Nov 09, 2022 07:53 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (28)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 28 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaendelea kuzungumzia nukta nyingine ya akhlaqi katika Uislamu kwa kutilia mkazo juu ya taasisi muhimu ya familia. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Mpendwa msikilizaji, bila shaka ungali unakumbuka kuwa, katika kipindi kilichopita tulieleza kwamba, taasisi ya familia, si tu inaweza kuwa na taathira kubwa mno katika mustakabali wa watoto, lakini nafasi na mchango wake unaweza kuathiri pia vizazi vya baadaye; na kimsingi na muhimu zaidi kuliko yote hayo, kuchangia hatima yetu katika maisha ya milele ya baada ya kifo; ambapo jamaa wote wa familia iliyoishi maisha ya kweli ya Kiislamu, watakutanishwa pamoja kwenye Pepo ya Mwenyezi Mungu.

 Qur’ani tukufu inalizungumzia hilo kama ifuatavyo katika aya ya 23 na 24 za Suratu-Ra’ad: “Nayo ni Bustani za milele, wataziingia wao na walio wema miongoni mwa baba zao, na wake zao, na vizazi vyao. Na Malaika wanawaingilia katika kila mlango. (Wakiwaambia) Assalamu Alaikum! Amani iwe juu yenu, kwa sababu ya mlivyo subiri! Basi ni mema mno malipo ya Nyumba ya Akhera.”

Hapana shaka yoyote kuwa, hatima hiyo njema ya malipo bora kabisa ya Pepo ni matokeo ya mtindo wa maisha ya familia iliyokuwa imepambika hapa duniani kwa sifa na thamani zote za ibada za kiakhlaqi, kijamii, kidini na kiutu; na kwa kiwango fulani kwa kuishi maisha yenye mfanano na wa Peponi. Katika kuwazungumzia watu wa kundi hili, ambao hapa duniani walijisalimisha kwa Mwenyezi Mungu na wakapanga mipango na malengo ya maisha yao kwa namna alivyotaka Yeye Mola wao, aya ya 62 ya Suratu-Yunus inasema: “Jueni kuwa vipenzi vya Mwenyezi Mungu hawatakuwa na khofu wala hawatahuzunika.”

Wakati watu wengi hawaonyeshi kuridhika na jinsi walivyopitisha maisha yao ya huko nyuma na wana hofu na wasiwasi kuhusiana na mustakabali wao, sababu gani inawafanya vipenzi vya Mwenyezi Mungu wasiwe hivyo, bali wawe kwenye hali ya utulivu maalumu? Aya inayofuatia ya sura hiyo, inalijibu suali hilo la msingi kwa kusema: “Hao ni ambao wameamini na wakawa wanamcha Mungu.”

Hata kama Mwenyezi Mungu Mtukufu amebainisha ndani ya kitabu cha mwongozo wa maisha cha Qur’ani misingi mikuu ya kufuatwa kwa ajili ya kuishi maisha bora, lakini inatupasa kujifunza na kufuata kigezo na mfano wa kivitendo wa maisha hayo katika sira ya Bwana Mtume SAW na ya watu maasumu na watoharifu wa kizazi chake, ambayo imewapa na itaendelea kuwapa ilhamu ya kuiga mawalii na vipenzi vya Mwenyezi Mungu.

Bwana Mtume SAW alikuwa akiuusia umma wake kwa kusema: “Yeyote anayetaka maisha yake na kufa kwake viwe sawa na nilivyoishi mimi na kutawafu; na kwa hivyo aweze kuingia kwenye “jannatu adn”, ambayo ni Pepo iliyoahidiwa na Mwenyezi Mungu, inampasa amfanye Ali na wanawe walio maasumu, viongozi na maimamu wake; kwani wao ni watu bora kwa elimu na ufahamu na waongozaji watu kuelekea njia ya uongofu.” (Tafsiri ya Nuru-thaqalaini, Juzuu ya Pili)

