Aug 06, 2022 03:54 UTC
  • Jumamosi tarehe 6 Agosti 2022

Leo ni tarehe 8 Muharram 1444 Hijria sawa na Agosti 6 mwaka 2022.

Tarehe 8 Muharram mwaka 61 Hijria maji yaliadimika kabisa katika mahema ya mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as) na watu wengine wa familia yake katika jangwa lenye joto kali la Karbala. Kharazmi katika kitabu cha Maqtalul Hussein na Khiyabani katika Waqaiul Ayyam wameandika kwamba: Katika siku ya nane ya Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Imam Hussein na masahaba zake walikuwa wakisumbuliwa na kiu kali, kwa msingi huo Imam Hussein alichukua sururu na akapiga hatua kama 19 nyuma ya mahema kisha akaelekea kibla na kuanza kuchimba ardhi. Maji matamu ya kunywa yalianza kutoka na watu wote waliokuwa pamoja naye walikunywa na kujaza vyombo vyao kisha maji yakatoweka na hayakuonekana tena. Habari hiyo ilipofika kwa Ubaidullah bin Ziad alimtumia ujumbe kamanda wa jeshi la Yazid mal'uuni, Umar bin Sa'd akimwambia: Nimepata habari kwamba Hussein anachimba kisima na kupata maji ya kutumia, hivyo baada ya kupata risala hii kuwa macho zaidi ili maji yasiwafikie na zidisha mbinyo na mashaka dhidi ya Hussein na masahaba zake."

Siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, nchi ya Bolivia ilifanikiwa kupatia uhuru kutoka mikononi mwa mkoloni Muhispania. Ukoloni wa Uhispania dhidi ya Bolivia ulianza katika karne ya 16 kwa kupora utajiri wa madini wa nchi hiyo. Katika kipindi cha utawala wa Wahispania kulishuhudiwa harakati mbalimbali za wananchi waliokuwa wakipambana na wakoloni hao wakidai uhuru chini ya kiongozi wao Simón Bolívar. Mapinduzi hayo yalianza mwaka 1809 na taratibu yakaenea katika nchi yote ya Bolivia na hatimaye yakafanikiwa kuwaondoa wakoloni hao na kupatikana uhuru katika siku kama ya leo mwaka 1825.

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, alizaliwa Alexander Fleming tabibu, mwanabiolojia na mtaalamu wa madawa wa Scotland. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, tabibu huyo pamoja na wasomi wenzake wawili Chain na Florey, waligundua dawa ya antibiotic ya Penicillin. Mwaka 1945, wasomi hao watatu kwa pamoja walitunukiwa tuzo ya Nobel katika elimu ya tiba kutokana na ugunduzi wao huo muhimu. Penicillin inatumika sana hivi sasa katika elimu ya tiba.

Alexander Fleming

Siku kama leo miaka 77 iliyopita, kwa mara ya kwanza kabisa duniani Marekani iliushambulia vikali kwa mabomu ya nyuklia mji wa Hiroshima huko Japan mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Mabomu hayo yalikuwa na nguvu kubwa ya uharibifu iliyokuwa sawa na tani elfu 20 ya mada za milipuko za TNT. Katika mashambulizi hayo watu zaidi ya elfu 90 waliuawa na wengine 75 elfu kujeruhiwa. Athari mbaya za mabomu hayo ya nyuklia zingali zinashuhudiwa hadi hii leo huko Hiroshima licha ya kupita miaka mingi sasa tangu kufanyike mashambulizi hayo ya nyuklia ya Marekani. Muda mfupi baada ya kuushambulia mji wa Hiroshima, Marekani iliushambulia pia kwa mabomu ya nyuklia mji wa Nagasaki huko huko Japan na kuilazimisha nchi hiyo kusalimu amri. Maafa hayo ya kutisha na kusikitisha yaliyofanywa na Marekani katika miji miwili ya Japan ambayo yanahesabiwa kuwa jinai kubwa zaidi ya kivita katika historia, yanaonyesha kuwa silaha za nyuklia ni wenzo hatari sana katika mikono ya nchi zinazopenda kujitanua duniani kama Marekani na ndiyo maana kuna udharura wa kusimamiwa na kudhibitiwa silaha hizo na taasisi husika, na hatimaye kutokomezwa kabisa kwa ajili ya usalama wa dunia.

Mji wa Hiroshima uliangamizwa na bomu la nyuklia la Marekani

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita nchi ya Jamaica inayopatikana huko Amerika ya Kati ilipata uhuru. Jamaica iligunduliwa mwaka 1494 na mvumbuzi Christopher Columbus na kuwa chini ya himaya ya Uhispania kuanzia karne ya 16 hadi ya 18. Nchi hiyo baadaye ilikoloniwa na Uingereza; na maghasibu wa Ulaya wakawafukuza wenyeji wa kisiwa hicho na badala yake wakawachukua makumi ya maelfu ya watumwa weusi kwa ajili ya kuwalimia mashamba yao.

Siku kama ya leo miaka 34 iliyopita, dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein alilazimika kukubali usitishaji vita na Iran. Baada ya Iran kukubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo tarehe 27 Tir mwaka 1367 Hijria Shamsia ambalo lilijumuisha usitishaji vita baina ya pande mbili, ilitarajiwa kuwa mapigano ya kijeshi baina ya nchi hizo mbili pia yangekomeshwa. Hata hivyo siku kadhaa baadaye Saddam Hussein alifanya mashambulizi makubwa dhidi ya ardhi ya Iran ambayo yalifeli kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa Kiirani. Hatimaye Saddam Hussein ambaye aliilazimisha Iran kuingia katika vita vya miaka 8 vilivyosababisha hasara kubwa ya hali na mali na hakuweza kufikia malengo yake, alikubali kusitisha mapigano katika siku kama hii ya leo na kutekeleza makubaliano hayo wiki mbili baadaye.

Na Miaka 27 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani Agosit 6, 1995, Profesa Kighoma Ali Malima aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha NRA katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi nchini Tanzania aliaga dunia. Malima alizaliwa mwaka 1938 katika wilaya ya Kisarawe mkoa wa Pwani. Akiwa kijana mdogo mwenye umri wa miaka 19 na mwanafunzi hodari alikatisha masomo yake ya sekondari ili ajiunge na TANU katika harakati za kuikomboa Tanganyika kutoka katika utumwa wa Waingereza. Hayati Profesa Malima, atakumbukwa na wapenda haki wengi nchini Tanzania kutokana na kupinga kwake dhulma. Profesa Kigoma Ali Malima aliaga dunia ghafla katika mazingira ya kutatanisha huko mjini London, Uingereza alikopitia kutoka Makka alikokwenda kufanya Umra, zikiwa zimepita siku chache tu tangu alipotangaza uamuzi wake wa kukihama chama tawala cha CCM kufuatia kujiuzulu wadhifa wa uwaziri katika serikali ya chama hicho. Suala hilo lilimfanya akasirikiwe sana na chama hicho cha CCM.

Profesa Kighoma Ali Malima

 

Tags