Nov 07, 2022 08:55 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (22)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 22 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitahusu mambo yenye ulazima kwa jamii ili kuweza kuwa na umoja. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Mpendwa msikilizaji, bila shaka ungali unakumbuka, katika sehemu kadhaa zilizopita za kipindi hiki tulizungumzia msingi wa uadilifu katika Mfumo wa Kiislamu na nafasi yake katika mfumo wa uumbaji na sharia za Uislamu. Mkabala na kinyume na msingi huu wa uadilifu kuna suala la dhulma, ambayo kama itapenya na kusambaa katika nguzo za jamii, inaweza kusababisha madhara makubwa kwa uhai na kudumu kwa jamii hiyo. Bila shaka katika mfumo wa kisiasa na kijamii wa Uislamu, ambao ndani yake inatawala misingi kama umoja, suluhu na urafiki, uadilifu na haki; dhulma ni kitu ambacho hakina nafasi ndani yake. Hata hivyo wasiwasi na mshawasha wa mali na madaraka haviwapi utulivu watu wanaojali matumbo na maslahi yao tu, ambao huwa hawawezi kuridhia uadilifu utekelezwe; na kwa sababu hiyo, hupanga na kuandaa kila aina ya njama kwa ajili ya kupambana na mfumo wa kiuadilifu wa Uislamu ili kwa kutumia dhulma, ubaguzi na upendeleo wa kidhalimu waitoe jamii kwenye mkondo wa uadilifu na kufanikisha malengo na maslahi yao ya binafsi na ya kimirengo. Na ni kwa sababu hiyo, Uislamu unapinga vikali na kutukanya hata kukaribiana na madhalimu kwa kusema:  Wala msiwategemee wanao dhulumu, usije ukakuguseni Moto. Wala nyinyi hamna walinzi badala ya Mwenyezi Mungu, wala tena hamtasaidiwa. (Hud 113).

Hakuna shaka kwamba, kama watu na mataifa hayatakubali kuvutwa na kutekwa na madhalimu, iwe ni kwa vitisho au kurubuniwa, mfumo wa kidhalimu hautaweza kusimama katu; na haitatokea kamwe dhalimu yeyote yule kuweza kuwatawalia mambo yao na kuwalazimisha kufuata matakwa yake.

Ni muhimu tutambue kwamba, katika sehemu ya mwisho ya aya tuliyosoma, Qur'ani inaonya kuwa, ikiwa jamii yoyote ile itakubali kuburuzwa na madhalimu, watu wake, si tu hawataonja hata tone la furaha lakini pia itaandamwa na masaibu machungu kwa kuridhia kwake dhulma na uonevu. Si hayo tu, lakini wakati watu hao watakapokuwa wanahiliki kwa dhulma za madhalimu, hatatokea yeyote wa kuwasaidia; na kwa kuwa wameacha kujiegemeza na kuutegemea utawala wa kiuadilifu wa Allah, Yeye Mola pia, ambaye ni mlinzi na msaidizi wa kweli wa waja wake, hatawashika mkono kuwasaidia.

Baadhi ya watu wenye uelewa wa kijuujuu wa mambo huwa wanadhani kwamba, ikiwa madhalimu wataihodhi na kuiburuza jamii yoyote ile, watakaoathirika ni wale watu wa juu, mashuhuri na walio na hadhi tu katika jamii hiyo; na wao hawatapatwa na hatari yoyote. Lakini Qur'ani inaukataa mtazamo huo potofu na kusema: "Na jikingeni na Fitna ambayo haitowasibu walio dhulumu peke yao kati yenu. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mkali wa kuadhibu." (Suratul-Anfal, aya ya 25)

Nukta muhimu na yenye kutafakarisha katika sehemu ya mwisho ya aya tuliyosoma ni kwamba, kuridhia na kusaidia dhulma inayofanywa na madhalimu, mbali na kuharibu maisha ya watu, Mwenyezi Mungu hawasamehe pia wasiojali wala kushughulishwa na hali hiyo; na kutokana na kaida na utaratibu usiobadilika aliouweka Yeye Mola, atawafanya wote wawili, wanaodhulumu na wanaoridhia dhulma, wawe na mwisho mmoja, kama isemavyo aya ya 45 ya Suratul Hajj ya kwamba: "Miji mingapi tuliiangamiza iliyo kuwa ikidhulumu, ikawa imebaki magofu, na visima vilivyo achwa, na majumba yaliyo kuwa madhubuti?"

