May 24, 2023 15:50 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 909. Baada ya kukamilisha tarjumi na maelezo ya sura ya 43 ya Az-Zukhruf, katika darsa hii tutaanza kutoa tarjumi na maelezo kwa muhtasari ya sura ya 44 ya Ad-Dukhan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya kwanza hadi ya nne ya sura hiyo ambazo zinasema:

حم

H'a Mim

وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ

Naapa kwa Kitabu kinacho bainisha,

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ

 Hakika tumekiteremsha katika usiku ulio barikiwa. Hakika Sisi ni Waonyaji. 

فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ

Katika usiku huo hubainishwa kila jambo la hikima,

Kuna sura saba za Qur'ani ambazo zinaanza kwa herufi za mkato za Haa miim. Mbali na sura hii ya ad-Dukhan, sura nne za kabla yake na sura nyingine mbili zinazofuatia baada yake, nazo pia zimeanza kwa herufi hizo. Kama tulivyotangulia kueleza hapo kabla, kiujumla, baada ya kutangulia herufi hizi, huwa inazungumziwa adhama ya Qur'ani na nafasi yake katika kumuelekeza mwanadamu kwenye uongofu. Katika sura hii ya ad-Dukhan pia Allah SWT ameiapia Qur'ani; kitabu ambacho muhtawa na yaliyomo ndani yake yako wadhiha na yanaweka wazi kila kitu; na mafundisho yake yako hai daima dawamu; na yenyewe Qur'ani, ni hoja ya kuthibitisha ukweli wake. Sehemu inayofuatia ya aya za sura hii inaashiria hadhi ya Kitabu hicho mbele ya Allah SWT na kueleza kwamba: Kitabu hiki kimeteremshwa katika wakati bora kabisa wa kila mwaka, ambao ni Lailatul-Qadr. Kisha aya zinazungumzia sifa muhimu ya usiku huo wenye cheo na kueleza kwamba, usiku wa Lailatul-Qadr ilioteremshwa Qur'ani ni usiku wenye baraka nyingi, ambapo kwa kuteremshwa ndani yake kitabu hicho kitukufu, mambo uliyokadiriwa ulimwengu wa wanadamu yalipata sura na hali mpya; ni usiku ambao majaaliwa ya viumbe na yale ambayo Mola amewakadiria kwa muda wa mwaka mzima huandikwa; na kila jambo lenye umuhimu maalumu huainishwa na kuwekwa wazi. Aya hizi tulizosoma za Suratu-Dukhan zinaashiria nukta nyingine ya msingi, nayo ni kwamba Qur'ani imeteremshwa kwa ajili ya kutoa maonyo na indhari kwa watu, kama ilivyokuwa kwa vitabu vingine vya mbinguni vilivyotangulia, ambavyo navyo pia vililetwa kwa lengo hilohilo la kuwaonya na kuwapa indhari wanadamu ili wasije wakaiharibu na kuitumia vibaya rasilimali ya uhai waliyopewa. Kwa hakika tunaweza kusema kuwa, hii ni kaida na utaratibu wa kudumu aliouweka Allah SWT wa kutuma Mitume wake ili waje kutoa maonyo na indhari kwa madhalimu na waliopotoka; na Bwana Mtume Muhammad SAW ndiye kiungo cha mwisho kilichokamilisha na kufunga mkufu na silisili ya Manabii hao. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, katika utamaduni wa Kiislamu, baadhi ya nyakati zina utukufu na umuhimu mkubwa zaidi. Mfano wake ni Lailatul-Qadr, ambao ni usiku wa kuteremshwa Qur'ani na wa kuainishwa majaaliwa ya waja. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, wakati wa usiku una hadhi maaluumu kwa ajili ya utukukaji na ujengekaji kimaanawi wa mwanadamu. Na ndiyo maana imeusiwa sana katika mafunzo ya Qur'ani kufanya ibada na kunong'ona na Allah katika wakati huo. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, katika jamii ambayo watu wake wameghafilika mno, maonyo na indhari yanahitajika zaidi na huwa na athari kubwa zaidi kuliko kuwaaidhi watu kwa njia ya kuwapa matumaini na bishara njema.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 5 na ya 6 ambazo zinasema:

أَمْرًا مِّنْ عِندِنَا ۚ إِنَّا كُنَّا مُرْسِلِينَ

Ndiyo hukumu itokayo kwetu. Hakika Sisi ndio wenye kutuma.

رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ

Ni rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.

