundisho ya Uislamu.

Siku kama ya leo miaka 88 iliyopita inayosadifiana na tarehe Pili Agosti 1934, alifariki dunia Field Marsha Paul von Hindenburg, rais wa zamani wa Ujerumani na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya majeshi ya nchi hiyo wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Hindenburg alichaguliwa kuwa Rais wa Kwanza wa Ujerumani mwaka 1925.

Tarehe Pili Agosti miaka 77 iliyopita, kongamano la Potsdam lilikamilisha kazi zake. Kongamano hilo la tatu na la mwisho la viongozi waitifaki walioshiriki katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, lilianza tarehe 17 mwezi Julai na kumalizika tarehe Pili Agosti 1945. Kongamano hilo lililofanyika katika mji wa Potsdam karibu na mji mkuu wa Ujerumani, Berlin lilihudhuriwa na Joseph Stalin, Harry S. Truman na Winston Churchill, marais wa wakati huo wa Urusi ya zamani, Marekani na Uingereza.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulitumwa katika nchi za Iran na Iraq na ukatoa ripoti mbili ambazo zilieleza kuwa, utawala wa zamani wa Iraq ulitumia mara kadhaa silaha za kemikali dhidi ya majeshi na raia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Umoja wa Mataifa kukiri waziwazi kwamba, jeshi la Iraq lilitumia silaha za kemikali dhidi ya Iran. Pamoja na hayo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halikutoa azimio lolote dhidi ya utawala wa dikteta Saddam Hussein wa Iraq ambao ulikuwa ukiungwa mkono na nchi za Magharibi, kwa kutumia silaha za kemikali. Masaa kadhaa baada ya kutolewa ripoti hizo, ndege za kivita za Iraq ziliushambulia tena mji wa Ushnawiye kwa mabomu ya kemikali na kujeruhi watu 2400.

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, jeshi la Iraq liliishambulia na kuikalia nchi jirani ya Kuwait. Huo ulikuwa uvamizi wa pili wa Iraq kwa jirani zake baada ya ule wa Iran wa mwaka 1980. Utawala wa Saddam ulikuwa ukidai kwamba, ardhi ya Kuwait ni sehemu ya ardhi yake. Mashambulio ya Iraq dhidi ya Kuwait yalikabiliwa na radiamali kali ulimwenguni. Nchi nyingi duniani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilaani uvamizi huo na kuvitaka vikosi vya Iraq kuondoka mara moja katika ardhi ya nchi hiyo. Nchi kadhaa zikiongozwa na Marekani zilituma vikosi vyao vya kijeshi katika Ghuba ya Uajemi ili kuviondoa vikosi vamizi vya Iraq kutoka katika ardhi ya Kuwait na kuhitimisha uvamizi huo Februari 28 mwaka 1991.
