Aug 04, 2022 06:39 UTC
  • Sibtain katika Qur'ani na Hadithi

Assalaama Alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kama mnavyojua huzungumzia sifa na fadhila za wajukuu wawili wa Mtume wetu Mtukufu Muhammad al-Mustafa (saw) ambao si wengine bali ni Imam Hassan na Hussein (as).

Ndugu wasikilizaji, ni wazi kuwa isma au kinga ya mtu kutofanya dhambi ni miongoni mwa sifa na mambo ya dharura anayopasa kuwa nayo mtume la sivyo watu hawatakuwa na imani naye wala kufuata mafundisho yake. Miongoni mwa umuhimu wa isma ni kumzuia mtu aliye na kipawa au sifa hiyo kutofanya au kujuzisha mambo kinyume cha sheria, ukweli wa mambo au kukiuka haki za watu wengine.

Hivyo basi mambo yote aliyoyafanya Mtume Mtukufu (saw) na kuyazungumzia kuhusu Ahlu Bayt wake na fadhila zao, yote hayo yaliambatana kikamilifu na ukweli ambao alifahamishwa na Mwenyezi Mungu na kumuamuru awafahamishe watu ili wapate kuyafuata bila ya kuhitilafiana kwayo. Mtume (saw) alisema na kubainisha wazi kwamba sifa za Manabii na Mitume ziliwekwa na kudhihiri katika makhalifa na warithi wake wa haki ambao ni Imam Ali, Hassan na Hussein pamoja na Maimamu wengine tisa waliotokana na kizazi cha Imam Hussein (as). Mtume Mtukufu alizunguimzia kwa marefu na mapana sifa na fadhila nyingi walizokuwanazo wajukuu wake al-Hassan na al-Hussein na kubainisha wazi sifa za mbinguni na za kipekee walizokuwa nazo watukufu hao. Miongoni mwa sifa hizo ni sifa za Uimamu ambao waliainishiwa moja kwa moja na Mwenyezi Mungu. Maimamu hao waliteuliwa na kuchaguliwa na mwenyezi Mungu kwa kutaja majina yao kupitia Mtume Mtukufu (saw). Si wawili hao tu bali majina yote ya Maimamu kumi na wawili yalitajwa na kuwekwa wazi na Mtume (saw). Je, ni sifa na viwango gani hivi vilivyoanishwa na Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake kwa ajili ya Maimamu ambao wangekuja na kuuongoza Umma wa Kiislamu baada yake? Na je, sifa hizo zilidhihirishiwa watu gani? Tutapata kujua jibu la maswali haya hivi punde.

***********

Ndugu wasikilizaji, maumbile ya mwanadamu humfanya ahitajie nuru na mwangaza wa elimu ambao utamuongoza katika maisha yake ya dunia na kwenye njia ya haki kuelekea maisha ya baadaye huko Akhera. Nuru hiyo inapasa kumuongoza kwenye haki na heri ili asipate kupotea katika ulimwengu huu uliojaa vishawishi vya Shetani na upotovu. Ni wazi kuwa katika hali hiyo mwanadamu huhitajia kiongozi na Imamu asiyefanya makossa wala dhambi na ambaye ameteuliwa na Mweyezi Mungu ili apate kuwaongoza waja wake katika njia nyoofu inayowawezesha wafanye mambo mema na ya heri yanayomridhisha Mungu Muumba.

Mbali na kutekeleza majukumu yake ya ulinganiaji na kubainisha sheria za Mwenyezi Mungu kwa waja wake, Mtume Mtukufu (saw) alituletea bishara nyingi njema, kubwa zaidi ikiwa ni ya kuongozwa na Maimamu watoharifu na watukufu baada yake na ambao waliteuliwa na kutangazwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe. Baada ya kutaja sifa na fadhila zao, Mtume aliwahakikishia Waislamu kwamba hawangepotea njia ya wokovu na saada ya humu duniani na huko Akhera kama wangefuata kwa dhati mafundisho, maamrisho na makatazo ya Maimamu hao watoharifu. Aliwasisitizia wafuate na kushikamana na Maaimamu hao wa nyumba yake, wakiwemo wajukuu wake wawili watukufu Hassan na Hussein (as).

Khawarazmi al-Hanafi mwanazuoni mashuhuri wa Kisuni anasema katika kitabu chake cha Maqtal Hussein (as) akimnukuu sahaba mashuhuri Ibn Abbas kwamba alisema: 'Mtume Mtukufu (saw) alisema: 'Mimi ni mizani ya elimu, Ali ni sahani zake mbili (za mizani), Hassan na Hussein kamba zake, Fatwimah kiunganishi na Maimamu waliosalia wa Umma wangu ni mhimili (nguzo) yake, ambapo zitapimwa ndani yake amali za wanaotupenda na wanaotuchukia.'

