Nov 10, 2022 16:31 UTC
  • Akhlaqi Katika Uislamu (38)

Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 38 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitazungumzia umuhimu wa uhuru na kujitawala kiutamaduni katika Akhlaqi za Kiislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.

Bila shaka mpendwa msikilizaji ungali unakumbuka kuwa katika vipindi kadhaa vilivyopita tulizungumzia nafasi ya elimu na fikra, urazini na utumiaji akili na jinsi ujinga na ujahili unavyopigwa vita katika mfumo wa kiutamaduni wa Uislamu. Tukaeleza kwamba vielezi hivi na sifa zake maalumu za thamani ndivyo vinavyoupa umma wa Kiislamu lengo, muelekeo na utambulisho maalumu. Sambamba na hayo, msingi muhimu sana unaohifadhi utambulisho huo ni "kujitawala kiutamaduni". Katika mtazamo jumla, utamaduni unajumuisha dini, lugha, mila na desturi, mtindo wa maisha, sanaa, mfumo wa elimu, vyombo vya habari vya sauti na filamu, vya kawaida na vya intaneti pamoja na ulimwengu wa siasa na uchumi. Na baina ya vyote hivyo, mitazamo ya kiimani na kiitikadi ndio mhimili wenye nafasi kuu na ya msingi.

Tunapotupia jicho harakati za Mitume wa Mwenyezi Mungu tutabaini kuwa zililenga kupambana na utamaduni uliochanganyika na shirki, ujahili pamoja na kutii na kufuata mambo kibubusa, ambao uliwafanya watu wa mataifa waridhie kunyongeshwa na kugeuzwa watumwa dhalili na kukosa kuwa na uwezo wowote wa kuchagua na kujichukulia maamuzi. Kwa kufuata ilhamu waliyopata katika fikra safi za tauhidi, Manabii wa Mwenyezi Mungu walijitahidi kwa uwezo wao wote kuhakikisha wanawakomboa watu wa zama zao na kila aina ya utegemezi au kuridhia kunyongeshwa; na kuufufua ndani ya nafsi zao moyo wa kujiamini, kuwa na izza na kuwa huru.

Bwana Mtume SAW aliendeleza njia ya Mitume waliomtangulia kwa kuasisi misingi ya "Kujitawala Kiutamaduni" kupitia mbiu ya Laa Ilaaha Ila Allah iliyosimama dhidi ya utamaduni wa mihimili ya wenye nguvu za madaraka na utajiri wa mali; na kwa kuwataalamisha watu kupitia miongozo ya wahyi akaweza kuwajenga kimtazamo na kiitikadi, wakawa na utamaduni wa kujitawala na kujitegemea. Lakini mkabala na harakati hiyo, maashrafu na mamwinyi wa Kikureishi na watawala madikteta, ambao walihisi mamlaka yao ya kiistikbari na kimabavu yako hatarini, wao walijitokeza uwanjani kwa nguvu na uwezo wao wote kuhakikisha watu wanaendelea kubaki ujingani na utumwani na kutoweza kuwa viumbe waliokomboka kifikra na kiimani.

Mpendwa msikilizaji, ili tuweze kupata mwanga zaidi wa kuelewa nafasi na mchango wa kipekee wa "Uhuru na Kujitawala Kiutamaduni" inatupasa tujue kwamba leo hii kuliko zama zozote zile, kina Abu Sufiyan na kina Muawiya wa zama hizi, wamepatwa na wasiwasi mkubwa katika kipindi hiki nyeti na hasasi cha kuufufua Uislamu wa asili, unaoleta mageuzi ya msingi kiimani na kiitikadi; na wamejitokeza uwanjani kupambana na Uislamu. Uislamu ambao katika aya ya 110 ya Suratu Aal Imran unauhutubu umma wake ya kwamba: "Nyinyi mmekuwa bora ya umma walio tolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu"… na katika aya ya 139 ya sura hiyohiyo unawaambia: "Wala msilegee, wala msihuzunike, kwani nyinyi ndio wa juu mkiwa ni Waumini."  Na katika aya ya 8 ya Suratul-Munafiqun, Uislamu huo unanadi: "Na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye utukufu - Yeye, na Mtume wake, na Waumini."

