May 28, 2023 08:03 UTC
  • Maonyesho ya kiteknolojia ya Iran

Hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kujiunga nami katika makala hii ambayo huangazia baadhi ya mafanikio katika uga wa sayansi, tiba na teknolojia nchini Iran na maeneo mengine duniani. Ni matumaini yangu kuwa mtaweza kunufaika.

Toleo la 12 la Iran la Kitekonolojia la INOTEX 2023 ambalo linajumuisha maonyesho ya Kimataifa ya Ubunifu na Teknolojia limefanyika  mwezi Mei 2023, katika Bustani ya Teknolojia ya Pardis (PTP) jijini Tehran.

Makampuni zaidi ya 400 ya ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia yameshiriki katika maonyesho hayo.

Sehemu muhimu zaidi ya maonyesho ya mwaka huu ilikuwa katika uga wa ndege zisizo na rubani.

Kitengo cha Sayansi na Teknolojia cha Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad, kwa kuzingatia dhamira yake maalum na mwingiliano maalum na Bustani ya Teknolojia ya Pardis, huandaa hafla ya kila mwaka ya kitaifa ya teknolojia mpya katika uwanja wa ndege zisizo na rubani au UAV's .

Madhumuni ya maonyesho ya Innotex 2023 yalikuwa ni kutambua kampuni za kibunifu na za kiteknolojia.

INOTEX haifanyiki tu kutambulisha bidhaa na kuunda ushirikiano, bali pia kutoa maarifa mbalimbali kuhusu bei za hivi punde za ushindani wa kimataifa, viwango vya ubora, maendeleo, matokeo ya kisayansi na mawazo ya kiuchumi na teknolojia.

Makamu wa Rais wa Iran katika Masuala ya Sayansi, Teknolojia na Uchumi wa Kiteknolojia amesema: msaada maalum umezingatiwa kwa makampuni mapya yanayotegemea teknolojia ili kuunda sekta yenye manufaaa na faida.

Akitoa hotuba katika hafla ya uzinduzi wa tukio la Innotex 2023, Rouhollah Dehghani Firouzabadi alisema: Leo, sekta ya teknolojia nchini inastawi na imeandaa fursa ya kusaidia mashirika kustawi.

Wakati huo huo, Maafisa wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) wamesema hivi karibuni kwamba kwa kuzingatia ukweli kwamba mpango wa nyuklia wa Iran unaendelezwa na wataalamu wa ndani ya nchi, vitisho vya kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran havina maana.  

Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran Behroz Kamalvandi amesema kuzingatia ukweli kwamba sekta ya nyuklia inaendelezwa kwa kuwategemea wataalamu na wanasayansi wa ndani ya nchi, vitisho vya maadui dhidi ya sekta haviwezi kuyumbisha nchi. Kamalvandi aliyasema hayo katika kikao cha wanadiplomasia wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi kilichofanyika katika Wizara ya Mambo ya Nje. 

Aidha amesema, "Sekta ya nyuklia inafanya kazi kama nguvu katika tasnia nyingine tofauti na haikomei katika nyanja maalum ya uzalishaji nishati. Teknolojia ya nyuklia ya Iran inatumika katika sekta kama vile matibabu, uzalishaji dawa, kilimo na viwanda mbali mbali.

@@@

Kampeni kubwa zaidi barani Afrika ya chanjo dhidi ya polio tangu 2020 inaanza Mei 26 katika nchi tatu za Afrika Magharibi na Kati, katika juhudi za pamoja za mamlaka ya kitaifa ya kutoa chanjo kwa watoto milioni 21 walio chini ya umri wa miaka mitano.

Taarifa iliyotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani Kanda ya Afrika, WHO Afrika huko mjini Brazzaville, Jamhuri ya Kongo,  imeeleza zoezi hilo linaanzia nchini Cameroon, Chad na Niger kabla ya kuongezwa hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati  na linakuja kudhibiti ugunduzi 19 wa virusi vya polio vya aina ya 2 katika nchi hizo; wagonjwa 2 nchini Niger, wagonjwa 10 nchini Chad, wagonjwa 4 nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati na wagonjwa 3 nchini Cameroon.

Mkakati huo wa nchi nyingi unaungwa mkono na WHO kupitia Mpango wa Kutokomeza Polio Duniani (GPEI), na unajumuisha chanjo zilizounganishwa na pia mipango ya pamoja katika jumuiya za mpakani kukomesha maambukizi ya polio.

Dkt Matshidiso Moeti, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika amesema, "Hili ni jukumu muhimu la kuziba mapengo ya chanjo kutokana na janga la COVID-19 na litawapa mamilioni ya watoto ulinzi muhimu kutokana na hatari ya kupooza kwa ugonjwa wa kupooza." Aidha ameongeza kuwa "Kuunganisha kampeni hiyo kutahakikisha kuwa kundi kubwa la watoto katika nchi zote nne wanapokea chanjo hiyo kwa wakati mmoja ili kuimarisha kinga ya polio katika eneo pana la kijiografia."