Aya hizi zinaendeleza yaliyozungumziwa katika aya zilizotangulia kuhusu kuteremshwa kwa Qur'ani na kueleza kwamba: kuteremshwa Qur'ani na kubaathiwa yaani kutumwa Bwana Mtume SAW kufikisha risala ya unabii, yote mawili yametokana na amri ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na yanatokana na takrima na rehma zake Mola kwa waja wake. Ni wazi kuwa, neema za kimaada ambazo Allah SWT amemruzuku mwanadamu huwa zinakamilika pale zinapoandamana na uongofu wa kumfikisha kiumbe huyo kwenye saada na fanaka; na uongofu huo hawezi kuufikia mwanadamu bila ya kuletwa kitabu cha mbinguni pamoja na Mtume anayetokana na wanadamu wenyewe, ambaye atakuwa ruwaza na kigezo cha wao kuiga na kufuata. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Qur'ani yote na kwa ukamilifu wake imeteremshwa na Allah SWT; na ni maneno yake Yeye Mola, si maneno ya Nabii Muhammad SAW. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kuteremshwa kitabu peke yake hakutoshi. Kitabu chenyewe kinahitaji mbainishaji, atakayekuwa pia mfano na kigezo cha kuigwa na kufuatwa kivitendo kwa yale yaliyomo ndani yake. Hapana shaka Mitume ndio waliokuwa watekelezaji wa majukumu hayo. Halikadhalika tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, wito wa wahyi na uongofu kwa wanadamu ni miongoni mwa madhihirisho ya rehma za Mwenyezi Mungu, japokuwa kwa masikitiko, akthari ya watu wameamua kuzinyima na kuzikosesha nafsi zao rehma hiyo.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 7 na ya 8 za sura yetu ya Ad-Dukhan ambazo zinasema:

رَبِّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا ۖ إِن كُنتُم مُّوقِنِينَ

Mola Mlezi wa mbingu na ardhi na vilivyomo baina ya viwili hivyo, ikiwa nyinyi mna yakini.

لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ ۖ رَبُّكُمْ وَرَبُّ آبَائِكُمُ الْأَوَّلِينَ

Hakuna mungu ila Yeye; anahuisha na anafisha, Mola Mlezi wenu na Mola Mlezi wa baba zenu wa mwanzo.

Miongoni mwa imani na itikadi potofu ambazo walikuwa nazo washirikina ni kuamini kuwepo miungu maalumu inayoendesha mbingu na ardhi na vitu vingine vya maumbile kama upepo na mvua, mpaka wakafika hadi kuziabudu nembo za miungu hiyo. Aya hizi tulizosoma zinaivunja hoja hiyo potofu na imani hizo batili na kusisitiza kuwa, mwendeshaji wa mambo yote ya dunia na Mola wa ulimwengu wote wa maumbile ni huyohuyo Muumba wa viumbe vyote, ambaye ni mmoja tu, si zaidi yake; kwa hivyo hakuna maana ya kuwepo mwingine wa kuabudiwa ghairi yake Yeye tu. Kama mtu anataka apate yakini ya kumjua Mwenyezi Mungu, basi njia ya wazi zaidi na ya kufikia yakini kamili juu yake Yeye, ni ya mtazamo wa Umoja na Upekee wake. Kwa sababu athari na ishara za Umoja, Upekee wa Allah na kuwa kwake Mlezi wa kila tu unashuhudiwa katika kila chembe mojamoja ya vitu vilivyopo katika ulimwengu wa uumbaji. Kwa hivyo inapasa tumuelekee na kumwabudu Yeye tu. Yeye si Mola Muumba wa ulimwengu tu, bali ni Mola aliyekuumbeni nyinyi, baba zenu waliotangulia pamoja na wanadamu wote, kuanzia mwanzo wenu hadi sasa; hakuna mwabudiwa wa haki isipokuwa Yeye; na uhai na mauti ya wanadamu wote yako mikononi mwake. Hakuna shaka yoyote, uhai na mauti ni masuala yenye umuhimu mkubwa mno. Kwa sababu kama kuna mambo yenye taathira kubwa zaidi katika maisha ya wanadamu na wakati huohuo yaliyo tata zaidi kuhusiana na ulimwengu wa maumbile, na yaliyo hoja wadhiha na ya wazi zaidi ya kuthibitisha uwezo wa Mwenyezi Mungu, basi ni hilo la uhai na mauti ya viumbe. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, Muumba, Mmiliki na Mtawala wa ulimwengu ni mmoja; na ulimwengu wote wa maumbile unaendeshwa kwa tadbiri na ulezi wa ujudi mmoja tu, ambao ni Mwenyezi Mungu Mmoja na wa Pekee. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, mteremshaji wa kitabu cha mbinguni, ndiye huyuhuyo Muumba wa mbingu na ardhi na vitu vingine vyote; na taratibu za sharia alizoweka zinawiyana na kanuni za maumbile. Wa aidha tunajielimisha kutokana na aya hizi kwamba, badala ya kufuata mila na imani potofu za waliotangulia, watu wafuate na kutii maamrisho ya Mwenyezi Mungu, ambaye ndiye Muumba wao na wa wazee wao waliopita. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 909 ya Qur'ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azifanye thabiti imani zetu, atughufirie madhambi yetu na aufanye mwema mwisho wetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.../