Aug 04, 2022 07:18 UTC
  • Sibtain Katika Qur'ani na Hadithi

Assalaam Aalaykum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambacho huzungumzia fadhila na sifa za wajukuu wawili wa Mtume Mtukufu (saw) ambao si wengine bali na Maimamu al-Hassan na al-Hussein (as) ambao aliwapenda sana Mtume na kuwausia Waislamu pia wawapende wa kuwalinda dhidi ya madhara na mabaya yote. Karibuni.

Ndugu wasikiliza, maisha ya Mtukufu Mtume (saw) yalijaa mafunzo, hekima yenye manufaa na wakati huo huo kuwa hoja ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake humu duniani. Hii ni kutokana na ukweli kwamba maisha ya mtukufu huyo ni ishara inayoongoza kwenye haki na kutahadharisha dhidi ya batili.

Maisha ya Mtume (saw) yalithibitisha na kuutenganisha ukweli na batili kiasi kwamba kila mtu aliyeangamia baada ya hapo alifanya hivyo kutokana na kiburi na ukaidi wake mwenyewe na sio kwamba hakuwa anajua ukweli uko wapi. Aliyeongoka na kufuata njia sahihi kutokana na matendo yake bila shaka alifanya hivyo kutokana na chaguo lake mwenyewe baada ya kubainishiwa ukweli na Mtume Mtukufu (saw) na Watu wa Nyumba yake Tukufu (as). Miongoni mwa mambo aliyoyabainisha wazi na katika matukio na sehemu kadhaa ni kuhusiana na suala zima la Uimamu na Maimamu watoharifu ambao waliainishwa kuchukua nafasi ya Mtume (saw) baada ta Mtukufu huyo kuondoka duniani. Mtume alitabiri uonevu na mateso ambayo wangeyapitia watukufu hao kutokana na kusalitiwa na Waislamu na watawala waovu wa wakati huo na kuwataka watu wawanusuru na kuwatetea kutokana na dhulma ambayo wangeelekezewa na watawala pamoja na maadui wao ambao hawakujali mafundisho ya dini wala maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake mtukufu (saw).

Lakini je, Umma uliyasikia mawaidha na nasasa hizo za Mtukufu Mtume (saw), au ulizipuuza na kisha kuamua kuwadhulumu Watu wa Nyumba yake tukufu, haki na vyeo vyao ambavyzo waliainishiwa na Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake asiyetamka kutokana na matamanio bali huwa ni Wahyi wa mbinguni? Si hilo tu bali waovu katika umma huo waliamua kwenda mbali zaidi na kuchukua hatua ya kuwatesa na hatimaye kuwaua kikatili. Mtume Mtukufu alibashiri na kutahadharisha juu ya jambo hilo kwa kusema: "Hakuna Nabii wala Wasii ambaye hakuuawa shihidi."

Ama kuhusu Maimamu wawili al-Hassan na al-Hussein (as) kuna hadithi na riwaya nyingi ambazo zinaashiria kuuawa kwao shahidi miongoni mwazo ikiwa ni ile Hadithi iliyopokelewa na kunukuliwa na Sayyid bin Twawous katika kitabu chake cha al-Iqbal ala Allahi Bil A'maal mbapo baada ya kunukuu hadithi hiyo ndefu kuhusiana na tukio la Mubahala aliokuwa nao Mtume na Wakristo wa Najran, inasemekana kwamba katika baadhi ya maneno aliyoyasema Nabii Isah (as) kuhusu Mtume (saw) ni kuwa: " Kizazi chake kitatokana na Swadiqah Mbarikiwa (Khadija as) ambaye atamzalia binti ambaye naye atazaa watoto wawili ambao watakuwa mabwana na ambao watauawa shahidi. Nam, kizazi cha Ahmad kitatokana na wawili hao."