Eneo la bonde la Ziwa Chad linakabiliana na mojawapo ya matukio ya muda mrefu zaidi ya ghasia za kutumia silaha duniani. Pia ni nyumbani kwa idadi kubwa zaidi ya watoto wanaotambulika kwa mawasiliano ya chanjo kama "dozi sifuri" ulimwenguni, ambao hawajachanjwa au walichanjwa kidogo

Nchi zote nne zimefanya juhudi kubwa kuimarisha utambuzi wa polio, kuzuia kuenea kwa virusi na kuwalinda watoto dhidi ya hatari ya kuambukizwa na kupooza kwa maisha yote. Hata hivyo, licha ya kwamba wote wamethibitishwa kuwa hawana virusi vya polio mwitu lakini polio aina ya 2 inaendelea. 

Katika nchi zote, serikali zimeendelea kuboresha ubora wa shughuli za chanjo, zikiimarishwa na utekelezaji mpana wa kampeni za ziada za chanjo. Haya yanalengwa katika kushughulikia hatari zilizobaki za aina zote za virusi vya polio, huku pia zikiimarisha chanjo ya kawaida katika ngazi ya nchi. 

Aidha, usambazaji chanjo wa nyumba kwa nyumba umewapunguzia wazazi mzigo wa kuwasafirisha watoto wao katika vituo vya afya kupata chanjo. Wafanyakazi wa afya, kwa usaidizi kutoka kwa WHO, sasa pia wanatoa chanjo majumbani, na pia katika vituo vya kidini, sokoni na shuleni. 

Viongozi wa dini na jamii, kama mabingwa wa kutokomeza virusi vya polio, pia husaidia kuhamasisha walezi kuwachanja watoto wao sio tu dhidi ya polio, lakini magonjwa yote yanayoweza kuzuilika. 

Muhimu, data za kuaminika ni muhimu kwa ufuatiliaji wa magonjwa na hatua dhidi ya mlipuko. Kufuatia milipuko inayoendelea ya virusi vya polio vinavyozunguka, nchi pia zimeongeza ufuatiliaji ili kugundua visa. 

@@@

Na Naibu Spika wa Bunge la Uganda, Thomas Tayebwa anasema mustakabali wa Uganda unategemea sayansi, teknolojia na uvumbuzi.
Akitoa mada katika makabidhiano ya vifaa vya sayansi kwa shule 20 za msingi wilayani Mitooma hivi karibuni, Tayebwa aliipongeza wizara ya elimu na Serikali kwa kuwekeza katika masomo ya sayansi katika hatua za awali za elimu.
Alisema, "Ili kuipeleka nchi mbele na kubadilisha jamii kiuchumi, ni lazima tuthamini umuhimu wa sayansi na teknolojia ili kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi ya nchi yetu."
Tayebwa aliwataka walimu wakuu wa shule zilizonufaika kuhakikisha kuwa vifaa vya sayansi vinatumiwa kikamilifu na wanafunzi na pia kushirikiana na shule za jirani ambazo bado hazijanufaika na mpango huo.
Uganda imefufua juhudi za kupeleka sayansi, teknolojia na uvumbuzi kama vichocheo vya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii.
Hili linathibitishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2020/21 -2024/25 kuhusu Ubunifu na Maendeleo ya Teknolojia.

Lengo la programu hii ni kuongeza maendeleo, kupitishwa, uhamisho na biashara ya teknolojia na ubunifu kupitia maendeleo ya sayansi, teknolojia na uvumbuzi eco-mfumo ulioratibiwa vyema.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa ya Teknolojia na Ubunifu 2021 inahimiza mataifa yote yanayoendelea kujiandaa kwa kipindi cha mabadiliko ya kina na ya haraka ya kiteknolojia ambayo yataathiri pakubwa masoko na jamii.

Na tukiwa bado nchini Uganda, Wizara ya Sayansi na Teknolojia imesema, setilaiti ya PearlAfricaSat-1 ya nchi hiyo iliyotumwa anga za juu  Novemba mwaka  bado haijafanya kazi kikamilifu kutokana na kutokamilika mfumo wake wa kazi na ucheleweshaji wa ujenzi wa kituo cha ardhi kwa ajili ya kuamrisha, kudhibiti na kusimamia satelaiti hiyo. Bonny Omara, mhandisi mkuu wa mradi huo, aliwaambia waandishi wa habari katika mahojiano ya hivi majuzi kwamba wako mbioni  kutegeneza kituo cha ardhini ili kuweza kupokea moja kwa moja taarifa zinazotumwa satelaiti hiyo.

Waziri wa Sayansi na Teknolojia wa Uganda Monica Musenero alisema satelaiti hiyo ilikusudiwa kutoa data za utafiti na uchunguzi kwa ajili ya ufumbuzi wa utabiri wa hali ya hewa, usalama wa mpaka, ufuatiliaji wa kilimo, ardhi, vyanzo vya maji, mipango ya miundombinu, kuzuia maafa na ramani ya madini - lakini bado haiwezi kufanya haya yote. Satalaiti hiyo ya Uganda ilirushwa katika anga za mbali na shirika moja la Japan.

@@@

Naam na hadi hapo ndio tunafika mwisho