May 27, 2023 04:51 UTC
  • Sura ya Muhammad, aya ya 29-32 (Darsa ya 934)

Wasikilizaji wapenzi wa Darsa ya Qur’ani, Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh. Bismillahir Rahmanir Rahim. Hamdu na sifa zote njema zinamstahikia Allah SWT, na rehma na amani zimshukie Mtume wake Mtukufu na Aali zake watoharifu.

Kwa taufiki yake Mola Karima aliyetupa uhai na uzima tumekutana tena katika mfululizo mwengine wa Darsa ya Qur’ani. Hii ni darsa ya 934 na sura tunayoizungumzia hivi sasa ni ya 47 ya Muhammad. Tunaianza darsa yetu kwa aya ya 29 na 30 za sura hiyo ambazo zinasema:

أَمْ حَسِبَ الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ أَن لَّن يُخْرِجَ اللَّهُ أَضْغَانَهُمْ

Je! Wenye maradhi nyoyoni mwao wanadhani kwamba Mwenyezi Mungu hatazidhihirisha chuki zao?

وَلَوْ نَشَاءُ لَأَرَيْنَاكَهُمْ فَلَعَرَفْتَهُم بِسِيمَاهُمْ ۚ وَلَتَعْرِفَنَّهُمْ فِي لَحْنِ الْقَوْلِ ۚ وَاللَّهُ يَعْلَمُ أَعْمَالَكُمْ

Na kama tungependa tungekuonyesha hao na ungeli watambua kwa alama zao; na bila ya shaka utawajua kwa namna ya msemo (wao). Na Mwenyezi Mungu anavijua vitendo vyenu.

Katika darsa iliyopita tuliwazungumzia wanafiki, ambao badala ya kufanya yanayomridhisha Mwenyezi Mungu, wanayaendea yale yanayozipendeza nafsi zao, japokuwa hayampendezi na hayamridhishi Yeye Mola Mwenye Enzi. Aya hizi tulizosoma zinazungumzia alama nyingine za watu hao kwa kusema: Wao sio tu hawapendezwi na Mtume SAW na mafundisho yake, bali hata nyoyoni mwao wana chuki na uadui na mjumbe huyo wa Allah pamoja na waumini. Kidhahiri wanaonesha wameamini na wako pamoja na waumini, lakini wanapenda kuwa na mahusiano na ushirikiano na maadui ili waweze kufanikisha maslahi yao ya kimaada na ya kidunia. Badala ya kusimama imara kukabiliana na njama za maadui, wanaungana na kushirikiana nao kwa kauli na matendo yao na kuudhoofisha upande wa waumini.  Tab'an kama Allah SWT atataka, bila shaka anaweza akajaalia ikadhihirika alama au ishara fulani katika nyuso zao ili watu wote wawatambue kwa alama hiyo waliyonayo kwenye nyuso. Lakini mipango ya Mwenyezi Mungu haiko hivyo, kwamba azidhihirishe batini na hakika za watu hapa duniani. Hata hivyo waumini walio werevu wanaweza kubaini batini zao kutokana na kauli na uzungumzaji wao na hivyo kuutambua unafiki wa watu hao. Ni kama pale inapotolewa amri ya kupigana Jihadi, ambapo wao hutoa kauli za kuvunja moyo zinazowafanya waumini wasiende kwenye Jihadi; na au husema maneno ya kuzikuza nguvu na suhula za adui kiasi cha kuwaogopesha na kuwatia hofu watu wasijitokeze kwenye medani ya mapambano. Wanafiki hao wasijidhani kama wao ni watu werevu na wajanja. Kwa sababu Allah SWT anayaelewa vyema yaliyomo nyoyoni mwao na mambo wayafanyayo dhidi ya Waislamu; kwa hivyo atawaadhibu pale utakapofika wakati mwafaka. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hizi ni kwamba, inapasa tuzichunge nyoyo na roho zetu; na wala tusidhani kwamba, kama tuna nia mbaya na dhamira chafu zitaweza kufichika milele. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hizi ni kuwa, kinyongo na uhasidi ni miongoni mwa mambo yanayoibua maradhi ya unafiki na mtu kuwa na nyuso mbili. Tusiwe na vinyongo na waumini, kwani hiyo ni katika alama za wanafiki. Vilevile aya hizi zinatuelimisha kwamba, hulka na dhati ya nafsi ya mtu inaathiri pia sura na dhahiri yake. Kwa maneno mengine ni kwamba, kwa kiwango fulani, sura na kauli za mtu zinabainisha dhamiri na batini yake, hata kama atajaribu kuficha hakika ya nafsi yake.

