Aug 04, 2022 06:33 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Bismillahir Rahmanir Rahiim. Salamu njema na bora zaidi zimuendee Mtume wetu Mtukufu Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu (as). Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni wasaa mwingine wa kujiunga nanyi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi.

 

Bismillahir Rahmanir Rahiim. Salamu njema na bora zaidi zimuendee Mtume wetu Mtukufu Muhammad (saw) na Aali zake watoharifu (as). Assalaam Alaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni wasaa mwingine wa kujiunga nanyi katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi.

********

Hitoria ya sira na maisha ya Mtume Mtukufu (saw) imetunukulia na kutupasha habari kuhusu sifa njema na fadhila za Maimamu wawili ambao ni wajukuu wake Mtume, al- Imamain Hassan na Hussein (as), kwamba watukufu hao waliteuliwa na kuzingatiwa kwa njia maalumu na Mwenyezi Mungu tangu wangali wadogo. Aliwapa karama na miujiza mingi ambayo inamfanya muumini apate imani na yakini thabiti kwamba watukufu hao waliteuliwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Miongoni mwa karama hizo ni ile ambayo imepokelewa na Ibn Abbas kama inavyonukuliwa na Shahab ad-Deen al-Hamadani katika kitabu chake cha Mawaddat al-Qurba na Khawarazmi al-Hanafi katika kitabu cha Maqtan al-Hussein (as) kwamba siku moja Imam Hassan na Hussein walikuwa wakijishughulisha kuandika mstari (mchoro/ mwandiko) na kila mmoja akamwambia mwenzake kuwa ndiye aliyekuwa na mstari (mchoro/mwandiko) mzuri zaidi. Hatimaye waliamua kumwendea mama yao Bibi Fatwimah (as) ili apate kuamua ni nani kati yao alikuwa amechora mstari mzuri zaidi. Lakini mama yao huyo kwa kuhofia kumkasirisha mmoja wao kwa uamuzi wake aliamua suala hilo lipelekwe kwa baba yao Ali Amir al-Mu'mineen (as). Amir Mu'mineen naye alikataa kutoa uamuzi kuhusu kadhia hiyo na kupendekeza uamuzi wa mwisho utolewe na Mtume Mtukufu (saw). Mtume pia alikataa kuamua na kulirejesha suala hilo kwa Malaika Jibril (as). Jibril naye alikataa kutoa uamuzi na kusema uamuzi utolewe na Malaika Israfil ambaye naye alikataa kutoa uamuazi na kusema utolewe na Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Mwenyezi Mungu alimwambia Jibril amuombe Bibi Fatwimah (as) atoe uamuazi wa mwisho kuhusu kadhia hiyo kati ya watoto wake wawili wapendwa. Mama huyo mwenye huruma na muamuzi mwadilifu aliwaambia wanaye: 'Enyi wanangu wapendwa! Nitamwaga chini mbele yenu shanga za mkufu huu. Atakayekusanya shanga nyingi zaidi ndiye atakayekuwa na mstari (mchoro) mzuri zaidi. Bila kupoteza wakati alifungua mkufu kutoka shingoni kwake na kumwaga chini shanga zake mbele ya wanawe wapendwa. Jibril ambaye alikuwa ametumwa na Mwenyezi Mungu wakati huo wote alikuwa amesimama pembeni akitazama mandhari hiyo ya kuvutia. Kwa kuwa watoto wawili hao walikusanya idadi sawa ya shanga hizo, kwa amri ya Mwenyezi Mungu Jibril (as) alikchukua ushanga mmoja uliokuwa umesasilia chini na kuukata katika vipande viwili vilivyo sawa, na kisha kumpa kila mmoja kipande cha ushanga huo. Hivyo hakuna yeyote kati ya wawili hao aliyeudhika wala kuvunjika moyo kuhusiana na suala hilo.'

Salman al-Farsi anasema kwamba alienda kwa Mtume Mtukufu (saw) na kumsalimu. Bibi Fatwimah (as) alikuwa amemuomba ampelekee wanawe wawili, al-Hassan na Hussein (as) kwa Mtume (saw) huku wakiwa wanahisi njaa. Walipofika kwake aliwauliza Mtume: 'Kuna tatizo gani wapendwa wangu? Walimwambia: Tuna njaa ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu.' Hapo Mtume aliwaombea dua kwa Mwenyezi Mungu kwa kusema mara tatu: 'Allahumma wape chakula!' Salman anasema kwamba ghafla aliona chakula cheupe na kitukufu kupindukia kikiwa mikononi mwa Mtume (saw), chakula ambacho kilikuwa cheupe kuliko theluji, kitamu kuliko asali na chororo kuliko siagi. Mtume (as) alikigawa katika sehemu mbili ambapo alimpa kimoja Imam Hassan na kingine Imam Hussein (as). Alimwambia Salman ambaye alikuwa akitazama na kukitamani sana chakula hicho kwamba kilikuwa kimetoka peponi na kwamba hakingeliwa na mtu yoyote isipokuwa yule ambaye alikuwa amenusurika kuhesabiwa na Mwenyezi Mungu kutokana na matendo yake. Pamoja na hayo alimwambia Salman kwamba alikuwa Salama Inshallah.'

Hadithi hii pia imenukuliwa na al-Khawarazmi katika kitabu cha Maqtal al-Hussein na inayofanana nayo na Sheikh Abdurahman as-Swafuri as-Shafi katika kitabu cha Nuzhat al-Majalis.