Kwa mujibu wa aya hii, chanzo cha kuangamizwa staarabu nyingi zilizopita ni dhulma na udhalimu kutawala katika staarabu hizo; mpaka imefikia kuzoeleka sana kusemwa kwamba: "Utawala unaweza kubaki na ukafiri, lakini hauwezi ukadumu kwa dhulma."

Kwa mtazamo wa Uislamu, ambao unapinga na kupiga vita dhulma; kuridhia na kutii tawala za kidhalimu na kiistikbari hakuwezi kutetewa wala kukubalika kwa namna yoyote ile. Ni kuchagua moja kati ya mawili; ama kukabiliana na madhalimu kwa jihadi na mapambano, au kama hakutakuwa na njia yoyote ile ya kuwawezesha wanajamii kukabiliana na kupambana na madhalimu, basi watu na wahajiri kwa kuihama ardhi hiyo na kuhamia ardhi nyingine, ambako wataweza kuendeleza mapambano hadi kuitokomeza dhulma. Qur'ani tukufu inalielezea hilo kama ifuatavyo katika aya ya 97 ya Suratu-Nisaa ya kwamba: "Hakika Malaika watawaambia wale ambao wamewafisha nao wamejidhulumu nafsi zao: Mlikuwa vipi? Watasema: Tulikuwa tunaonewa. Watawaambia: Kwani ardhi ya Mwenyezi Mungu haikuwa na wasaa wa kuhamia humo? Basi hao makaazi yao ni Jahannamu, nayo ni marejeo mabaya kabisa."

Hata kama utamaduni wa kupiga vita dhulma wa dini tukufu ya Uislamu unatufunza kuwa, jukumu la kupambana na madhalimu liko wakati wote na mabegani mwa watu wote, lakini uzito wake unajitokeza na kudhihirika zaidi pale mfumo wa kidhalimu unapowaminya na kuwakandamiza unaowadhulumu mpaka wakalazimika kupaza juu sauti zao za vilio kwa ajili ya kuomba msaada. Inapofika hatua hiyo, Qur'ani inawatangazia na kuwafikishia ujumbe watu wa jamii ya Kiislamu, hasa wale wanaojihisi kuwa hawana masuulia yoyote kwa watu wanaodhulumiwa, kwa kuwaambia: "Na mna nini msipigane katika Njia ya Mwenyezi Mungu na ya wale wanao onewa, wanaume na wanawake na watoto, ambao husema: Mola Mlezi wetu! Tutoe katika mji huu ambao watu wake ni madhaalimu, na tujaalie tuwe na mlinzi anaye toka kwako, na tujaalie tuwe na wa kutunusuru anaye toka kwako." (Suratu-Nisaa, aya ya 75)

Mpendwa msikilizaji, baada ya maelezo yote hayo, tunafikia hitimisho kwamba, jamii ya Kiislamu itaweza kulinda na kudumisha umoja na mshikamano wake pale itakapoelekeza matumaini yake katika kutekeleza uadilifu, ikawa na nguvu, uwezo na heshima; na watu wake wakaishi katika anga ya udugu bila kuwepo dalili au alama yoyote ya dhulma na uonevu katika mfumo wake wa kisiasa na kijamii. Na kwa maelezo hayo basi  mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa sehemu ya 22 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 23 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/

 

 

Tags