Wapenzi wasikilizaji mambo aliyoyasema Mtume Mtukufu wa Uislamu (saw) katika kuwasifu Ahlul Bait wake kwa hakika ni jambo linalompelekea kila Mwislamu mwenye insafu ajivunie watukufu hawa na kuwa na fahari kuwa ndio viongozi wake wanaomuongoza katika maisha ya humu duniani kwa ajili ya kumfikisha kwenye saada na mafanikio ya milele huko Akhera. Viongozi hawa watoharifu na maasumu ni maulama wenye hekima, waja wa Mwenyezi Mungu wenye takwa, Maimamu waliotakaswa wakatakasika na ambao waliteuliwa kwa haki na Mwenyezi Mungu miongoni mwa wanadamu kwa ajili ya kuwaongoza waja wake na kuwaelekeza kwenye njia nyoofu. Hii ni kinyume kabisa na watu wanaojitwalia uongozi kwa nguvu au kwa mbinu nyingine za hila na ujanja na kwa ajili ya kujilimbikizia mali za humu duniani na kukidhi matamanio yao ya kibinafsi na mwishowe kuwapotosha wanadamu kwa kuwatumbukiza kwenye madhambi na mambo yaliyoharamishwa na Mwenyezi Mungu.

Khatib al-Baghdadi anaandika katika kitabu chake mashuhuri cha Tarikh al-Baghdad kupitia hadithi iliyonukuliwa na Ibn Abbas kwamba Mtume (saw) alisema: 'Usiku ule niliopaishwa mbinguni niliona kwenye mlango wa Peponi pakiwa pameandikwa: La Ilaha Ila Allah Muhammad Rasulu Allah, Ali ni kipenzi cha Mwenyezi Mungu, Hassan na Hussein ni wateule wake na Fatwimah ni kheri yake. Laana ya Mwenyezi Mungu iwateremkie wale wanaowachukia.'

Khawarazmi ameandika Haidithi inayofanana na hii lakini inayomalizikia kwa Imam Ali (as) katika kitabu chake cha Maqtal al-Hussein (as) inayosema kwamba Mtume Mtukufu (saw) alisema: 'Nilipopaishwa mbinguni niliona kwenye mlango wa Peponi pakiwa pameandikwa: La Ilaha Ila Allah, Muhammad ni kipenzi cha Mwenyezi Mungu, Ali ni Walii wake (Mwenyezi Mungu), Fatwimah ni mtumishi wake na Hassan na Hussein ni wateule wake. Laana ya Mwenuezi Mungu iwateremkie wanaowachukia.'

Ndugu wasikilizaji, hii ni bishara na uongozi kwa wakati mmoja. Hili ni Jambo ambalo linawafanya Waislamu kuwa na imani na utulivu wa moyo kuhusiana na mafundisho na ushauri unaotolewa kwao na Mtume Mtukufu (saw) na hasa hasa kuhusiana na Ahlu Bait wake (as). Hawa ndio viongozi ambao Mtume Mtukufu mwenyewe na kwa mwongozo na amri ya Mwenyezi Mungu aliwasifu kuwa viongozi wanoongoza kwenye njia nyoofu inayoelekeza kwenye nuru na mafanikio ya humu duniani na huko Akhera na kwamba anayewafuata kwenye mafundisho ya dini huwa amesibu na kufuata njia ya haki na kuepuka upotovu. Hao ndio viongozi na Maimamu ambao wametukuzwa, kusafishwa na kusifiwa na maandiko matakatifu kuwa ni viongozi wema na maasumu ambao hawaneni ila haki na kwamba haki iko pamoja nao, ndani yao, inaelekeza kwao na kuwa wao ndio warithi halisi wa mafundisho ya Mtume Mtukufu (saw). Mafundisho ya mbinguni na Hadithi za Mtume zinasema wazi kwamba anayewafuata huwa amefuata njia ya haki na anayetengana nao huwa amepotea njia na kuchagua batili. Anayewapenda huwa amempenda Mwenyezi Mungu na anayewachukia huwa amemchukia Mwenyezi Mungu. Kwa msingi huo anayewafuata na kushikamana nao huwa ameshikamana na Kamba ya Mwenyezi Mungu inayoongoza kwenye nuru na heri na kuelekeza kwenye Pepo ya milele na anayewachukia na kuwafanyia uadui huwa ameangamia ambapo moto mkali wa Jahannam ndiyo yatakayokuwa makazi yake ya milele.

Nam wapenzi wasikilizaji, ni kupitia watukufu hawa wa Ahl Bait wa Mtume (saw) ndipo waja watapata mafanikio ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu na wale wanaokiuka na kuwapinga kupata adhabu ya milele. Al-Khawarazmi anasema katika Hadithi iliyopokelewa kupitia Ibn Abbas kwamba Mtume (saw) alisema kwa maneno yaliyo wazi kuwa: 'Mlionywa kupitia kwangu na kisha mkaongoka kupitia Ali.' Kisha Mtume akasoma Aya ifuatayo: Hakika wewe ni Mwonyaji, na kila kaumu ina wa kuwaongoa.

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa timenufaika kwa pamoja na yale yote tuliyoyasikia katika kipindi che leo. Basi hadi juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aalykum Warahmatullahi Wabarakatuh.