May 24, 2023 16:00 UTC

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SW, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 910 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 44 ya ad-Dukhan. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 9 hadi ya 11 ya sura hiyo ambazo zinasema:

بَلْ هُمْ فِي شَكٍّ يَلْعَبُونَ

Lakini wao wamo katika shaka wakicheza.

فَارْتَقِبْ يَوْمَ تَأْتِي السَّمَاءُ بِدُخَانٍ مُّبِينٍ

Basi ingoje siku ambayo mbingu italeta moshi ulio dhaahiri,

يَغْشَى النَّاسَ ۖ هَٰذَا عَذَابٌ أَلِيمٌ

Utakao wafunika watu: Hii ni adhabu iumizayo!

Katika darsa iliyopita tulisoma aya zilizozungumzia kuteremshwa kwa Qur'ani na kubaathiwa Mitume kwa ajili ya kuwaelekeza watu kwenye uongofu, ambayo ni ishara mojawapo ya rehma kubwa za Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Aya tulizosoma zinasema: lakini licha ya kufikiwa na rehma hiyo, baadhi ya watu, pamoja na kuitambua haki, hawako tayari kuifuata, bali hujaribu kila mara kuzitia shaka nafsi zao na za wenzao. Badala ya kuachana na shaka na kuweza kuifikia hakika na yakini juu ya haki, wanazishughulisha nafsi zao na mambo ya kutia shaka huku wakiufanyia mchezo ukweli wa mafundisho matukufu ya kitabu cha mbinguni. Kisha aya zinawaonya makafiri hao wakaidi na wapinzani wakubwa wa haki kwamba, mtakapoziona ishara za adhabu ya Mwenyezi Mungu, utando wa mghafala uliogubika macho yenu utaondoka; mtabaini kosa lenu kubwa mlilofanya na mtafahamu kuwa waliyokuambieni Mitume wa Mwenyezi Mungu yalikuwa sahihi na ya kweli, wala si khurafa na maneno ya upuuzi. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, shaka haipasi kuwa chanzo cha kumtia mtu mghafala na udumavu. Kilicho kibaya na kisicho sahihi ni mtu kuselelea kwenye shaka; ama kuwa na shaka ya jambo ndivyo yalivyo hasa maumbile ya akili ya mwanadamu. Inachopasa kufanya ni kuchunguza na kuhakiki, ili kuondoa shaka iliyopo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kupumbazika na kushughulishwa na kauli za watu wanaochochea na kujenga shaka juu ya mambo yanayohusu imani za dini na kuzifanyia mchezo aya za Mwenyezi Mungu kutampatisha mtu adhabu kali.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 12 hadi 14 ambazo zinasema:

رَّبَّنَا اكْشِفْ عَنَّا الْعَذَابَ إِنَّا مُؤْمِنُونَ

Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu hii. Hakika tutaamini. 

أَنَّىٰ لَهُمُ الذِّكْرَىٰ وَقَدْ جَاءَهُمْ رَسُولٌ مُّبِينٌ

Kutafaa nini kukumbuka kwao? Na alikwisha wafikia Mtume mwenye kubainisha?

ثُمَّ تَوَلَّوْا عَنْهُ وَقَالُوا مُعَلَّمٌ مَّجْنُونٌ

Na wao wakamgeuzia uso, na wakasema: Huyu amefunzwa, naye ni mwendawazimu.

Ni kawaida kwamba wamkanushao Mwenyezi Mungu wanapodhihirikiwa na ishara za adhabu yake Mola, nafsi zao hujawa na woga, hofu na mshtuko; wakamlilia hali Mwenyezi Mungu na kumwambia: Ewe Mola, tuondolee adhabu, sisi tutaiamini haki. Hali ya kuwa imani inayotokana na woga na hofu haina thamani yoyote. Kwa kweli imani yenye thamani ni ile itokanayo na hiari ya mtu; na si ile anayoitamka kuwa nayo kwa sababu ya woga na mashinikizo ya nje ya nafsi yake. Kisha aya zinaendelea kueleza kwamba: kuzinduka na kumrudia Mola wenu kwa namna hiyo hakukufaeni kitu, kwa sababu wakati Mtume alipokujieni na miujiza na hoja wadhiha na za wazi, badala ya kuyakubali maelekezo yake na kumwamini Mungu mmoja pekee wa haki, mliipa kisogo haki. Mafundisho yake yake ya uongofu mliyanasibisha na watu wengine na hamkuwa tayari kuyakubali kuwa ni wahyi na maneno ya Mwenyezi Mungu. Kuna wakati mlikuwa mkisema yeye anawasiliana na majini na wao ndio waliomfunza yale ayasemayo. Na wakati mwingine mkasema, maneno anayokuambieni amefunzwa na watu wengine kisha yeye anayanasibisha na Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, wale ambao leo wanaifanyia shere na mchezo dini, iko siku macho yao yatakuja fumbuka na utando wa mghafala na shaka uliokuwa umeyagubika utaondoka na watabainikiwa na hakika. Hapo wataomba warudi tena duniani, lakini ombi lao halitakubaliwa. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Mwenyezi Mungu hawaadhibu makafiri na wakanushaji mpaka awe ametimiza dhima yake juu yao. Wa aidha aya hizi zinatuonyesha kwamba, badala ya makafiri kutoa hoja na sababu za kimantiki za kuyakataa maneno ya Mitume, wanachofanya ni kujaribu kuchafua na kutia doa shakhsia za waja hao wateule kwa kuwavurumizia tuhuma na maneno ya uzushi. Zifuatazo sasa ni aya za 15 na 16 ambazo zinasema:

إِنَّا كَاشِفُو الْعَذَابِ قَلِيلًا ۚ إِنَّكُمْ عَائِدُونَ

Hakika tutaiondoa adhabu kidogo, (lakini) nyinyi kwa yakini, mtarudia!

