Akhlaqi Katika Uislamu (46)
Amani ya Allah, rehma na baraka zake ziwe juu yako mpendwa msikilizaji popote pale ulipo wakati huu. Nakukaribisha kusikiliza sehemu hii ya 46 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu nikiwa na matumaini kuwa, mimi pamoja na wewe tutanufaika na yale tutakayoyasikia katika kipindi hiki ambacho kwa leo kitaendelea kuzungumzia na kuchambua "Akhlaqi za Kisiasa" katika Uislamu. Endelea kuwa nami basi hadi tamati ya mazungumzo yetu.
Mpendwa msikilizaji, bila shaka ungali unakumbuka kuwa katika mfululizo uliopita wa 45 wa kipindi hiki tulianza kuzungumzia mfungamano usiopambanulika wa “dini na siasa” kulingana na mafundisho ya Uislamu; na kwa kutaja mifano ya wazi iliyoshuhudiwa wakati wa ukhalifa wa Imam Ali AS tukaonyesha kuwa, hakuna mfanano wala nukta yoyote ya pamoja kati ya siasa za Uislamu wa asili na siasa za kishetani na kitaghuti za watawala wa kiimla na kidikteta wa zama na mahala popote pale.
Katika kuichambua na kuichanganua zaidi maudhui hii, leo tutagusia machache yaliyoelezwa na Qur’ani kuhusu misingi ya akhlaqi za kisiasa za Uislamu.
Kinyume na mtazamo finyu na wa kijuujuu wa mambo walionao baadhi ya watu kwamba Qur’ani ni kitabu kilichojifunga kuzungumzia baadhi ya masuala ya kiakhlaqi, kimaadili na kimaanawi tu, ukweli ni kwamba, kitabu hicho kitukufu cha mbinguni kimetoa dira na mwongozo kamili kwa ajili ya maisha safi, ya saada na fanaka na ya kuipa ukamilifu jamii ya wanadamu katika nyanja zote za mtu binafsi na jamii kwa ujumla. Kutokana na mtazamo wake huo unaojumuisha kila kitu, na ili kuwafanya viongozi waweze kuwa na nafasi kuu na ya misngi katika kuainisha hatima za kila taifa na umma, sio tu Qur’ani haijaufumbia macho ulimwengu wa siasa, bali umeasisi pia chuo cha siasa ambacho kimevipiku vyuo na nadharia zote za kisiasa zilizobuniwa ulimwenguni.
Katika mtazamo na uono wa kiujumla, Qur’ani inazigawanya tawala za kisiasa katika sura ya tawala za tauhidi na haki; na za kishetani zinazojumuisha shirki na ukafiri na batili. Katika kulifafanua hilo, kitabu hicho cha mbinguni kimetoa taswira ya tawala za hekima na busara za manabii Yusuf, Daud na Suleiman (AS), ambazo zilikuwa na sifa za kipekee katika kila nyanja; na kwa upande mwingine kimezungumzia tawala za kidhalimu na za shirki za kina Namrud, Firauni na kaumu za Adi na Thamudi na kubainisha kupanda na kuporomoka kwao kulingana na kaida na utaratibu alioweka Mwenyezi Mungu. Qur’ani tukufu inauelezea pia ujumbe wa Mitume wote wa Mwenyezi Mungu kwa watu kama inavyoeleza aya ya 36 ya Suratu-Nahl ya kwamba: “Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani”.
Ni kwa kuzingatia madhumuni ya wito huo wa Mwenyezi Mungu, ndipo Nabii Ibrahim AS alisimama kuukabili utawala mwovu na wa kidhalimu wa zama zake; na licha ya kuandamwa na kila aina ya vitisho, akapeperusha bendera ya Tauhidi na imani ya Mungu pekee wa haki na akawatangazia kinagaubaga na kwa moyo thabiti mataghuti kama isemavyo aya ya nne ya Suratul-Mumtahinah ya kwamba:”Hakika sisi tumejitenga nanyi na hayo mnayo yaabudu badala ya Mwenyezi Mungu. Tunakukataeni; na umekwisha dhihiri uadui na chuki baina yetu na nyinyi mpaka mtakapo muamini Mwenyezi Mungu peke yake.”
Aya hii tukufu inabainisha kwa uwazi kabisa kwamba lugha na misamiati ya Uislamu ya kisiasa, kitauhidi na ya kupambana na ukafiri inatakiwa iwe ya uwazi na ya msimamo wa kujiamini; na mpaka pale kambi ya ubeberu na uistikbari itakapokuwa tayari kuacha misimamo na mielekeo yake ya kuipiga vita haki, wafuasi wa njia ya Tauhidi wasilegeze kamba wala wasirudi nyuma katika msimamo wao, isipokuwa kama mabeberu hao wataacha vitimbi na uadui wao wa siri na wa dhahiri pamoja na njama na fikra zao za kishetani.