Naye Sheikh Majlisi ananukuu katika kitabu chake cha Bihar Anwar Hadithi kutoka kwa Imam Ali Amir al-Mu'mineen (as) kwamba alisema: "Siku moja tulikuwa mbele ya Mtume naye akawa ametutazama na kuanza kulia: Nikamuuliza ni kitu gani kunachokuliza ewe Mtume wa Mwewnyezi Mungu? Akajibu: Ninalia kutokana na kile watakachokufanyieni baada yangu. Nikauliza: Ni kitu gani hicho ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: Ninalia kutokana na upanga utakaopigwa wewe kichwani, kofi atakayopigwa Fatwimah kwenye shavu, jeraha atakalopata Hassan kwenye paja pamoja na kunyeshwa sumu na mauaji atakayofanyiwa Hussein. Katika hali hiyo watu wote waliokuwa nyumbani hapo wakawa wanalia."

Sayyid Hasim al-Bahrani anasema katika Tafsiri yake ya al-Burhan katika kutafsiri kauli ya Mwenyezi Mungu inayosema: Na tulipochukua agano lenu kuwa hamtamwaga damu zenu, wala hamtatoana majumbani mwenu; nanyi mkakubali nanyi mnashuhudia. Kisha nyinyi kwa nyinyi mnauana, na mnawatoa baadhi yenu majumbani kwao, mkisaidiana kwa dhambi na uadui…..(al-Baqarah 84-85)  kwamba Aya hizi ziliteremka katika kukosoa na kuwakaripia Mayahudi ambao walivunja ahadi na agano lao na Mwenyezi Mungu. Walikiuka amri ya Mwenyezi Mungu, wakamkadhibisha Mtume (saw) na kisha kuwaua Manabii wa Mwenyzi Mungu. Mtume Mtukufu (saw) aliwaambia masahaba zake: 'Enyi Masahaba zangu! Je, nikufahamisheni Mayahudi wa Umma wangu ambao ni sawa na wao?! Wakajibu: Ndio Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mtume (saw) akasema: Kaumu katika Bani Umayyia watadai kuwa wao ni katika Umma wangu, wanadhani kwamba wao ni katika mila yangu. Wanaua wabora wa kizazi changu, wema wa ukoo wangu na kizazi cha binti yangu. Wanabadilisha sheria yangu na kuacha Sunna yangu, wanawaua wanangu wawili, Hassan na Hussein, kama babu zao Mayahudi walivyowaua Zakariya na Yahya. Jueni kwamba, Mwenyezi Mungu anawalaani kama alivyowalaani huko nyuma, na kama anavyosema katika Qur'ani. Kabla ya kuwadia Kiyama, Mahdi wa Umma wa Kiislamu na anayetokana na kizazi cha Hussein madhlumu atawaua na kuwatumbukiza kwenye Jahannam pamoja na mabaki ya dhuria wao, na hivyo kulipiza kisasi cha babu yake al-Hussein, na Siku ya Kiyama watapata adhabu kali zaidi na majaaliwa mabaya…!

************

Na tunaendelea kuzungumzia mambo aliyoyasema Mtume Mtukufu (saw), ambayo ni moja ya dalili za kutumwa kwake humu duniani, ili kuwaarifisha Maimamu kwa wanadamu na kuwajulisha kwamba Watu wa Nyumba yake (as) wanastahiki kutiiwa, kufuatwa, kunusuriwa na kuheshimiwa na si kwamba wavunjiwe heshima na mwishowe kuuawa kinyama. Sheikh Swadouq ananukuu katika kitabu chake cha Aamali hadithi ndefu, ambapo Ibn Abbas amesema: "Siku moja Mtume (saw) alikuwa ameketi ambapo alifika hapo Hassan, na alipomuona alianza kulia. kisha akamwambia: Njoo kwangu, mwanangu. Akaendelea kumkumbatia hadi alipomketisha kwenye mguu wake wa kulia. Kisha akaja Hussein na alipomwona alilia kisha akamwambia: Njoo kwangu, mwanangu. Akaendelea kumkumbatia mpaka akamketisha kwenye mguu wake wa kushoto. Kisha akaja Fatwimah, na alipomuona alilia kisha akamwambia: Njoo kwangu ewe binti yangu! Akamketisha mbele yake. Kisha akafika mbele yake Amirul Muuminina (Ali), na alipomuona, alilia kisha akamwambia: Njoo (karibia) kwangu ewe ndugu yangu! Aliendelea kumshikilia hadi alipomketisha upande wake wa kulia."