Kwa maana hiyo, inatupasa tuwe makini kwa kila hali katika kuchagua kigezo cha kufuata kwa ajili ya kufunga ndoa na kuasisi familia bora. Ikiwa kigezo na ruwaza yetu itakuwa ni waja wateule wa Mwenyezi Mungu, hapana shaka tutaweza kuyafikia malengo na matarajio yetu matukufu ya kidini na kiutu. La kama tutaamua kuiga vigezo vya Kimagharibi, tukawa hatujui chochote kuhusu misingi na thamani za Uislamu halisi; na tukajenga taasisi ya ndoa na familia kwa kufuata fikra na nadharia zao, hapana shaka mwishowe tutakuja kushuhudia kuporomoka kwa familia zetu katika kila nyanja. Katika Hadithi yenye kusisimua mwili na kuutingisha moyo, Bwana Mtume SAW, aliitabiri hatima hii chungu na ya kuhuzunisha alipotukanya kwa kusema: “Msiba ulioje kwa watoto wa Aakhiru-zaman kutokana na mwenendo wa baba zao.” Hapo akauliza mwenye kuuliza: Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ni kutokana na baba zao walio washirikina? Bwana Mtume akasema: “Kutokana na baba zao (waonekanao kidhahiri kuwa ni) Waislamu, ambao hawawafunzi watoto wao mafundisho yoyote ya dini; na hata kama wao wenyewe watataka kujifunza mafundisho ya Kiislamu, wanawazuia. Kitu pekee kinachowashughulisha ni kuwa na hali nzuri kiuchumi, hata kama si cha hali ya kuridhisha. Mimi ninachukizwa na baba hao (ambao kidhahiri ni) Waislamu na wao pia wanachukizwa na mimi (na mwenendo wangu wa maisha). “(Jaamiul-Akhbar, uk, 106- Mustadrakul-Wasaail)

Qur’ani tukufu imeweka wazi kuhusu hatima ya familia bora ya Kiislamu katika ulimwengu wa milele wa akhera na pia ya familia iliyojiweka mbali na misingi na thamani za kidini. Kuhusiana na watu wa kundi la kwanza, ambao wameasisi ndoa na familia zao kwa ajili ya kuyafikia malengo ya ukamilifu wa kiutu yatokanayo na Uislamu wa asili na kwa kufuata miongozo ya Mola wao na dini yao, aya ya 64 ya Suratu-Yunus inasema: “Wao wana bishara njema katika maisha ya dunia na katika Akhera. Hapana mabadiliko katika maneno ya Mwenyezi Mungu. Huko ndiko kufuzu kukubwa.”

Na ama kuhusu familia za kundi la pili, mbali na kutaja sifa zao mbaya, aya ya 25 ya Suratu-Ra’ad inabainisha wazi pia mwisho wao utakavyokuwa katika ulimwengu mwingine kwa kusema: “Na wale wanao vunja ahadi ya Mwenyezi Mungu baada ya kuzifunga, na wanakata aliyo amrisha Mwenyezi Mungu yaungwe, na wanafanya ufisadi katika nchi: hao ndio watakao pata laana, na watapata Nyumba mbaya.”

Katika hitimisho la mazungumzo yetu haya tunaweza kusema kwamba, maelezo ya aya za Mwenyezi Mungu yanaweka wazi kwa kila namna nafasi ya kipekee ya taasisi ya ndoa na familia katika Uislamu. Kwa maana hiyo, haitakiwi kwa namna yoyote ile mtu akimbilie kufunga ndoa kwa sababu ya vivutio vya kihisia tu na mambo ya kupita; bali kinyume chake. Yaani afanye uchunguzi na uhakiki kwa uelewa na wa pande zote katika kuanzisha taasisi ambayo, itakuwa sababu ya yeye kufuzu na kupata hatima njema duniani na akhera. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji niseme pia kuwa, sehemu ya 28 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 29 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/