Hata hivyo, kinyume na ilivyokuwa njia na sira ya Mitume wote, ya kusimama kuzikabili tawala za kitaghuti za zama zao ili kuimarisha na kulinda utamaduni wa kitauhidi; katika kila zama walikuwepo na wanaendelea kuwepo baadhi ya watu ambao, pamoja na kuonyesha kuwa wana imani ya dini, lakini kwa sababu ya kulinda nafasi na maslahi yao, huwa tayari wakati wowote ule kujikurubisha kwa watawala mataghuti. Katika aya ya 60 ya Suratu-Nisaa, Qur’ani tukufu inaukana waziwazi mtazamo na muelekeo wa watu hao ambao unakinzana na utamaduni wa kisiasa na kitauhidi wa Uislamu wa asili iliposema: “Huwaoni wale wanao dai kwamba wameamini yale yaliyo teremshwa kwako na yaliyo teremshwa kabla yako? Wanataka wakahukumiwe kwa njia ya upotofu, na hali wameamrishwa wakatae hayo! Kama tunavyoona katika sehemu ya mwisho ya aya hii, na ili kutubainishia ni nani hasa anayewasukuma na kuwaelekeza watu hao kwenye msimamo huo potofu wa kisiasa, Mwenyezi Mungu anasema: “Na Shet'ani anataka kuwapotezelea mbali”.
Kwa maelezo haya ni kwamba, kutokana na utamaduni asili wa tauhidi, haiwezekani mtu awe na itikadi sahihi ya usuli na misingi ya tauhidi, kisha avutike kwa namna yoyote ile kuzikumbatia tawala za kibeberu na kiistikbari. Mbali na nukta hii kuthibitisha jinsi dini na siasa zisivyoweza kutenganishwa, inabainisha kwa uwazi pia kwamba, utamaduni wa kitauhidi na kisiasa wa Uislamu haufanani na wala hauendani pamoja kwa namna yoyote na ulimwengu wa siasa za watawala na vinara wa ukafiri, shirki na unafiki. Ulimwengu ambao, umejengwa juu ya msingi wa uchupaji mipaka, uonevu, udhalimu, ukandamizaji na ukanyagaji haki za kidini na kiutu za jamii ya wanadamu.
Inafaa tujue pia kwamba, katika fikra za kisiasa za Uislamu, kuzikana na kuzikataa tawala za kitaghuti kumetangulizwa mwanzo kabla ya kumwamini na kumkubali Mungu na Mola pekee wa haki. Katika sehemu ya aya ya 256 ya Suratul-Baqarah, Qur’ani tukufu inasema: “Basi anaye mkataa Shet'ani na akamuamini Mwenyezi Mungu bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisicho vunjika”.
Kwa kutegemea usuli na misingi hii ya kitauhidi, na ili kuubainisha na kuuonyesha kwa matendo mfungamano na mshikano huo wa dini na siasa, baada ya Bwana Mtume SAW kuhajiri Makka na kuhamia Madina aliasisi utawala imara na madhubuti, uliosimama kuyakabili madhihirisho yote ya tawala za kishetani na kiistikbari. Wakati wa utawala wake huo, Bwana Mtume SAW aliwaandikia barua viongozi wa madola makubwa na yenye nguvu ya zama hizo, zilizowalingania na kuwaita kwenye Uislamu; na chini ya kivuli cha mfumo wa kisiasa wa Uislamu aliondoa mifarakano akajenga umoja, akafuta dhulma na kuleta haki na uadilifu, akautokomeza ubaguzi na upendeleo na kuleta usawa, akazima moto wa vita na uadui na kuleta suluhu na amani, akaviondoa vinyongo na chuki kwa upendo na urafiki na akafuta kila itikadi na ibada potofu ya kuabudu masanamu kwa tauhidi na imani ya Mungu pekee wa haki. Na kwa maelezo hayo mpendwa msikilizaji, niseme pia kwamba, sehemu ya 46 ya kipindi cha Akhlaqi Katika Uislamu imefikia tamati. Hivyo sina budi kukuaga hadi wakati mwingine inshallah, tutakapokutana tena katika sehemu ya 47 ya kipindi hiki. Namuomba Mola wa haki akubariki; na amani, rehma na baraka zake ziendelee kuwa juu yako…/