Tunaendelea kusalia na Mtume Mtukufu (saw) wasikilizaji wapenzi ambapo imenukuliwa katika Hadithi nyingi kwamba mtukufu huyo aliwapenda sana wajukuu wake wawili Hassan na Hussein (as) kiasi kwamba alikuwa akitumia muda mrefu kuwachunga na kuwa karibu nao kutokana na utukufu waliokuwa nao mbele ya Mwenyezi Mungu. Khawarazmi ambaye ni wa madhehebu ya Hanafi anasema katika Hadithi ndefu ambayo inaishia kwa Bibi Aisha ambaye alikuwa mmoja wa wake za Mtukufu Mtume (saw) akisema kwamba siku moja alikuwa nyumbani kwake na ghafla akawa ameomba nguo zake ili apate kwenda kuwaona wajukuu zake hao kwa binti yake Bibi Fatwimah (as). Alipofika huko aliambiwa kuwa walikuwa wametoka naye Mtume akatoka kuwafuata. Alipokuwa njiani alikutana na Abu Darda' ambaye alimuuliza iwapo alikuwa amewaona wakujuu wake hao. Abu Darda' alimwambia kuwa alikuwa amewaona wakiwa wamelala chini ya kivuli cha ukuta wa Bani Judh'an kutokana na makali ya njaa. Mtume (as) alielekea huko na kuwakumbatia kwa upendo mkubwa huku wakiwa wanalia. Mtume alifuta machozi yao na hapo Abu Darda' akawa amemwomba Mtume apewe fursa ya kuwabeba. Mtume alimwambia amwache awafute machozi na kuapa kwa jina la Mwenyezi Mungu kuwa hata kama tone moja tu la machozi yao lingendondoka ardhini basi baa la njaa lingebakia kwenye umma wake hadi Siku ya Kiama. Kisha akawa amewabeba huku wanalia naye analia pia. Hapo Malaika Jibril akawa ameteremka na kumpa salamu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Alimuuliza ni kwa nini alikuwa na huzuni na kulia. Akamjibu kuwa hakuwa analia kutokana na hofu wala woga bali alikuwa analia kutokana na udhalilishaji wa dunia. Alimwambia aombe kupitia kitu kilichokuwa kimeanguka pembeni ya ukuta huo na hapo akawa ameteremshiwa chakula ambacho aliombwa akule yeye pamoja na wajukuu wake wawili hao na vilevile Watu wa Nyumba yake.

Inasemekana kwenye Hadithi nyingine kwamba Mtume (saw) alipokuwa akihisi njaa alikuwa akitoka kwenda kuwatazama Hassan na Hussein (as) na hapo njaa ilimwondokea.

Imethibiti katika vitabu vingi vya historia na wataalamu wa Hadithi kwamba aliwapenda sana wajukuu wake wawili, al-Hassan na al-Hussein kiasi kwamba mara nyingine alikuwa akirefusha sijda kwenye swala hadi wajukuu hao walipoteremka kutoka kwenye mgongo wake. Alikuwa akichukia kuwateremsha hadi wenyewe walipoamua kuteremka na alipoamua kuwateremsha basi alifanya hivyo kwa uangalifu mkubwa ili kulinda mapenzi na upendo mkubwa uliokuwa baina yake na wajukuu hao. Jambo hilo limezungumziwa kwa urefu na Ahmad bin Hambal katika kitabu cha Musnad, Ibn Athir katika al-Mukhtar na vile vile katika Usud al-Ghaba Ibn Qayyim al-Jauziyya katika Ighathat al-Lahfan Ad-Dhabi as-Shafi' katika Siyar A'laam an-Nubalaa na Haithami as-Shafi katika Majmau az-Zawahid.

Hadithi inayohusiana na suala hilo pia imenukuliwa na al-Hakim an-Nisaburi as-Shafi katika kitabu cha Mustadrak ala Swahihain akimnukuu Abu Huraira, Ibn Asakir ad-Dimashqi as-Shafi' katika Tarikh ad-Dimashq, al-Muhib at-Tabari katika Dhakhair al-Uqba Ibn Hajar as-Asqalani katika Tahdhib at-Tahdhib Ibn Kathir katika al-Bidaya wa an-Nihaya na wasomi wengine wengi.

Je, suala hili lina maana gani?

Hakuna shaka yoyote wapenzi wasikilizaji kwamba kama ambavyo maneno na vitando vya Mtume Mtukufu (saw) ni maasumu hisia zake pia ni hivyo hivyo. Yaani hisia hizo hubainishwa na kuwekwa wazi kutokana na radhi za Mwenyezi Mungu. Hizo ni sifa walizotengewa wajukuu wawili hao wa Mtume (saw) na Mwenyezi Mungu Mtukufu na bila shaka zinaashiria kufadhilishwa kwao na kupewa cheo cha Uimamu na Mwenyezi Mungu. Jambo hilo lilibainishwa wazi na Mtume Mtukufu (saw) kabla ya kifo chake aliposema: 'Ama Hassan ana hadhi na heshima yangu, na Hussein ana ujasiri na huruma yangu.'
Hadithi zinazozungumzia suala hili zimenukuliwa kwa mapana na marefu na wanazuoni wengi wa Kiislamu katika madhehebu zote mbili za Shia na Suni katika vitabu vyao na hilo linaashiria wazi heshima, hadhi na utukufu walionao wajukuu wawili hawa wapendwa wa Mtume (saw) katika Uislamu.
Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji hatuna budi kukuageni tukitumai kwamba tumenufaika sote na kipindi hiki kilichokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena juma lijalo, tunakuageni nyote tukisema, kwaherini.