Kisha Ibn Abbas anasema kuwa Mtume (saw) aliwatabiria maswahaba zake mambo ambayo yangewafika Ahlu Bait wake, mmoja baada ya mwingine, kutokana na dhulma, mateso na mauaji ambayo yangewafika. Moja ya mambo aliyosema yalitamkwa na Mtume (saw) ni kwamba alisema: "Ama al-Hassan, yeye ni mwanangu anayetokana nami. Ni kiburudisho cha macho yangu, nuru na tunda la moyo wangu. Ni Bwana wa vijana wa Peponi, na Hoja ya Mwenyezi Mungu kwa Umma. Amri yake ni amri yangu na kauli yake ni kauli yangu. Anayemfuata huwa ni katika mimi na anayemuasi huwa si katika mimi. Ninapomtazama huwa ninakumbuka yatakayomfika kutokana na madhila atakayofanyiwa baada yangu. Atafanyiwa hayo yote hadi atakapouawa kwa sumu kidhulma na kiuadui. Hapo Malaika na mbingu zote zitalia. Kila kitu kitamlilia wakiwemo ndege wa angani na samaki wa baharini. Hivyo kila anayelia kwa ajili yake, macho yake hayatapofuka katika siku ambayo macho yatapofuka, na mwenye kuhuzunika kwa ajili yake, moyo wake hautahuzunika katika Siku ambayo nyoyo zitahuzunika, na atakayemzuru (kaburi lake), miguu yake itakuwa thabiti katika Siku ambayo miguu mingine itakuwa inateleza.

Ama al-Hussein - na Hadithi bado ni ya Mtume Mtukufu (saw) – anatokana nami, naye ni mtoto na mwanangu. Ni mbora wa viumbe baada ya ndugu yake, naye ni Imamu wa Waislamu, msimamizi wa waumini, khalifa wa Mola wa walimwengu, msaidizi wa wanaoomba msaada, pango la wanaoomba msaada, Hoja ya Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake wote, na ni Bwana wa vijana wa Peponi na mlango wa kunusurika Umma. Amri yake ni amri yangu na utiifu kwake ni utiifu kwangu. Anayemfuata ni katika mimi, na anayemuasi si katika mimi. Ninapomuona hukumbuka yale yatakayomfika (masaibu/mateso) baada yangu. Ni kana kwamba amefika kwangu (Makka) kuomba hifadhi na asipewe hifadhi hiyo wala kunusuriwa. Akiwa usingizini (kwenye kitanda) ninamkumbatia kifuani na kumwamuru asafiri kutoka mahali pa hijra yangu, na kumpa bishara njema ya kuuawa shahidi. Hivyo anaondoka hapo kuelekea katika ardhi ambako atauawa, ardhi ya huzuni, msiba, mauaji na maangamizi. Kundi la Waislamu litamsaidia, ambapo hao watakuwa miongoni mwa mabwana wa mashahidi wa Umma wangu, Siku ya Kiyama. Ni kana kwamba ninamtazama jinsi alivyopigwa mshale na kuanguka chini kutoka kwenye farasi wake. Kisha anakatwa kichwa kama kondoo dume aliyedhulumiwa. Kisha Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) akalia na wale waliokuwa karibu naye wakalia kwa sauti kubwa, kisha akainuka na kusema:

((Ewe Mola wangu! Ninakushtakia Wewe yatakayowafika Ahlul Bayt wangu baada yangu))... Kisha akaingia nyumbani kwake.

Na hadi hapo…..