Jun 20, 2016 23:33 UTC
  • Jumanne Juni 21

Leo ni Jumanne tarehe 15 Ramadhani 1437 Hijria sawa na Juni 21, 2016.

Siku kama ya leo miaka 1434 iliyopita, alizaliwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), mmoja wa Ahlul-Bait wa Mtukufu Mtume (saw). Imam Hassan (as) alikulia chini ya malezi na usimamizi wa Mtume, Bibi Fatimat Zahraa binti ya Mtume na Imam Ali (as). Baada ya kuuaw a shahidi baba yake, yaani Imam Ali bin Abi Twalib hapo mwaka wa 40 Hijiria, mtukufu huyo alifanya kazi kubwa ya kusimamia na kuwaongoza Waislamu. Mwanzoni Waislamu wengi walimbai na kumpa mkono wa utiifu Imam Hassan, lakini mfumo wa utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiongozwa na Muawiya mwana wa Abu Sufiyan ambao wakati huo ulikuwa na nguvu kubwa, ulianzisha uadui na chuki dhidi ya mjukuu huyo wa Mtume. Hatimaye Imam Hassan (as) alijiandaa kukabiliana na Bani Umayyah, lakini viongozi wengi wa jeshi lake walidanganyika na ahadi za uongo za maadui na kumuacha peke yake Imam, hali iliyomlazimu mtukufu huyo kufanya suluhu na mtawala huyo wa Bani Umayyah kwa lengo la kulinda dini tukufu ya Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita yaani sawa na tarehe 21 Juni 1970, alifariki dunia Dakta Ahmed Sukarno mpigania uhuru wa Indonesia. Sukarno alizaliwa mwaka 1901, na alikuwa mstari wa mbele katika mapambano yake dhidi ya mkoloni Mholanzi nchini humo. Kwa minajili hiyo, Sukarno aliwahi kukamatwa na kufungwa jela miaka minne na utawala wa kikoloni wa Uholanzi. Baada ya kifungo hicho alitiwa tena mbaroni na kubaidishwa. Mnamo mwaka 1949 alichaguliwa kuwa rais wa Indonesia na ilipofika mwaka 1965 Ahmed Sukarno aliondolewa madarakani baada ya kufanyika mapinduzi ya kijeshi yaliyoongozwa na Janerali Suharto.

Na miaka 35 iliyopita sawa na tarehe Mosi Tir mwaka 1360 kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, hayati Imam Ruhullah Khomeini alipasisha uamuzi wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu wa kutokuwa na imani na rais wa wakati huo Abul Hassan Bani Sadr na kwa utaratibu huo kiongozi huyo akalazimika kung'atuka madarakani. Bani Sadr ni miongoni mwa watu waliojidhihirisha kuwa wapenzi na watetezi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya Imam Khomeini kuhamia Paris, Ufaransa na alifanikiwa kushika madaraka ya nchi na kuwa rais katika uchaguzi wa kwanza wa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini kwa kutumia ujanja wa kipropaganda. Muda mfupi baadaye Imam Khomeini alimkabidhi ukamanda wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo Bani Sadr aliyekuwa mtu mwenye uchu wa madaraka, mwenye kiburi na msaliti alianza mara moja kushirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuangusha utawala wa Kiislamu nchini Iran.