Aug 29, 2022 08:07 UTC
  • Iran imeanza kupelekea chanjo zake za corona barani Afrika

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Waziri wa Afya, Tiba na Elimu ya Tiba wa Iran ametangaza kuwa Iran iko tayari kuzipatia nchi za Afrika chanjo ya corona.

Wanasayansi na wataalamu vijana wa Iran; Licha ya vikwazo vya Marekani dhidi ya binadamu, wamefanikiwa kuzalisha aina mbalimbali za chanjo za sindano na za kuvuta ili kukabiliana na virusi vya corona, na Shirika la Afya Duniani limethibitisha ubora wa juu wa chanjo zinazotengenezwa na Iran.

Daktari Bahram Ainollahi, Waziri wa Afya wa Iran, aliyasema hayo Agosti 28 wakati akizungumzia mafanikio ya usimamizi wa ugonjwa wa "Covid-19" nchini Iran. Amesema  tayari  Iran imeshaiuzia Venezuela chanjo ya corona na kuongeza kuwa: Tumezitangazia pia nchi za Afrika kuwa tuko tayari kuzikabidhi chanjo ya corona.

Hivi karibuni katika safari yake nchini Mali, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian aliikabidhi nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika zawadi ya chanjo milioni moja za corona aina  ya COVIran Barekat iliyotengenezwa kikamilifu nchini Iran.

Waziri wa Afya wa Iran ameashiria juhudi na ushujaa wa matibabu na wafanyikazi wa matibabu nchini katika kudhibiti na kukabiliana na virusi vya corona, Dakta Ainollahi ameongeza kuwa katika kilele cha kudunga watu dozi ya corona, Iran ilifanikiwa kuweka rekodi ya kudunga dozi milioni moja na elfu 600 za chanjo kwa siku, na chanjo milioni nane na 600 kwa wiki, ambayo ni sawa na idadi ya watu wote katika baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi. Amesema kudunga idadi kubwa ya watu chanjo katika muda mfupi kulifanikisha watu kupata kinga.

Waziri wa Afya amesema pia kuwa iwapo aina yoyote ya kirusi na mikrobu itaonekana duniani, chanjo yake itazalishwa kwa urahisi nchini nchini Iran.

Daktari Bahram Ainollahi , Waziri wa Afya wa Iran aidha amebainisha kwamba kwa mujibu wa ripoti iliyowasilishwa na taasisi za Umoja wa Mataifa nchini Iran, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni miongoni mwa nchi 6 bora katika mapambano dhidi ya Corona.

Hadi sasa Wanasayansi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wanazalisha chanjo mbalimbali kwa kutumia teknolojia na utaalamu wa aina tofauti kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19. 

Chanjo za COVIran Barekat, Razi Cov-Pars Spikogen, PastuCovac, Fakhra na Noura ni miongoni mwa chanjo za ugonjwa wa UVIKO-19 zilizotengenezwa na wataalamu wa Iran na ambazo majaribio na usajili wao umefanyika kwa mafanikio.

Iran inajizalishia dawa

Wakati huo huo, Shirika la Dawa na Chakula la Iran (FDA) limesema asilimia 98 ya dawa zilizoko nchini zinazalishwa na wataalamu wa taifa hili, na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ni miongoni mwa nchi 20 duniani zinazojizalishia dawa kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu.

Bahram Daraei, Mkuu wa Shirika la Dawa na Chakula la Iran aliyasema hayo Agosti 29 katika mahojiano na kueleza kuwa, mafanikio haya yamepatikana licha ya mifumo ya dawa na matibabu ya Jamhuri ya Kiislamu kuwa chini ya vikwazo.

Daraei amenukuliwa na shirika la habari la IRNA akisema kuwa, Marekani inaihadaa dunia kwamba vikwazo vyake havilengi bidhaa za kibinadamu kama dawa.

Afisa huyo wa Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili lilifanikiwa kuzalisha aina sita za chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19, na kwa utataribu huo likafanikiwa pakubwa dhidi ya janga la Corona ambalo linaendelea kusumbua baadhi ya nchi mpaka sasa.

Kadhalika amepongeza mfumo wa afya wa nchi hii, ambao uliundwa na serikali kwa ajili ya kusimamia usambazaji wa dawa kote nchini, jambo ambalo limesaidia kudhibiti magendo ya dawa.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, vikwazo vya Marekani vinazuia kufikishwa vifaa tiba, dawa, teknolojia na ushirikiano wa Iran na taasisi za kifedha za kimataifa, na kuitaja jinai hiyo kama ugaidi wa kimatibabu.