يَوْمَ نَبْطِشُ الْبَطْشَةَ الْكُبْرَىٰ إِنَّا مُنتَقِمُونَ

Siku tutakayo shambulia mshambulio mkubwa, hakika Sisi ni wenye kutesa. 

Baada ya madai ya makafiri ambao walipoziona ishara za adhabu walisema, sasa wako tayari kuiamini haki, aya tulizosoma zinasema: sisi tunawaondolea kidogo adhabu lakini hawapati ibra na mazingatio. Kwani hurejea tena kwenye ukafiri wao na matendo yao maovu na wala hawajuti kwa mabaya wanayotenda.  Kwa maneno mengine ni kwamba, kama pale makafiri inapowanyaka adhabu kutokana na matendo yao wanaonyesha majuto na wanaamua wabadilike, hilo huwa ni jambo la muda na la kupita tu; kwa sababu inapotulia tufani na dhoruba ya misukosuko wanayotiwa, huyarudia tena yaleyale waliyokuwa wakiyafanya. Basi kuonyesha kwao wameamini kunatokana na woga tu na wala hakuna thamani yoyote. Kwa hivyo, ikiwa itatokea kuhafifishiwa adhabu hapa duniani, adhabu kubwa na kali mno inawangojea huko akhera. Sababu ni kuwa, madhalimu wameghadhibikiwa na Mwenyezi Mungu na wala hawawezi kusalimika na adhabu yake. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, si hasha ikawa imetokea mara nyingi Mwenyezi Mungu akafumbia macho mabaya tunayofanya na kutotuadhibu katika dunia hii ili tujirekebishe, lakini sisi wenyewe tukaamua kuendelea kufanya maovu na madhambi hayo. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, Allah SWT ni mwenye kuwahami Mitume na waumini na atawaadhibu makafiri na madhalimu kwa sababu ya dhulma walizofanya kuhusiana na Mitume na waja wake waumini.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 17 na 18 ambazo zinasema:

وَلَقَدْ فَتَنَّا قَبْلَهُمْ قَوْمَ فِرْعَوْنَ وَجَاءَهُمْ رَسُولٌ كَرِيمٌ

Na hakika kabla yao tuliwafanyia mtihani watu wa Firauni, na aliwafikia Mtume aheshimiwaye. 

أَنْ أَدُّوا إِلَيَّ عِبَادَ اللَّهِ ۖ إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ

Akasema: Nipeni waja wa Mwenyezi Mungu; kwa hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu. 

Baada ya aya zilizotangulia kuzungumzia namna washirikina wa Makka walivyoamiliana na Bwana Mtume Muhammad SAW, aya hizi za 17 na 18 za Suratu-Dukhan zinaashiria yaliyojiri baina ya Nabii Musa (as) na Firauni. Inafaa tukumbushe hapa kuwa, kaumu ya Firauni ilifikia kilele cha uwezo na nguvu kutokana na kuwa na utawala madhubuti, utajiri mkubwa wa mali na suhula chungu nzima zisizo na kifani. Lakini nguvu na mamlaka hayo yaliwatia ghururi na majivuno watu wa kaumu hiyo wakaghariki kwenye lindi la madhambi ya kila aina, pamoja na dhulma na uonevu dhidi ya watu. Ilikuwa ni katika mazingira hayo, Nabii Musa (as) aliwaendea watu wa kaumu hiyo; na kwa lugha ya upole na heshima akamtaka Firauni na watu wake wawaachie huru watu wa kaumu yake ya Bani Israil, ambao walikuwa wamewageuza watumwa na wajakazi wao, ili kwa kuwalingania wito wa Mwenyezi Mungu, awaelekeze kwenye uongofu utakaowafikisha kwenye saada. Miongoni mwa mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, jukumu la kwanza la Mitume ni kuwakomboa watu kwa kuwatoa kwenye minyororo ya madhila ya ubeberu wa watawala madhalimu na watumiaji mabavu na kuwaokoa wanyonge na wanaodhulumiwa kwa unyonyaji na utumikishwaji. Ni kwa mantiki hiyo, Nabii Musa (as) alimwendea Firauni na watu wa utawala wake kabla ya kuwafuata watu wa kaumu yake ya Bani Israil. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa Mitume, walikuwa watu waaminifu waliokubaliwa na kuaminiwa na watu. Asili yao ya kuwa waja safi na wema ilichangia kuaminiwa kupewa jukumu la Utume na kuwafanya watu pia waukubali wito wao. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 910 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah atuonyeshe haki na atupe taufiki ya kuifuata na atuonyeshe batili na atuwezeshe kuiepuka. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/