Kwa muktadha huo, Uislamu sahihi unauonyesha umma wa Kiislamu, bali ulimwengu mzima wa wanadamu njia na namna ya kuufikia "Uhuru na Kujitawala Kiutamaduni" ambao ndio msingi mkuu wa kujitawala kisiasa, kiuchumi na kijeshi. Kwa maneno mengine ni kuwa, katika mtazamo na imani ya tauhidi ya Uislamu hakuna njia wala kisingizio chochote cha kuhalalisha msimamo wa kuridhia kunyongeshwa na kudhalilishwa na tawala za kikafiri duniani; na hatua yoyote inayochukuliwa na jamii au serikali yoyote ile hususan tawala zinazojionyesha kidhahiri kuwa ni za Kiislamu, ya kujidhalilisha mbele ya viongozi madikteta wa Marekani, Ulaya na wa Kizayuni, inakinzana na irada na takwa la Mwenyezi Mungu, kama inavyoeleza sehemu aya mwisho ya 141 ya Suratu-Nisaa ya kwamba: "...wala Mwenyezi Mungu hatawapa makafiri njia ya kuwashinda Waumini." 

Kwa kufuata ilhamu ya utamaduni unaojenga izza, uhuru na kujitawala wa tauhidi inayotokana na Qur'ani, Imam Ali (AS) anasema hivi katika sehemu ya barua ya 31 ya Nahjul-Balagha: "usiwe mtumwa wa mtu na hapana shaka Mwenyezi Mungu amekuuumba wewe ukiwa huru." Hata hivyo vinara wa ubeberu, ambao lengo lao ni kuwatwisha Waislamu utamaduni wa kikoloni, wameamua kutumia mbinu mbalimbali za kuanzisha matapo ya fikra na itikadi potofu kama ya Uwahabi wa Saudia, Ukufurishaji, Matalibani, Daesh na Irfani za kisasa ili kukabiliana na Uislamu wa asili. Kwa upande mwingine, wamekuwa wakiendesha kampeni mbalimbali za kuchoma moto misahafu, kuchapisha na kusambaza vikatuni vya kumvunjia heshima Mtume SAW, kuwahami waandishi vibaraka kama Salman Rushdie, kutoa vitisho, kuweka vikwazo na kuwasha moto wa vita kwa nia ya kuyapoka mataifa ya Kiislamu uhuru na kujitawala kwao kifikra, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi. Na wakati huohuo wanatumia pia nyenzo za sanaa, fasihi na vyombo vya habari ili kuwadumza kifikra, kuzima mwamko na kudhoofisha uelewa wa watu wa mataifa hayo.

Kuna nukta moja muhimu na ya kuzingatia hapa, nayo ni kwamba, kama tunataka kulinda uhuru wetu wa kiutamaduni kulingana na mafunzo ya Uislamu, yaani kutunza imani zetu za kidini na thamani za kiutu za umma wa Kiislamu pamoja na kutetea utambulisho na uhuru wetu, tujue kuwa, lengo la kufanya hivyo si kuacha kufaidika pia na mafanikio yaliyopatikana katika tamaduni za mataifa mengine. Kwa maneno mengi ni kwamba, sisi kama Waislamu, tunakaribisha kuwa na mabadilishano ya kiutamaduni na wengine, lakini hatukubaliani na hujuma za kiutamaduni. Ni kama alivyoeleza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamanei ya kwamba lengo ni “kusimama imara dhidi ya vipimo batili na vibovu vya dunia na njama za kuleta mabadiliko ambayo mlengwa wake mkuu ni Mapinduzi ya Kiislamu.” Katika sehemu ya hotuba aliyotoa atrehe 13 Julai 1992, Ayatullah Khamenei alitahadharisha kwa kusema: “adui anatumia njia ya uenezaji utamaduni mchafu, ufisadi na ufuska ili kutupokonya vijana wetu”.

Mfano mmoja muhimu sana wa kihistoria wenye kutoa ibra na mazingatio kuhusu udharura wa kulinda uhuru wa kiutamaduni, ni kadhia ya kuanguka utawala wa miaka 800 wa Waislamu katika ardhi ya Uhispania ambao ulikuwa umefikia kilele cha nguvu na uwezo; lakini kutokana na ushawishi wa madola ya Magharibi, kudhoofika kwao kiutamaduni kwa kuruhusu mahusiano holela baina ya vijana, kuenea maovu na ufisadi, kudhoofika imani za kidini, kubadilishwa mfumo wa elimu, kupoteza utambulisho kizazi cha vijana na kupinduliwa viongozi Waislamu wa majina na wapenda starehe na anasa, zama za nguvu, izza na utukufu wa Waislamu zilihitimishwa katika ardhi hiyo; na hiyo kwa hakika ni kengele ya tahadhari kwa Ulimwengu wa Kiislamu na ambayo Qur’ani tukufu imeibainisha kwa kueleza lengo kuu la maadui walioukamia Uislamu, kama inavyotufahamisha sehemu ya aya ya 217 ya Suratul Baqarah ya kwamba: "Wala hawatoacha kupigana nanyi mpaka wakutoeni katika Dini yenu kama wakiweza." Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji, niseme pia kwamba, sehemu ya 38 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 39 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/