Tanzania yahimiza utafiti wa kisayansi

Serikali ya Tanzania imewataka Wahadhiri wa vyuo vikuu nchini kuongeza machapisho ya tafiti katika majarida makubwa duniani ili waweze kutambulika ulimwenguni kama watafiti wabobezi.

Hayo yalisemwa Agosti 26  jijini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda wakati akifunga Mkutano wa wadau wa kupokea maoni kuhusu Sera ya Taifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu na Kiunzi Cha Uratibu wa Ubunifu nchini, ulioandaliwa na Wizara hiyo, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni (UNESCO)  jijini Dodoma.

Prof. Mkenda amesema kuwa kwa sasa wahadhiri wengi wanaogopa sana kufanya tafiti hasa zile za kisayansi.

Aidha Prof. Mkenda amesema ulimwengu wa sasa hauwezi kuepukana na masuala ya sayansi na Teknolojia hivyo kutaka wadau wote kuchochea udadisi na ubunifu kwa watoto ili baadae waweze kuajirika na kujiajiri.

Hata hivyo  Prof. Mkenda amesema kuwa wizara hiyo ipo mbioni kutambulisha mpango wa ufadhili wa masomo wa “Samia Scholarship” kwa wanafunzi bora 600 waliofanya vizuri kwenye masomo ya sayansi.

Aidha Waziri Mkenda amelishukuru Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) pamoja na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kuwezesha kufanyika mkutano huo huku akiwataka wadau walioshiriki kikao hicho kuendelea kutoa maoni kupitia majukwaa yatakayowekwa.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu Prof. Maulilio Kipanyula, amesema kuwa wamepokea maoni kutoka kwa wadau kuhusiana na kuhuisha rasimu ya Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na kuahidi kwenda kuyafanyia kazi.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Aloyce Kamamba ameiomba serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuyafanyia kazi maoni ya wadau pamoja na kuzichukua, kuzitambua, kuzifadhili na kuziendeleza bunifu zinazobuniwa.

Pia amesema kuwa mawazo yaliyotolewa na wadau yasibakie katika makaratasi yafanyiwe kazi ili kutatua changamoto zilizopo katika jamii kupitia Sayansi, Teknolojia na Ubunifu.

Teknolojia kukabiliana na njaa Kenya

Na  upungufu wa chakula nchini Kenya utaangaziwa endapo wakulima watakumbatia mifumo mbalimbali ya uvunaji maji.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Radeecal Communications, Bw Sanyal Desai alitangaza mapema mwezi Agosti kuwa baa la njaa la mara kwa mara Kenya litakuwa historia wakulima wakihamasishwa kukumbatia mifumo ya kuteka maji katika msimu wa mvua.

Amesema hilo, litawawezesha kukuza mazao mfululizo.

“Ninahimiza Wakenya wakumbatie mifumo na teknolojia za kuvuna maji msimu wa mvua, wayatumie kuendeleza shughuli za kilimo wakati wa kiangazi na ukame,” Bw Desai amesema.

Akisifia udongo wa Kenya katika kufanikisha zaraa, afisa huyo amesema mataifa kama vile India na Misri, baadhi yakiwa jangwani yameweza kukabiliana na kero ya njaa kupitia mifumo ya kuvuna maji.

Desai amesema kuna teknolojia chungu nzima za kuendeleza kilimo, ambazo zikitua nchini zitawaletea wakulima afueni.

Shirika la Radeecal Communications kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo na Ufugaji, liliandaa Maonyesho ya Kimataifa ya Agritech Africa, mwaka huu 2022.

Makala hayo ya saba, yalifanyika katika ukumbi wa KICC, jijini Nairobi, yakivutia washirika kutoka ndani na nje ya nchini.

Mifumo na teknolojia mbalimbali za kuboresha kilimo na ufugaji, ilionyeshwa wakulima wakishauriwa kuikumbatia ili kuimarisha mazao.

Mada ya maonyesho hayo ikiwa ni ‘Uboreshaji Mapato ya Wakulima Kupitia Ubunifu na Teknolojia’, Desai amesisitiza kwamba utoshelevu wa chakula hasa katika kipindi hiki ambapo Kenya na ulimwengu kwa ujumla unatatizwa na mabadiliko ya tabianchi, utachangiwa pakubwa na mifumo ya kisiasa katika kuokoa sekta ya kilimo.

Athari za tabianchi zimechangia mabadiliko ya hali ya hewa, misimu ya mvua kubwa ikisambaratika.