Jun 21, 2016 23:23 UTC
  • Jumatano, Juni 22, 2016

Leo ni Jumatano tarehe 16 Ramadhani 1437 Hijria inayosadifiana na tarehe 22 Juni 2016.

Siku kama ya leo miaka 75 iliyopita, wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, jeshi la Ujerumani ya Kinazi lilianza mashambulizi makubwa dhidi ya Urusi ya zamani kwa jina la Operesheni ya Barbarossa. Kwa utaratibu huo Adolph Hitler akaanzisha vita vingine katika upande wa mashariki mwa Ujerumani kwa shabaha ya kutimiza mipango yake ya kutaka kujitanua zaidi. Hadi wakati huo tayari dikteta huyo alikuwa ameteka nchi kadhaa za Ulaya.

Katika operesheni hizo, askari wa Ujerumani walisonga mbele na kufika katika viunga vya mji mkuu wa nchi hiyo, Moscow. Hata hivyo jeshi la Ujerumani lilipata matatizo makubwa kufuatia kuanza kipindi cha baridi kali na hivyo likashindwa kusonga mbele. Wananchi na jeshi la Urusi katika miji mbalimbali ya nchi hiyo hususan Moscow, Leningrad na Stalingrad walipambana vikali na jeshi hilo vamizi na kulilazimisha kurudi nyuma. Mwezi Agosti 1944 jeshi la Urusi lilifika katika mipaka ya Ujerumani.

Miaka 383 iliyopita katika siku kama hii ya leo mnajimu, mtaalamu wa hisabati na mwanafizikia wa Italia Galileo Galilei alilazimika kukana itikadi zake za kisayansi na kielimu mbele ya viongozi wa Kanisa. Mwaka 1632 Galilei aliandika kitabu akijibu na kukosoa mitazamo ya Betlemosi kuhusu sayari ya jua na kutangaza kuwa dunia inazunguma jua. Mwaka mmoja baadaye Papa wa Kanisa Katoliki alimwita Galileo mjini Roma na kuitaja mitazamo hiyo ya kisayansi kuwa ukafiri. Kwa msingi huo, kanisa lilimlazimisha Galileo akane itikadi zake za kielimu la sivyo akabiliwe na adhabu ya kifo. Japokuwa msomi huyo alikana mitazamo yake hiyo ya kielimu kidhahiri tu lakini wakati alipotoka nje ya mahakama alipiga chini mguu wake na kuiambia ardhi: "Licha ya haya yote lakini wewe unazunguka."

 Na siku kama ya leo miaka 710 iliyopita yaani tarehe 16 Ramadhani mwaka 727 Hijria alifariki dunia msomi na mtaalamu wa hadithi na fasihi wa Kiislamu Ibn Zamlakani. Alipata elimu kwa maulama wakubwa wa zama hizo na kupata ruhusa ya kutoa fatuwa akiwa kijana mwenye umri wa miaka 20. Sambamba na kujishughulisha na masuala ya ukadhi, Ibn Zamlakani alitoa elimu na kufundisha katika vyuo vingi vya Damascus. Miongoni mwa vitabu vya msomi huyo wa Kiislamu ni al Burhanul Kashif An Iijazil Qur'an.