Tunaiendeleza darsa yetu kwa aya ya 31 ya sura yetu ya Muhammad ambayo inasema:

وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّىٰ نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ

Na bila ya shaka tutakujaribuni mpaka tuwadhihirishe wapiganao Jihadi katika nyinyi na wanao subiri. Nasi tutazifanyia mtihani khabari zenu.

Aya hii inazungumzia moja ya kaida na utaratibu muhimu aliouweka Allah SWT kuhusiana na wanadamu na hasa waumini na kueleza kwamba, wanaodai kuwa wameamini ni wengi mno; kwa sababu hiyo, Yeye Mola amewapangia waja wake njia na mambo mbalimbali ya kuwatahini ili ibainike ni nani walio wakweli wa madai yao kwamba wamemwamini Allah na nani walio waongo. Na hii ni kwa ajili ya kupambanuka wale ambao wanapofikwa na shida na misukosuko hupoteza imani wakaiacha dini yao, na wale ambao hata wanapofikwa na masaibu na mitihani mikubwa kabisa wanabaki imara na thabiti katika imani na msimamo wao. Ni kawaida kwamba katika hali ngumu na ya misukosuko, wanafiki hushindwa kuficha batini na dhati yao, kwa hivyo huwa wanafanya mambo yanayofichua siri zilizofichikana ndani ya nafsi zao wakatambulika na kufedheheka. Miongoni mwa tunayojifunza kutokana na aya hii ni kwamba, Mwenyezi Mungu anawatahini wanaodai kuwa wameamini, ili wao wenyewe waweze kujifahamu ni wakweli kwa kiwango gani katika madai yao na vilevile watu waweze kuwatambua wana imani kiasi gani juu ya Mwenyezi Mungu na dini yake. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, subira na istikama na kusimama imara katika njia ya dini na kuvumilia misukosuko inayojitokeza katika njia hiyo ni miongoni mwa alama za kuwa muumini wa kweli. Wa aidha aya hii inatutaka tujue kwamba, kipimo cha imani ni kutoyumba na kuwa thabiti wakati wa shida na matatizo, kwa sababu wakati wa raha na wepesi, akthari ya watu hujigamba kuwa ni waumini wa kweli.

Darsa yetu ya leo inahitimishwa na aya ya 32 ambayo inasema:

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّهِ وَشَاقُّوا الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْهُدَىٰ لَن يَضُرُّوا اللَّهَ شَيْئًا وَسَيُحْبِطُ أَعْمَالَهُمْ

Kwa hakika walio kufuru na wakazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wakapinzana na Mtume baada ya kwisha wabainikia uwongofu, hao hawatamdhuru Mwenyezi Mungu kwa lolote. Naye ataviangusha vitendo vyao. 

Aya hii inaendeleza maudhui ya aya zilizotangulia zilizowazungumzia wanafiki kwa kuashiria usuli na kanuni moja kuu, nayo ni kwamba, watu wote waliokufuru, wawe ni makafiri wanaodhihirisha ukafiri wao kwa ndimi zao, au wanafiki wanaoficha ukafiri wao ndani ya nyoyo zao, makundi yote hayo mawili yana uadui na Allah na Mtume wake. Ijapokuwa haki imewabainikia watu hao na wanaelewa fika kwamba dini na njia anayowalingania Bwana Mtume SAW ni ya haki, lakini wanasimama kuipinga na kuipiga vita. Wao wanadhani kwamba, wanaweza kuidhuru dini ya Allah na kuizuia isienee; hali ya kuwa irada na hukumu yake Mola ni kuona dini ya nuru, ya haki na uongofu ya Uislamu inastawi na kuenea; na ukafiri na unafiki unatoweka na kuangamia. Baadhi ya mafunzo tunayopata kutokana na aya hii ni kwamba, ukaidi na kuifanyia inadi haki na kumuasi Allah SWT havina mwisho mwingine isipokuwa hasara na maangamizi. Funzo jengine tunalopata kutokana na aya hii ni kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametimiza dhima kwa waja wake kwa kuwawekea nyenzo na sababu za kuufikia uongofu, kwa hivyo wanachopaswa kufanya watu ni kuitambua haki na kuifuata. Halikadhalika aya hii inatutaka tujue kwamba mipango na njama za makafiri na wanafiki hazitafika popote; na kinyume chake, dini ya Allah ya Uislamu itaendelea kustawi na kuenea siku baada ya siku. Wapenzi wasikilizaji, darsa ya 934 ya Qur’ani imefikia tamati. Tunamwomba Allah azitakase na unafiki nyoyo zetu, aziepushe na ria amali zetu na azihifadhi na uongo ndimi zetu. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/